48
Manase na Efraimu
Baada ya muda Yusufu akaambiwa, “Baba yako ni mgonjwa.” Kwa hiyo akawachukua wanawe wawili Manase na Efraimu pamoja naye. Yakobo alipoambiwa, “Mwanao Yusufu amekuja kukuona,” Israeli akajitia nguvu, akaketi kitandani.
Yakobo akamwambia Yusufu, “Mungu Mwenyezi*Kiebrania El-Shaddai (yaani Mungu Mwenye utoshelevu wote). alinitokea huko Luzu katika nchi ya Kanaani. Akanibariki, naye akaniambia, ‘Nitakufanya ustawi na uongezeke kwa idadi. Nitakufanya kuwa jamii ya mataifa, nami nitakupa nchi hii uimiliki milele, wewe na wazao wako baada yako.’
“Sasa basi, wanao wawili waliozaliwa kwako huku Misri kabla sijaja hapa kwako watahesabiwa kuwa wangu; Efraimu na Manase watakuwa wangu, vile Reubeni na Simeoni walivyo wangu. Lakini watoto utakaowazaa baada yao watakuwa wako. Katika nchi watakayoirithi, watatambuliwa kwa jina la ndugu zao. Nilipokuwa ninarudi kutoka Padani, nilihuzunika sana kwa sababu Raheli alifariki katika nchi ya Kanaani tulipokuwa tukisafiri, tukiwa karibu kufika Efrata. Kwa hiyo nilimzika huko, kando ya njia iendayo Efrata” (yaani Bethlehemu).
Israeli alipowaona wana wa Yusufu, akauliza, “Hawa ni nani?”
Yusufu akamjibu baba yake, “Hawa ni wana ambao Mungu amenipa nikiwa huku.”
Ndipo Israeli akasema, “Walete kwangu ili niwabariki.”
10 Basi macho ya Israeli yalikuwa hayaoni vizuri kwa sababu ya uzee, naye aliona kwa shida. Kwa hiyo Yusufu akawaleta wanawe karibu na baba yake, naye Israeli akawabusu na kuwakumbatia.
11 Israeli akamwambia Yusufu, “Kamwe sikutazamia kuuona uso wako tena, lakini sasa Mungu ameniruhusu kuwaona watoto wako pia.”
12 Ndipo Yusufu akawaondoa wanawe magotini mwa Israeli, naye akasujudu, uso wake ukagusa chini. 13 Yusufu akachukua wale wana wawili, Efraimu kwenye mkono wake wa kuume akimwelekeza kwenye mkono wa kushoto wa Israeli, na Manase katika mkono wake wa kushoto akimwelekeza kwenye mkono wa kuume wa Israeli, akawaleta karibu na babu yao. 14 Lakini Israeli akaupeleka mkono wake wa kuume, akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, ingawa ndiye alikuwa mdogo; nao mkono wake wa kushoto, ukipishana na mkono wa kuume, akauweka juu ya kichwa cha Manase, ingawa Manase ndiye alikuwa mzaliwa wa kwanza.
15 Ndipo akambariki Yusufu akisema,
“Mungu ambaye baba zangu
Ibrahimu na Isaka walimtii,
Mungu ambaye amekuwa mchungaji
wa maisha yangu yote hadi leo,
16 Malaika ambaye aliniokoa kutoka madhara yote,
yeye na awabariki vijana hawa.
Na waitwe kwa jina langu
na kwa majina ya baba zangu
Ibrahimu na Isaka,
wao na waongezeke kwa wingi
katika dunia.”
17 Yusufu alipoona baba yake akiweka mkono wa kuume juu ya kichwa cha Efraimu, hakupendezwa, kwa hiyo akauchukua mkono wa baba yake kutoka kichwa cha Efraimu na kuuweka juu ya kichwa cha Manase. 18 Yusufu akamwambia, “Hapana, baba yangu, huyu ndiye mzaliwa wa kwanza; uweke mkono wako wa kuume juu ya kichwa chake.”
19 Lakini baba yake akakataa, akasema, “Ninajua, mwanangu, ninajua. Yeye pia atakuwa taifa, naye pia atakuwa mkuu. Hata hivyo, ndugu yake mdogo atakuwa mkuu kuliko yeye, nao wazao wake watakuwa kundi la mataifa.” 20 Akawabariki siku ile na kusema,
“Kwa jina lenu Israeli watatamka baraka hii:
‘Mungu na awafanye kama Efraimu na Manase.’ ”
Kwa hiyo akamtanguliza Efraimu mbele ya Manase.
21 Ndipo Israeli akamwambia Yusufu, “Ninakaribia kufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, na atawarudisha katika nchi ya baba zenu. 22 Kwako wewe, kama aliye juu ya ndugu zako, ninakupa sehemu moja zaidi ya ndugu zako, lile eneo nililoteka kwa Waamori kwa upanga wangu na upinde wangu.”

*48:3 Kiebrania El-Shaddai (yaani Mungu Mwenye utoshelevu wote).