Habakuki
1
1 Neno la unabii alilopokea nabii Habakuki.
Lalamiko la Habakuki
2 Ee Mwenyezi Mungu, hata lini nitakuomba msaada,
lakini wewe husikilizi?
Au kukulilia, “Udhalimu!”
lakini hutaki kuokoa?
3 Kwa nini unanifanya nitazame dhuluma?
Kwa nini unavumilia makosa?
Uharibifu na udhalimu viko mbele yangu;
kuna mabishano na mapambano kwa wingi.
4 Kwa hiyo sheria imepotoshwa,
nayo haki haipo kabisa.
Waovu wanawazunguka wenye haki,
kwa hiyo haki imepotoshwa.
Jibu la Mwenyezi Mungu
5 “Yatazame mataifa,
uangalie na ushangae kabisa.
Kwa sababu katika siku zako nitafanya kitu
ambacho hungeamini,
hata kama ungeambiwa.
6 Tazama! Nitawainua Wakaldayo,
watu wakatili na wenye haraka,
ambao hupita dunia yote
ili kuteka makazi yasiyo yao.
7 Ni watu wanoogopwa na wanaotisha;
wenyewe ndio sheria yao,
na huinua heshima yao wenyewe.
8 Farasi wao ni wepesi kuliko chui,
na wakali kuliko mbwa-mwitu wakati wa machweo.
Askari wapanda farasi wao huenda mbio;
waendesha farasi wao wanatoka mbali.
Wanaruka kasi kama tai
ili kurarua mawindo;
9 wote wanakuja tayari kutenda udhalimu.
Makundi yao wanasonga mbele
kama upepo wa jangwani,
na kukusanya wafungwa
kama mchanga.
10 Wanawabeza wafalme,
na kuwadhihaki watawala.
Wanaicheka miji yote yenye ngome;
wanalundika udongo na kuiteka hiyo miji.
11 Kisha wanapita kasi kama upepo na kusonga mbele:
watu wenye hatia, ambao nguvu zao ndio mungu wao.”
Lalamiko la pili la Habakuki
12 Ee Mwenyezi Mungu, je, wewe sio wa tangu milele?
Mungu wangu, Uliye Mtakatifu wangu, hatutakufa.
Ee Mwenyezi Mungu, umewachagua wao ili watekeleze hukumu;
Ee Mwamba, umewaamuru watuadhibu.
13 Macho yako ni safi mno hata yasiweze kuutazama uovu,
wala huwezi kuvumilia makosa.
Kwa nini basi unawavumilia wadanganyifu?
Kwa nini unakuwa kimya wakati waovu
wanawameza wale wenye haki
kuliko wao wenyewe?
14 Umewafanya watu kama samaki baharini,
kama viumbe wa bahari wasio na mtawala.
15 Adui mwovu anawavuta wote kwa ndoana,
anawakamata katika wavu wake,
anawakusanya katika juya lake;
kwa hiyo anashangilia na anafurahi.
16 Kwa hiyo anatoa sadaka kwa wavu wake,
na kuchoma uvumba kwa juya lake,
kwa kuwa kwa wavu wake anaishi kwa starehe,
na anafurahia chakula kizuri.
17 Je, aendelee kuwatoa walio katika wavu wake,
akiangamiza mataifa bila huruma?