3
Hukumu kwa Yerusalemu na Yuda
1 Tazama sasa, Bwana,
Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,
yu karibu kuwaondolea Yerusalemu na Yuda
upatikanaji wa mahitaji na misaada,
upatikanaji wote wa chakula na tegemeo lote la maji,
2 shujaa na mtu wa vita,
mwamuzi na nabii,
mwaguzi na mzee,
3 jemadari wa kikosi cha watu hamsini
na mtu mwenye cheo, mshauri,
fundi stadi na msihiri mjanja.
4 Nitawafanya wavulana wawe viongozi wao;
watoto ndio watakaowatawala.
5 Watu watadhulumiana:
mtu dhidi ya mtu, na jirani dhidi ya jirani yake.
Kijana atainuka dhidi ya mzee,
mtu mnyonge dhidi ya mtu mwenye heshima.
6 Mtu atamkamata mmoja wa ndugu zake
katika nyumba ya baba yake na kusema,
“Unalo joho, sasa uwe kiongozi wetu,
tawala lundo hili la magofu!”
7 Lakini siku hiyo atapiga kelele akisema,
“Sina msaada.
Sina chakula wala mavazi katika nyumba yangu,
msinifanye niwe kiongozi wa watu.”
8 Yerusalemu inapepesuka,
Yuda inaanguka;
maneno yao na matendo yao ni kinyume na Mwenyezi Mungu,
wakiudharau uwepo wake uliotukuka.
9 Nyuso zao zinavyoonekana zinashuhudia dhidi yao,
hujivunia dhambi yao kama Sodoma,
wala hawaifichi.
Ole wao!
Wamejiletea maafa juu yao wenyewe.
10 Waambie wanyofu itakuwa heri kwao,
kwa kuwa watafurahia tunda la matendo yao.
11 Ole kwa watu waovu! Maafa yapo juu yao!
Watalipwa kwa ajili ya yale mikono yao iliyotenda.
12 Vijana wanawatesa watu wangu,
wanawake wanawatawala.
Enyi watu wangu, viongozi wenu wanawapotosha,
wanawapoteza njia.
13 Mwenyezi Mungu anachukua nafasi yake mahakamani,
anasimama kuhukumu watu.
14 Mwenyezi Mungu anaingia katika hukumu
dhidi ya wazee na viongozi wa watu wake:
“Ninyi ndio mlioharibu shamba langu la mizabibu,
mali iliyonyang’anywa maskini imo nyumbani mwenu.
15 Mnamaanisha nini kuwaponda watu wangu
na kuzisaga nyuso za maskini?”
asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
16 Mwenyezi Mungu asema,
“Wanawake wa Sayuni wana kiburi,
wanatembea na shingo ndefu,
wakikonyeza kwa macho yao,
wanatembea kwa hatua za madaha,
wakiwa na mapambo ya njuga kwenye vifundo vya miguu yao.
17 Kwa hiyo Bwana ataleta majipu kwenye vichwa vya wanawake wa Sayuni;
Mwenyezi Mungu atazifanya ngozi za vichwa vyao kuwa vipara.”
18 Katika siku ile Bwana atawanyang’anya uzuri wao: bangili, tepe za kichwani, mikufu yenye alama za mwezi mwandamo, 19 vipuli, vikuku, shela, 20 vilemba, mikufu ya vifundo vya miguu, mshipi, chupa za manukato na hirizi, 21 pete zenye muhuri, pete za puani, 22 majoho mazuri, mitandio, mavazi, kifuko cha kutilia fedha, 23 vioo, mavazi ya kitani, taji na shali.
24 Badala ya harufu ya manukato kutakuwa na uvundo;
badala ya mishipi, ni kamba;
badala ya nywele zilizotengenezwa vizuri, ni upara;
badala ya mavazi mazuri, ni magunia;
badala ya uzuri, ni alama ya aibu kwa chuma cha moto.
25 Wanaume wako watauawa kwa upanga,
nao mashujaa wako watauawa vitani.
26 Malango ya Sayuni yataomboleza na kulia,
ataketi mavumbini akiwa fukara.