12
Kushukuru na kusifu
Katika siku ile utasema:
“Nitakusifu wewe, Ee Mwenyezi Mungu.
Ingawa ulinikasirikia,
hasira yako imegeukia mbali
nawe umenifariji.
Hakika Mungu ni wokovu wangu;
nitamtumaini wala sitaogopa.
Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu,
ni nguvu zangu na wimbo wangu;
amekuwa wokovu wangu.”
Kwa furaha mtachota maji
kutoka visima vya wokovu.
Katika siku hiyo mtasema:
“Mshukuruni Mwenyezi Mungu, mliitie jina lake;
julisheni miongoni mwa mataifa yale aliyoyafanya,
tangazeni kuwa jina lake limetukuka.
Mwimbieni Mwenyezi Mungu, kwa kuwa ametenda mambo makuu,
hili na lijulikane duniani kote.
Pazeni sauti mwimbe kwa furaha, watu wa Sayuni,
kwa maana mkuu ni yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli miongoni mwenu.”