15
Unabii dhidi ya Moabu
Neno la unabii kuhusu Moabu:
Ari iliyo Moabu imeangamizwa:
imeharibiwa kwa usiku mmoja!
Kiri iliyo Moabu imeangamizwa,
imeharibiwa kwa usiku mmoja!
Diboni anakwea hadi kwenye hekalu lake,
hadi mahali pake pa juu pa kuabudia ili walie,
Moabu anaombolezea Nebo na Medeba.
Kila kichwa kimenyolewa
na kila ndevu limeondolewa.
Wamevaa magunia barabarani;
juu ya mapaa na kwenye viwanja
wote wanaomboleza,
wakilala kifudifudi na kulia.
Heshboni na Eleale wanalia,
sauti zao zinasikika hadi Yahazi.
Kwa hiyo watu wenye silaha wa Moabu wanapiga kelele,
nayo mioyo yao imezimia.
 
Moyo wangu unamlilia Moabu;
wakimbizi wake wanakimbilia Soari,
hadi Eglath-Shelishiya.
Wanapanda njia ya kwenda Luhithi,
wanaenda huku wanalia;
barabarani iendayo Horonaimu
wanaombolezea maangamizi yao.
Maji ya Nimrimu yamekauka
na majani yamenyauka;
mimea imekauka wala hakuna
kitu chochote kibichi kilichobaki.
Kwa hiyo mali waliyoipata na kujiwekea akiba
wamezichukua na kuvuka Bonde la Mierebi.
Mwangwi wa kilio chao umefika hadi mpakani mwa Moabu,
kilio chao cha huzuni kimefika hadi Eglaimu,
maombolezo yao hadi Beer-Elimu.
Maji ya Dimoni yamejaa damu,
lakini bado nitaleta pigo jingine juu ya Dimoni:
simba juu ya wakimbizi wa Moabu
na juu ya wale wanaobaki katika nchi.