26
Wimbo wa ushindi
Katika siku ile, wimbo huu utaimbwa katika nchi ya Yuda:
Tuna mji ulio na nguvu,
Mungu huufanya wokovu
kuwa kuta zake na maboma yake.
Fungua malango ili taifa lenye haki lipate kuingia,
taifa lidumishalo imani.
Utamlinda katika amani kamilifu
yeye ambaye moyo wake ni thabiti
kwa sababu anakutumaini wewe.
Mtumaini Mwenyezi Mungu milele,
kwa kuwa Mwenyezi Mungu,
Mwenyezi Mungu,
ni Mwamba wa milele.
Huwashusha wale wajikwezao,
huushusha chini mji wenye kiburi,
huushusha hadi ardhini
na kuutupa chini mavumbini.
Miguu huukanyagia chini:
miguu ya hao waliodhulumiwa,
hatua za hao maskini.
 
Mapito ya wenye haki ni nyoofu.
Ewe uliye Mwenye Haki,
waisawazisha njia ya mtu mnyofu.
Naam, Mwenyezi Mungu, tukienenda katika sheria zako,
twakungojea wewe,
jina lako na sifa zako
ndizo shauku za mioyo yetu.
Nafsi yangu yakutamani wakati wa usiku,
wakati wa asubuhi roho yangu yakuonea shauku.
Hukumu zako zinapokuja juu ya dunia,
watu wa ulimwengu hujifunza haki.
10 Ingawa neema yaoneshwa kwa waovu,
hawajifunzi haki;
hata katika nchi ya unyofu huendelea kutenda mabaya
wala hawazingatii utukufu wa Mwenyezi Mungu.
11 Ee Mwenyezi Mungu, mkono wako umeinuliwa juu,
lakini hawauoni.
Wao na waone wivu wako kwa ajili ya watu wako tena waaibishwe,
moto uliowekwa akiba kwa ajili ya adui zako na uwateketeze.
 
12 Mwenyezi Mungu, unaamuru amani kwa ajili yetu,
yale yote tuliyoweza kuyakamilisha ni wewe uliyetenda kwa ajili yetu.
13 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, mabwana wengine zaidi ya wewe wametutawala,
lakini jina lako pekee ndilo tunaloliheshimu.
14 Wao sasa wamekufa, wala hawako tena hai,
roho za waliokufa hazitarudi tena.
Uliwaadhibu na kuwaangamiza,
umefuta kumbukumbu lao lote.
15 Umeliongeza hilo taifa, Ee Mwenyezi Mungu,
umeliongeza hilo taifa.
Umejipatia utukufu kwa ajili yako mwenyewe,
umepanua mipaka yote ya nchi.
 
16 Mwenyezi Mungu, walikujia katika taabu yao,
wewe ulipowarudi,
waliweza kuomba kwa kunong’ona tu.
17 Kama mwanamke mwenye mimba aliyekaribia kuzaa
anavyogaagaa na kulia kwa ajili ya maumivu yake,
ndivyo tulivyokuwa mbele zako, Ee Mwenyezi Mungu.
18 Tulikuwa na mimba, tuligaagaa kwa maumivu,
lakini tulizaa upepo.
Hatukuleta wokovu duniani,
hatujazaa watu katika ulimwengu huu.
 
19 Lakini wafu wenu wataishi,
nayo miili yao itafufuka.
Ninyi mnaokaa katika mavumbi,
amkeni mkashangilie kwa furaha.
Umande wenu ni kama umande wa asubuhi,
dunia itawazaa wafu wake.
 
20 Nendeni, watu wangu, ingieni vyumbani mwenu
na mfunge milango nyuma yenu,
jificheni kwa kitambo kidogo
hadi ghadhabu yake ipite.
21 Tazama, Mwenyezi Mungu anakuja kutoka makao yake
ili kuwaadhibu watu wa dunia kwa ajili ya dhambi zao.
Dunia itadhihirisha umwagaji damu juu yake,
wala haitaendelea kuwaficha watu wake waliouawa.