42
Mtumishi wa Mwenyezi Mungu
“Huyu hapa mtumishi wangu, ninayemtegemeza,
mteule wangu, ninayependezwa naye;
nitaweka Roho yangu juu yake,
naye ataleta haki kwa mataifa.
Hatapaza sauti wala kupiga kelele,
wala hataipaza sauti yake barabarani.
Mwanzi uliopondeka hatauvunja,
na utambi unaofuka moshi hatauzima.
Kwa uaminifu ataleta haki,
hatazimia roho wala kukata tamaa,
hadi atakaposimamisha haki juu ya dunia.
Visiwa vitaweka tumaini lao katika sheria yake.”
 
Hili ndilo asemalo Mungu, Mwenyezi Mungu,
yeye aliyeziumba mbingu na kuzitanda,
aliyeitandaza dunia na vyote vinavyotoka humo,
awapaye watu wake pumzi,
na uzima kwa wale wanaoenda humo:
“Mimi, Mwenyezi Mungu, nimekuita katika haki;
nitakushika mkono wako.
Nitakulinda na kukufanya kuwa agano
kwa ajili ya watu
na nuru kwa Mataifa,
kuwafungua macho wale wasioona,
kuwaacha huru kutoka kifungoni wale waliofungwa,
na kuwafungua kutoka gerezani
wale wanaokaa gizani.
 
“Mimi ndimi Mwenyezi Mungu; hilo ndilo Jina langu!
Sitampa mwingine utukufu wangu
wala sanamu sifa zangu.
Tazama, mambo ya kwanza yametokea,
nami natangaza mambo mapya;
kabla hayajatokea
nawatangazia habari zake.”
Wimbo wa kumsifu Mwenyezi Mungu
10 Mwimbieni Mwenyezi Mungu wimbo mpya,
sifa zake toka miisho ya dunia,
ninyi mshukao chini baharini,
na vyote vilivyomo,
enyi visiwa na wote wanaoishi humo.
11 Jangwa na miji yake na vipaze sauti zao;
makazi anamoishi Kedari na yashangilie.
Watu wa Sela waimbe kwa furaha,
na wapige kelele kutoka vilele vya milima.
12 Wampe Mwenyezi Mungu utukufu,
na kutangaza sifa zake katika visiwa.
13 Mwenyezi Mungu ataenda kama mtu mwenye nguvu,
kama shujaa atachochea shauku yake,
kwa kishindo ataamsha ukelele wa vita,
naye atashinda adui zake.
 
14 “Kwa muda mrefu nimenyamaza;
nimekaa kimya na kujizuia.
Lakini sasa, kama mwanamke wakati wa kujifungua,
ninapiga kelele, ninatweta na kushusha pumzi.
15 Nitaharibu milima na vilima
na kukausha mimea yako yote;
nitafanya mito kuwa visiwa
na kukausha mabwawa.
16 Nitawaongoza vipofu kwenye njia ambayo hawajaijua,
kwenye mapito wasiyoyazoea nitawaongoza;
nitafanya giza kuwa nuru mbele yao,
na kufanya mahali palipoparuza kuwa laini.
Haya ndio mambo nitakayofanya;
mimi sitawaacha.
17 Lakini wale wanaotumaini sanamu,
wanaoviambia vinyago, ‘Ninyi ndio miungu yetu,’
watarudishwa nyuma kwa aibu kubwa.
Israeli ni kipofu na kiziwi
18 “Sikieni, enyi viziwi;
tazameni, enyi vipofu, mpate kuona!
19 Ni nani aliye kipofu isipokuwa mtumishi wangu,
na kiziwi kama mjumbe ninayemtuma?
Ni nani aliye kipofu kama yeye aliyejitoa kwangu,
aliye kipofu kama mtumishi wa Mwenyezi Mungu?
20 Mmeona vitu vingi, lakini hamkuzingatia;
masikio yenu yako wazi, lakini hamsikii chochote.”
21 Ilimpendeza Mwenyezi Mungu
kwa ajili ya haki yake
kufanya sheria yake kuwa kuu na tukufu.
22 Lakini hili ni taifa lililoibwa na kutekwa nyara,
wote wamenaswa katika mashimo,
au wamefichwa katika magereza.
Wamekuwa nyara,
wala hapana yeyote awaokoaye.
Wamefanywa mateka,
wala hapana yeyote asemaye, “Warudishe.”
 
23 Ni nani miongoni mwenu atakayesikiliza hili,
au atakayezingatia kwa makini katika wakati ujao?
24 Ni nani aliyemtoa Yakobo kuwa mateka,
na Israeli kwa wateka nyara?
Je, hakuwa yeye, Mwenyezi Mungu,
ambaye tumetenda dhambi dhidi yake?
Kwa kuwa hawakufuata njia zake,
hawakutii sheria zake.
25 Hivyo akawamwagia hasira yake inayowaka,
ukali wa vita.
Iliwazunguka kwa miali ya moto,
lakini hata hivyo hawakuelewa;
iliwateketeza, lakini hawakuyatia moyoni.