46
Miungu ya Babeli 
  1 Beli anasujudu, Nebo anainama;  
sanamu zao zabebwa na wanyama wa mizigo.  
Vinyago hivi mnavyobeba kila mahali ni mzigo wa kulemea,  
mzigo kwa waliochoka.   
 2 Vinyago pamoja na wale wanaovibeba wanainama chini;  
hiyo miungu haiwezi kuwaokoa watu,  
wote wanaenda utumwani pamoja.   
 3 “Nisikilizeni mimi, ee nyumba ya Yakobo,  
ninyi nyote mliobaki wa nyumba ya Israeli,  
ninyi ambao nimewategemeza tangu mlipotungwa mimba,  
nami nimewabeba tangu kuzaliwa kwenu.   
 4 Hata wakati wa uzee wenu na mvi, Mimi ndiye,  
Mimi ndiye nitakayewasaidia ninyi.  
Nimewahuluku, nami nitawabeba,  
nitawahudumia ninyi na kuwaokoa.   
 5 “Mtanilinganisha na nani,  
au mtanihesabu kuwa sawa na nani?  
Ni nani mtakayenifananisha naye  
ili tuweze kulinganishwa?   
 6 Wengine humwaga dhahabu kutoka mifuko yao,  
na kupima fedha kwenye mizani;  
huajiri mfua dhahabu kutengeneza mungu,  
kisha huisujudia na kuiabudu.   
 7 Huiinua mabegani na kuichukua;  
huiweka mahali pake, papo hapo ndipo isimamapo.  
Wala haiwezi kusogea kutoka mahali pale.  
Ingawa mtu huililia, haimjibu;  
haiwezi kumwokoa kwenye taabu zake.   
 8 “Kumbukeni hili, litieni akilini,  
liwekeni moyoni, enyi waasi.   
 9 Kumbukeni mambo yaliyopita, yale ya zamani za kale;  
mimi ndimi Mungu, wala hakuna mwingine;  
mimi ndimi Mungu,  
wala hakuna mwingine aliye kama mimi.   
 10 Ni mimi nitangazaye mwisho tangu mwanzo,  
naam, tangu zamani za kale,  
mambo ambayo hayajatendeka.  
Ninasema: Kusudi langu ndilo litakalosimama,  
nami nitatenda mapenzi yangu yote.   
 11 Kutoka mashariki ninaita ndege awindaye;  
kutoka nchi ya mbali,  
mtu atakayetimiza kusudi langu.  
Lile ambalo nimelisema, ndilo nitakalolitimiza;  
lile nililolipanga, ndilo nitakalolitenda.   
 12 Nisikilizeni, ninyi wenye mioyo migumu,  
ninyi mlio mbali na haki.   
 13 Ninaleta haki yangu karibu,  
haiko mbali;  
wala wokovu wangu hautachelewa.  
Nitawapa Sayuni wokovu,  
Israeli utukufu wangu.