5
Onyo kwa matajiri
1 Basi sikilizeni, ninyi matajiri, lieni na kuomboleza kwa ajili ya hali mbaya sana inayowajia. 2 Utajiri wenu umeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. 3 Dhahabu yenu na fedha yenu zimeliwa na kutu. Kutu yake itashuhudia dhidi yenu, nayo itaila miili yenu kama vile moto. Mmejiwekea hazina kwa ajili ya siku za mwisho. 4 Angalieni! Ule ujira wa vibarua waliolima mashamba yenu mliouzuia kwa hila unapiga kelele dhidi yenu, na vilio vya wavunaji vimefika masikioni mwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. 5 Mmeishi duniani kwa anasa na kwa starehe; mmejinenepesha tayari kwa siku ya kuchinjwa. 6 Mmewahukumu na kuwaua watu wenye haki, waliokuwa hawapingani nanyi.
Uvumilivu katika mateso
7 Kwa hiyo, ndugu zangu, vumilieni hadi kuja kwake Bwana Isa. Tazameni jinsi mkulima angojavyo ardhi itoe mavuno yake yaliyo ya thamani, na jinsi anavyovumilia kwa ajili ya kupata mvua ya kwanza na ya mwisho. 8 Ninyi nanyi vumilieni, tena simameni imara, kwa sababu kuja kwa Bwana Isa kumekaribia. 9 Ndugu zangu, msinung’unikiane, msije mkahukumiwa. Hakimu amesimama mlangoni!
10 Ndugu zangu, waangalieni manabii walionena kwa jina la Mwenyezi Mungu, wakiwa mfano wa uvumilivu katika kukabiliana na mateso. 11 Kama mnavyojua, tunawahesabu wale waliovumilia kuwa wabarikiwa. Mmesikia habari za uvumilivu wake Ayubu, na mmeona kile ambacho hatimaye Mwenyezi Mungu alimtendea. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, na amejaa rehema.
12 Zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, iwe kwa mbingu au kwa dunia, au kwa kitu kingine chochote. “Ndiyo” yenu na iwe ndiyo, na “Hapana” yenu iwe hapana, la sivyo mtahukumiwa.
Maombi ya imani
13 Je, mtu yeyote miongoni mwenu amepatwa na taabu? Basi inampasa aombe. Je, kuna yeyote mwenye furaha? Basi na aimbe nyimbo za kusifu. 14 Je, kuna yeyote miongoni mwenu aliye mgonjwa? Basi inampasa awaite wazee wa kundi la waumini wamwombee na kumpaka mafuta kwa Jina la Bwana Isa. 15 Kule kuomba kwa imani kutamwokoa huyo mgonjwa, naye Bwana Isa atamwinua, na kama ametenda dhambi, atasamehewa. 16 Kwa hiyo, ungamianeni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana ili mpate kuponywa. Maombi ya mwenye haki yana nguvu, tena yanafaa sana.
17 Ilya alikuwa mwanadamu kama sisi. Aliomba kwa bidii kwamba mvua isinyeshe, nayo haikunyesha juu ya nchi kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita. 18 Kisha akaomba tena, nazo mbingu zikatoa mvua, nayo ardhi ikatoa mazao yake.
19 Ndugu zangu, yeyote miongoni mwenu akipotoka na kuicha kweli, naye akarejeshwa na mtu mwingine, 20 hamna budi kujua kwamba yeyote amrejeshaye mwenye dhambi kutoka upotovu wake, ataiokoa roho ya huyo mwenye dhambi kutoka mauti na kufunika wingi wa dhambi.