10
Tola
Baada ya Abimeleki, Tola mwana wa Pua mwana wa Dodo, mtu wa Isakari, aliyeishi huko Shamiri, katika nchi ya vilima ya Efraimu, akainuka kuokoa Israeli. Akawa mwamuzi wa Israeli kwa miaka ishirini na tatu. Ndipo akafa, naye akazikwa huko Shamiri.
Yairi
Baada yake akafuatiwa na Yairi, Mgileadi, aliyekuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka ishirini na mbili. Alikuwa na wana thelathini waliopanda punda thelathini. Nao walikuwa na miji thelathini huko Gileadi, inayoitwa Hawoth-Yairi hadi leo. Yairi akafa, naye akazikwa huko Kamoni.
Yefta
Tena Waisraeli wakatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu. Wakaabudu Mabaali na Maashtorethi, na miungu ya Aramu, miungu ya Sidoni, miungu ya Moabu, miungu ya Waamoni, na miungu ya Wafilisti. Na kwa kuwa Waisraeli walimwacha Mwenyezi Mungu wala hawakuendelea kumtumikia, hivyo hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi ya Waisraeli. Naye akawatia mikononi mwa Wafilisti na Waamoni, ambao waliowaonea na kuwatesa mwaka huo. Kwa miaka kumi na nane wakawatesa Waisraeli wote upande wa mashariki mwa Mto Yordani huko Gileadi, katika nchi ya Waamori. Waamoni nao wakavuka Yordani ili kupigana na Yuda, Benyamini na nyumba ya Efraimu, nayo nyumba ya Israeli ikawa katika taabu kubwa. 10 Ndipo Waisraeli wakamlilia Mwenyezi Mungu wakasema, “Tumetenda dhambi dhidi yako, kumwacha Mungu wetu na kutumikia Mabaali.”
11 Mwenyezi Mungu akawaambia, “Wamisri, Waamori, Waamoni, Wafilisti, 12 Wasidoni, Waamaleki na Wamaoni walipowadhulumu ninyi, nanyi mkanililia na kuomba msaada, je, sikuwaokoa mikononi mwao? 13 Lakini ninyi mmeniacha na kuitumikia miungu mingine, kwa hiyo sitawaokoa tena. 14 Nendeni mkaililie ile miungu mlioichagua. Hiyo miungu na iwaokoe mnapokuwa katika taabu!”
15 Lakini Waisraeli wakamwambia Mwenyezi Mungu, “Tumetenda dhambi. Ututendee lile unaloona kuwa jema kwako, lakini twakusihi utuokoe sasa.” 16 Nao wakaiondoa hiyo miungu migeni kati yao nao wakamtumikia Mwenyezi Mungu. Naye akahuzunika kwa sababu ya taabu ya Israeli.
17 Waamoni walipoitwa vitani na kupiga kambi kule Gileadi, Waisraeli walikusanyika na kupiga kambi huko Mispa. 18 Viongozi wa watu wa Gileadi wakaambiana wao kwa wao, “Yeyote atakayeanzisha mashambulizi dhidi ya Waamoni atakuwa kiongozi wa wote wanaoishi Gileadi.”