12
Yefta na Efraimu
Watu wa Efraimu wakaita majeshi yao, wakavuka kwenda Zafoni. Wakamwambia Yefta, “Kwa nini mmeenda kupigana na Waamoni bila kutuita ili twende pamoja nawe? Basi tutaichoma moto nyumba yako, pamoja nawe ukiwa ndani yake.”
Yefta akajibu, “Mimi na watu wangu tulikuwa na ugomvi mkubwa na Waamoni. Ingawa niliwaita, hamkuniokoa kutoka mkono wao. Nilipoona kuwa hamniokoi, nikauhatarisha uhai wangu, nikavuka kupigana na Waamoni. Naye Mwenyezi Mungu akanipatia ushindi dhidi yao. Sasa kwa nini mnanijia leo ili kupigana nami?”
Ndipo Yefta akakusanya wanaume wa Gileadi pamoja na kupigana na Efraimu. Wagileadi wakawashinda Waefraimu, kwa kuwa Waefraimu walisema, “Ninyi Wagileadi ni waasi mliotoroka toka Efraimu na Manase.” Wagileadi wakaviteka vivuko vya Mto Yordani kuelekea Efraimu. Kisha ilikuwa yeyote aliyenusurika kutoka Efraimu aliposema, “Niache nivuke,” hao wanaume wa Gileadi walimuuliza, “Je wewe ni Mwefraimu?” Akijibu “Hapana,” walimwambia, “Sawa, sema ‘Shibolethi’.” Iwapo alitamka, “Sibolethi”, kwa sababu hakuweza kutamka hilo neno sawasawa, walimkamata na kumuua hapo kwenye vivuko vya Mto Yordani. Waefraimu elfu arobaini na mbili waliuawa wakati huo.
Yefta akawa mwamuzi wa Waisraeli kwa muda wa miaka sita. Kisha Yefta akafa, akazikwa katika mmoja wa miji ya Gileadi.
Ibzani, Eloni na Abdoni
Baada yake, Ibzani wa Bethlehemu akawa mwamuzi wa Israeli. Alikuwa na wana thelathini na binti thelathini. Akawaoza binti zake kwa watu wengine nje ya ukoo wake, na kuwatwalia wanawe wanawake thelathini toka nje ya ukoo wake. Ibzani akawa mwamuzi wa Israeli kwa muda wa miaka saba. 10 Kisha Ibzani akafa, akazikwa huko Bethlehemu.
11 Baada yake, Eloni Mzabuloni akawa mwamuzi wa Israeli kwa muda wa miaka kumi. 12 Kisha Eloni akafa, akazikwa huko Aiyaloni katika nchi ya Zabuloni.
13 Baada yake, Abdoni mwana wa Hileli Mpirathoni akawa mwamuzi wa Israeli. 14 Naye alikuwa na wana arobaini, na wajukuu thelathini waliopanda punda sabini. Akawa mwamuzi wa Israeli kwa muda wa miaka nane. 15 Kisha Abdoni mwana wa Hileli Mpirathoni akafa, akazikwa Pirathoni huko Efraimu, katika nchi ya vilima ya Waamaleki.