5
Hakuna hata mmoja aliye mkamilifu
“Pandeni na kushuka katika mitaa ya Yerusalemu,
tazameni pande zote na mtafakari,
tafuteni katika viwanja vyake.
Kama mtaweza kumpata hata mtu mmoja tu
atendaye kwa uaminifu na kutafuta kweli,
nitausamehe mji huu.
Ingawa wanasema, ‘Kwa hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo,’
bado wanaapa kwa uongo.”
 
Ee Mwenyezi Mungu, je, macho yako hayaitafuti kweli?
Uliwapiga, lakini hawakusikia maumivu,
uliwapondaponda, lakini walikataa maonyo.
Walifanya nyuso zao kuwa ngumu kuliko jiwe
nao walikataa kutubu.
Ndipo nikasema, “Hawa ni maskini tu;
wao ni wapumbavu,
kwa maana hawaijui njia ya Mwenyezi Mungu,
sheria ya Mungu wao.
Kwa hiyo nitaenda kwa wakuu
na kuzungumza nao,
hakika wao wanaijua njia ya Mwenyezi Mungu,
sheria ya Mungu wao.”
Lakini kwa nia moja nao pia walikuwa wameivunja nira
na kuvivunja vifungo.
Kwa hiyo simba wa mwituni atawashambulia,
mbwa-mwitu wa jangwani atawaangamiza,
chui atawavizia karibu na miji yao,
ili kumrarua vipande vipande yeyote atakayethubutu kutoka nje,
kwa maana uasi wao ni makubwa,
na kukengeuka kwao kumekuwa ni kwingi.
 
“Kwa nini niwasamehe?
Watoto wenu wameniacha kwa kuapa kwa miungu batili.
Niliwapatia mahitaji yao yote,
lakini bado wamefanya uzinzi na kusongamana katika nyumba za makahaba.
Wamelishwa vizuri, kama farasi dume wenye tamaa nyingi,
kila mmoja akimlilia mke wa mwanaume mwingine.
Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya hili?”
asema Mwenyezi Mungu.
“Je, nisijilipizie kisasi
juu ya taifa kama hili?
 
10 “Piteni katika mashamba yake ya mizabibu na kuyaharibu,
lakini msiangamize kabisa.
Pogoeni matawi yake,
kwa kuwa watu hawa sio wa Mwenyezi Mungu.
11 Nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda
wamekuwa si waaminifu kwangu kabisa,”
asema Mwenyezi Mungu.
 
12 Wamedanganya kuhusu Mwenyezi Mungu.
Wamesema, “Yeye hatafanya jambo lolote!
Hakuna dhara litakalotupata;
kamwe hatutaona upanga wala njaa.
13 Manabii ni upepo tu, wala neno halimo ndani yao;
kwa hiyo hayo wayasemayo na yatendeke kwao.”
14 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni:
“Kwa sababu watu hawa wamesema maneno haya,
nitayafanya maneno yangu vinywani mwenu kuwa moto,
na watu hawa wawe kuni
zinazoliwa na huo moto.
15 Ee nyumba ya Israeli,” asema Mwenyezi Mungu,
“Ninaleta taifa toka mbali dhidi yako,
taifa la kale na linaloendelea kudumu,
taifa ambalo lugha yao huijui,
wala msemo wao huwezi kuuelewa.
16 Podo lao ni kama kaburi lililo wazi,
wote ni mashujaa hodari.
17 Watayaangamiza mazao yenu na chakula chenu,
watawaangamiza wana wenu wa kiume na wa kike;
watayaangamiza makundi yenu ya kondoo na ya ng’ombe,
wataiangamiza mizabibu yenu na mitini yenu.
Kwa upanga wataiangamiza
miji yenye ngome mliyoitumainia.
18 “Hata hivyo katika siku hizo, sitakuangamiza kabisa,” asema Mwenyezi Mungu. 19 “Nao watu watakapouliza, ‘Kwa nini Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, ametufanyia mambo haya yote?’ utawaambia, ‘Kama mlivyoniacha mimi kwa kuitumikia miungu migeni katika nchi yenu wenyewe, ndivyo sasa mtakavyowatumikia wageni katika nchi ambayo si yenu.’
20 “Itangazie nyumba ya Yakobo hili
na ulipigie mbiu katika Yuda:
21 Sikieni hili, enyi watu wapumbavu, msio na akili,
mlio na macho lakini hamwoni,
mlio na masikio lakini hamsikii:
22 Je, haiwapasi kuniogopa mimi?” asema Mwenyezi Mungu.
“Je, haiwapasi kutetemeka mbele zangu?
Niliufanya mchanga kuwa mpaka wa bahari,
kizuizi cha milele ambacho bahari haiwezi kuupita.
Mawimbi yanaweza kuumuka, lakini hayawezi kuupita;
yanaweza kunguruma, lakini hayawezi kuuvuka.
23 Lakini watu hawa wana mioyo ya ukaidi na ya uasi,
wamegeukia mbali na kwenda zao.
24 Wao hawaambiani wenyewe,
‘Sisi na tumwogope Mwenyezi Mungu, Mungu wetu,
anayetupatia mvua za masika na za vuli kwa majira yake,
anayetuhakikishia majuma ya mavuno kwa utaratibu.’
25 Matendo yenu mabaya yamezuia haya yote,
dhambi zenu zimewazuia msipate mema.
 
26 “Miongoni mwa watu wangu wamo walio waovu
wanaovizia kama watu wanaotega ndege,
na kama wale wanaoweka mitego
kuwakamata watu.
27 Kama vitundu vilivyojaa ndege,
nyumba zao zimejaa udanganyifu;
wamekuwa matajiri na wenye nguvu,
28 wamenenepa na kunawiri.
Matendo yao maovu hayana kikomo;
hawatetei mashauri ya yatima wapate kushinda,
hawatetei haki za maskini.
29 Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya hili?”
asema Mwenyezi Mungu.
“Je, nisijilipizie kisasi
juu ya taifa kama hili?
 
30 “Jambo la kutisha na kushtusha
limetokea katika nchi hii:
31 Manabii wanatabiri uongo,
makuhani wanatawala kwa mamlaka yao wenyewe,
nao watu wangu wanapenda hivyo.
Lakini mtafanya nini mwisho wake?