11
Agano limevunjwa
Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu: “Sikia maneno ya agano hili, nawe uwaambie watu wa Yuda na wale wanaoishi Yerusalemu. Waambie kwamba hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Amelaaniwa mtu ambaye hatayatii maneno ya agano hili, maneno niliyowaamuru baba zenu nilipowatoa katika nchi ya Misri, kutoka tanuru la kuyeyushia vyuma.’ Nilisema, ‘Nitiini mimi na mfanye kila kitu ninachowaamuru, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu. Kisha nitatimiza kiapo nilichowaapia baba zenu, kuwapa nchi inayotiririka maziwa na asali,’ nchi ambayo mnaimiliki leo.”
Nikajibu, “Amen, Mwenyezi Mungu.”
Mwenyezi Mungu akaniambia, “Tangaza maneno haya yote katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu: ‘Sikilizeni maneno ya agano hili na kuyafuata. Tangu wakati ule niliwapandisha baba zenu kutoka Misri hadi leo, niliwaonya tena na tena, nikisema, “Nitiini mimi.” Lakini hawakusikiliza wala kujali. Badala yake, walifuata ukaidi wa mioyo yao miovu. Hivyo nikaleta juu yao laana zote za agano nililokuwa nimewaamuru wao kulifuata, lakini hawakulishika.’ ”
Kisha Mwenyezi Mungu akaniambia, “Kuna fitina inayoendelea miongoni mwa watu wa Yuda na wale wanaoishi Yerusalemu. 10 Wamerudia dhambi za baba zao waliokataa kusikiliza maneno yangu. Wameifuata miungu mingine na kuitumikia. Nyumba zote mbili za Israeli na Yuda zimelivunja agano nililofanya na baba zao. 11 Kwa hivyo, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Nitaleta juu yao maafa ambayo hawawezi kuyakimbia. Hata wakinililia, sitawasikiliza. 12 Miji ya Yuda na watu wa Yerusalemu wataenda kuililia miungu ambayo wameifukizia uvumba, lakini haitawasaidia kamwe wakati maafa yatakapowapiga. 13 Mnayo miungu mingi kama miji mliyo nayo, ee Yuda, nazo madhabahu mlizozijenga za kumfukizia uvumba huyo mungu wa aibu, Baali ni nyingi kama barabara za Yerusalemu.’
14 “Wewe usiwaombee watu hawa wala kufanya maombezi yoyote au kunisihi kwa ajili yao, kwa sababu sitawasikiliza watakaponiita wakati wa taabu yao.
15 “Mpendwa wangu anafanya nini hekaluni mwangu,
anapofanya mashauri yake maovu na wengi?
Je, nyama iliyowekwa wakfu yaweza
kukuondolea uovu wako?
Unashangilia unapojiingiza
katika uovu wako.”
 
16 Mwenyezi Mungu alikuita jina lako Mzeituni uliostawi,
wenye matunda yakupendeza.
Lakini kwa ngurumo ya mawimbi makuu
atautia moto,
nayo matawi yake yatavunjika.
17 Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, aliyekupanda, ametamka maafa juu yako, kwa sababu nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda mmefanya maovu na kunikasirisha kwa kumfukizia Baali uvumba.
Njama dhidi ya Yeremia
18 Kwa sababu Mwenyezi Mungu alinifunulia na kunionesha hila zao mbaya, na waliyokuwa wanayafanya niliyafahamu. 19 Nilikuwa kama mwana-kondoo mpole aliyeongozwa machinjoni; mimi sikutambua kwamba walikuwa wamepanga njama dhidi yangu, wakisema,
“Sisi na tuuangamize mti na matunda yake;
nasi tumkatilie mbali kutoka nchi ya walio hai,
ili jina lake lisikumbukwe tena.”
20 Lakini, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, wewe uhukumuye kwa haki,
uchunguzaye moyo na akili,
acha nione ukiwalipiza wao kisasi,
kwa maana kwako nimeweka shauri langu.
21 “Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu kuhusu watu wa Anathothi wanaotafuta uhai wako, wakisema, ‘Usitoe unabii kwa jina la Mwenyezi Mungu, la sivyo utakufa kwa mikono yetu’: 22 kwa hiyo hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Nitawaadhibu. Vijana wao wa kiume watakufa kwa upanga, wana wao wa kiume na wa kike watakufa kwa njaa. 23 Hayatabakizwa mabaki kwao kwa sababu nitaleta maafa kwa watu wa Anathothi katika mwaka wa kuadhibiwa kwao.’ ”