26
Yeremia atishiwa kuuawa
1 Mwanzoni mwa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, neno hili lilikuja kutoka kwa Mwenyezi Mungu: 2 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Simama katika ua wa nyumba ya Mwenyezi Mungu na useme na watu wote wa miji ya Yuda wanaokuja kuabudu katika nyumba ya Mwenyezi Mungu. Waambie kila kitu nitakachokuamuru, usipunguze neno. 3 Huenda watasikia na kugeuka, kisha kila mmoja kutubu na kuacha njia yake mbaya. Nami nitaghairi kuleta maafa niliyopanga kufanya dhidi yao kwa sababu ya matendo yao maovu. 4 Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Ikiwa hamtanisikiliza na kuifuata sheria yangu niliyoiweka mbele yenu, 5 na msipoyasikiliza maneno ya watumishi wangu manabii, ambao nimewatuma kwenu tena na tena (ijapokuwa hamkuwasikiliza), 6 ndipo nitaifanya nyumba hii kama Shilo na mji huu kuwa kitu cha kulaaniwa na mataifa yote ya dunia.’ ”
7 Makuhani, manabii na watu wote wakamsikia Yeremia akiyasema maneno haya ndani ya nyumba ya Mwenyezi Mungu. 8 Lakini mara tu Yeremia alipomaliza kuwaambia watu kila kitu Mwenyezi Mungu alichomwamuru kukisema, basi makuhani, manabii na watu wote walimkamata wakisema, “Ni lazima ufe! 9 Kwa nini unatoa unabii katika jina la Mwenyezi Mungu kwamba nyumba hii itakuwa kama Shilo na mji huu utakuwa ukiwa na kuachwa tupu?” Nao watu wote wakamkusanyikia na kumzunguka Yeremia ndani ya nyumba ya Mwenyezi Mungu.
10 Maafisa wa Yuda waliposikia kuhusu mambo haya, wakapanda kutoka jumba la kifalme, wakaenda katika nyumba ya Mwenyezi Mungu na kushika nafasi zao kwenye ingilio la Lango Jipya la nyumba ya Mwenyezi Mungu. 11 Kisha makuhani na manabii wakawaambia maafisa pamoja na watu wote, “Mtu huyu anastahili ahukumiwe kifo kwa sababu ametoa unabii mbaya dhidi ya mji huu. Mmesikia kwa masikio yenu wenyewe!”
12 Kisha Yeremia akawaambia maafisa wote na watu wote: “Mwenyezi Mungu amenituma kutoa unabii dhidi ya nyumba hii na mji huu mambo yote mliyoyasikia. 13 Sasa tengenezeni njia zenu na matendo yenu, na kumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Ndipo Mwenyezi Mungu atawahurumia na kuacha kuleta maafa aliyokuwa ameyatamka dhidi yenu. 14 Lakini mimi niko mikononi mwenu; nifanyieni lolote mnaloona kuwa jema na haki. 15 Hata hivyo, jueni kwa hakika, ikiwa mtaniua, kwa kumwaga damu isiyo na hatia, mtakuwa mmejipatia dhambi juu yenu wenyewe, juu ya mji huu, na juu ya wote wanaoishi ndani yake, kwa kuwa ni kweli Mwenyezi Mungu amenituma kwenu ili niseme maneno haya masikioni mwenu.”
16 Kisha maafisa na watu wote wakawaambia makuhani na manabii, “Mtu huyu asihukumiwe kifo! Amesema nasi katika jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wetu.”
17 Baadhi ya wazee wa nchi wakasogea mbele, wakaliambia kusanyiko lote la watu, 18 “Mika Mmoreshethi alitoa unabii katika siku za Hezekia mfalme wa Yuda. Akawaambia watu wote wa Yuda, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni:
“ ‘Sayuni italimwa kama shamba,
Yerusalemu itakuwa lundo la kokoto,
na kilima cha Hekalu kitakuwa kichuguu
kilichofunikwa na vichaka.’
19 Je, Hezekia mfalme wa Yuda au mtu mwingine yeyote katika Yuda alimhukumu Mika kufa? Je, Hezekia hakumcha Mwenyezi Mungu na kuhitaji msaada wake? Je, Mwenyezi Mungu hakuwahurumia na kughairi maafa aliyokuwa ametamka dhidi yao? Tunakaribia sana kujiletea maangamizi ya kutisha sisi wenyewe!”
20 Wakati huu, Uria mwana wa Shemaya kutoka mji wa Kiriath-Yearimu alikuwa mtu mwingine aliyetoa unabii kwa jina la Mwenyezi Mungu. Alitoa unabii juu ya mambo yaliyofanana na haya dhidi ya mji huu na nchi hii kama alivyofanya Yeremia. 21 Mfalme Yehoyakimu na wakuu wake wote na maafisa waliposikia maneno yake, mfalme alitafuta kumuua. Lakini Uria alipata habari, na kwa kuogopa akakimbilia Misri. 22 Hata hivyo, Mfalme Yehoyakimu alimtuma Elnathani mwana wa Akbori huko Misri, pamoja na watu wengine ili kwenda kumkamata Uria. 23 Wakamrudisha Uria kutoka Misri na kumpeleka kwa Mfalme Yehoyakimu, ambaye alimuua kwa upanga, na mwili wake kutupwa kwenye eneo la makaburi ya watu wasio na cheo.
24 Zaidi ya hayo, Ahikamu mwana wa Shafani akamuunga mkono Yeremia, kwa hiyo hakutiwa tena mikononi mwa watu ili auawe.