30
Kurejeshwa kwa Israeli 
  1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu:   2 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Andika katika kitabu maneno yote niliyonena na wewe.   3 Siku zinakuja,’ asema Mwenyezi Mungu, ‘nitakapowaleta watu wangu Israeli na Yuda kutoka uhamishoni, na kuwarudisha katika nchi niliyowapa baba zao ili kuimiliki,’ asema Mwenyezi Mungu.”   
 4 Haya ndio maneno aliyoyanena Mwenyezi Mungu kuhusu Israeli na Yuda:   5 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:  
“ ‘Vilio vya woga vinasikika:  
hofu kuu, wala si amani.   
 6 Ulizeni na mkaone:  
Je, mwanaume aweza kuzaa watoto?  
Kwa nini basi ninaona kila mwanaume mwenye nguvu  
ameweka mikono yake tumboni  
kama mwanamke aliye na uchungu wa kuzaa,  
kila uso ukigeuka rangi kabisa?   
 7 Ole! Kwa kuwa siku ile itakuwa ya kutisha.  
Hakutakuwa na nyingine kama hiyo.  
Utakuwa wakati wa dhiki kwa Yakobo,  
lakini ataokolewa kutoka dhiki hiyo.   
 8 “ ‘Katika siku ile,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,  
‘nitaivunja nira kutoka shingoni mwao  
na kuvipasua vifungo vyao;  
wageni hawatawafanya tena watumwa.   
 9 Badala yake, watamtumikia Mwenyezi Mungu, Mungu wao,  
na Daudi mfalme wao,  
nitakayemwinua kwa ajili yao.   
 10 “ ‘Hivyo usiogope, ee Yakobo mtumishi wangu,  
usifadhaike, ee Israeli,’  
asema Mwenyezi Mungu.  
‘Hakika, nitakuokoa kutoka mbali,  
wazao wako kutoka nchi ya uhamisho wao.  
Yakobo atakuwa tena na amani na usalama,  
wala hakuna atakayemtia hofu.   
 11 Mimi niko pamoja nawe, nami nitakuokoa,’  
asema Mwenyezi Mungu.  
‘Ingawa nitayaangamiza kabisa mataifa yote  
nilikokuwa nimewatawanya,  
sitawaangamiza ninyi kabisa.  
Nitawaadhibu, lakini kwa haki.  
Sitawaacha kabisa bila adhabu.’   
 12 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:  
“ ‘Kidonda chako hakina dawa,  
jeraha lako haliponyeki.   
 13 Hakuna yeyote wa kukutetea katika shauri lako,  
hakuna dawa ya kidonda chako,  
wewe hutapona.   
 14 Wale walioungana nawe wote wamekusahau,  
hawajali chochote kukuhusu wewe.  
Nimekupiga vile adui angekupiga,  
na kukuadhibu vile mtu mkatili angekuadhibu,  
kwa sababu hatia yako ni kubwa mno,  
na dhambi zako ni nyingi sana.   
 15 Kwa nini unalia kwa ajili ya jeraha lako,  
yale maumivu yako yasiyoponyeka?  
Kwa sababu ya uovu wako mkubwa na dhambi zako nyingi  
nimekufanyia mambo haya.   
 16 “ ‘Lakini watu wote wakuangamizao wataangamizwa;  
adui zako wote wataenda uhamishoni.  
Wale wote wakutekao nyara watatekwa nyara;  
wote wakufanyao mateka nitawafanya mateka.   
 17 Lakini nitakurudishia afya yako  
na kuyaponya majeraha yako,’  
asema Mwenyezi Mungu,  
‘kwa sababu umeitwa mwenye kutupwa,  
Sayuni ambaye hakuna yeyote anayekujali.’   
 18 “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:  
“ ‘Nitarudisha baraka za mahema ya Yakobo,  
na kuhurumia maskani zake.  
Mji utajengwa tena juu ya magofu yake,  
nalo jumba la kifalme litasimama mahali pake halisi.   
 19 Nyimbo za kushukuru zitatoka kwao  
na sauti ya furaha.  
Nitaiongeza idadi yao  
wala hawatapungua,  
nitawapa heshima  
na hawatadharauliwa.   
 20 Watoto wao watakuwa kama walivyokuwa  
siku za zamani,  
nayo jumuiya yao itaimarishwa mbele yangu;  
nitawaadhibu wote wanaowadhulumu.   
 21 Mmoja wao atakuwa kiongozi wao;  
mtawala wao atainuka miongoni mwao.  
Nitamleta karibu nami,  
naye atanikaribia mimi,  
kwa maana ni nani yule atakayejitolea  
kuwa karibu nami?’  
asema Mwenyezi Mungu.   
 22 ‘Kwa hiyo ninyi mtakuwa watu wangu,  
nami nitakuwa Mungu wenu.’ ”   
 23 Tazama, tufani ya Mwenyezi Mungu  
italipuka kwa ghadhabu,  
upepo wa kisulisuli uendao kasi  
utashuka juu ya vichwa vya waovu.   
 24 Hasira kali ya Mwenyezi Mungu haitarudi nyuma  
hadi atakapotimiza makusudi yote ya moyo wake.  
Siku zijazo  
mtayaelewa haya.