45
Ujumbe kwa Baruku
Hili ndilo nabii Yeremia alilomwambia Baruku mwana wa Neria katika mwaka wa nne wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, baada ya Baruku kuandika katika kitabu maneno ambayo yalitoka kinywani mwa Yeremia wakati ule: “Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, akuambialo wewe Baruku: Ulisema, ‘Ole wangu! Mwenyezi Mungu ameongeza huzuni juu ya maumivu yangu, nimechoka kwa kulia kwa uchungu wala sipati pumziko.’ ”
Lakini Mwenyezi Mungu akasema, “Mwambie hivi: ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Nitakibomoa kile nilichokijenga, na kung’oa kile nilichokipanda katika nchi yote. Je, utajitafutia mambo makubwa kwa ajili yako mwenyewe? Usiyatafute hayo. Kwa kuwa nitaleta maangamizi juu ya watu wote, asema Mwenyezi Mungu, lakini popote utakapoenda, nitayaokoa maisha yako.’ ”