50
Ujumbe kuhusu Babeli 
  1 Hili ndilo neno alilosema Mwenyezi Mungu kupitia nabii Yeremia kuhusu Babeli na nchi ya Wakaldayo:   
 2 “Tangazeni! Hubirini katikati ya mataifa,  
Inueni bendera na mkahubiri;  
msiache kitu chochote, bali semeni,  
‘Babeli utatekwa;  
Beli ataaibishwa,  
Merodaki atajazwa na hofu kuu.  
Sanamu zake zitaaibishwa  
na vinyago vyake vitajazwa hofu kuu.’   
 3 Taifa kutoka kaskazini litamshambulia,  
na kuifanya nchi yake ukiwa.  
Hakuna atakayeishi ndani yake,  
watu na wanyama wataikimbia.   
 4 “Katika siku hizo, wakati huo,”  
asema Mwenyezi Mungu,  
“watu wa Israeli pamoja na watu wa Yuda  
wataenda wakilia ili kumtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu wao.   
 5 Wataulizia njia iendayo Sayuni  
na kuelekeza nyuso zao huko.  
Watakuja na kuambatana na Mwenyezi Mungu  
katika agano la milele  
ambalo halitasahaulika.   
 6 “Watu wangu wamekuwa kondoo waliopotea;  
wachungaji wao wamewapotosha  
na kuwafanya wazurure mlimani.  
Walitangatanga juu ya mlima na kilima,  
na kusahau mahali pao pa kupumzikia.   
 7 Yeyote aliyewakuta aliwala;  
adui zao walisema, ‘Sisi hatuna hatia,  
kwa kuwa wao walitenda dhambi dhidi ya  
Mwenyezi Mungu, malisho yao halisi,  
Mwenyezi Mungu, aliye tumaini la baba zao.’   
 8 “Kimbieni kutoka Babeli;  
ondokeni katika nchi ya Wakaldayo,  
kuweni kama mbuzi wale waongozao kundi.   
 9 Kwa maana nitaamsha na kuleta dhidi ya Babeli  
muungano wa mataifa makubwa kutoka nchi ya kaskazini.  
Watashika nafasi zao dhidi yake,  
naye kutokea kaskazini atatekwa.  
Mishale yao itakuwa kama mishale ya mashujaa walio hodari,  
ambao hawawezi kurudi mikono mitupu.   
 10 Kwa hiyo Ukaldayo utatekwa nyara;  
wote wanaouteka, watapata nyara za kutosha,”  
asema Mwenyezi Mungu.   
 11 “Kwa sababu hushangilia na kufurahi,  
wewe utekaye urithi wangu,  
kwa sababu unachezacheza kama mtamba anayepura nafaka,  
na kulia kama farasi dume,   
 12 mama yako ataaibika mno,  
yeye aliyekuzaa atatahayari.  
Atakuwa mdogo kuliko mataifa mengine yote,  
atakuwa nyika, nchi kame na jangwa.   
 13 Kwa sababu ya hasira ya Mwenyezi Mungu hatakaliwa na mtu,  
lakini ataachwa ukiwa kabisa.  
Wote watakaopita Babeli watatiwa hofu na kudhihaki  
kwa sababu ya majeraha yake yote.   
 14 “Shikeni nafasi zenu kuzunguka Babeli,  
enyi nyote mvutao upinde.  
Mpigeni! Msibakize mshale wowote,  
kwa kuwa ametenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu.   
 15 Piga kelele dhidi yake kila upande!  
Anajisalimisha, minara yake inaanguka,  
kuta zake zimebomoka.  
Kwa kuwa hiki ni kisasi cha Mwenyezi Mungu,  
mlipizeni kisasi;  
mtendeeni kama alivyowatendea wengine.   
 16 Katilieni mbali mpanzi kutoka Babeli,  
pamoja na mvunaji na mundu wake akivuna.  
Kwa sababu ya upanga wa mdhalimu  
kila mmoja na arejee kwa watu wake mwenyewe,  
kila mmoja na akimbilie  
kwenye nchi yake mwenyewe.   
 17 “Israeli ni kundi lililotawanyika  
ambalo simba wamelifukuzia mbali.  
Wa kwanza kumla alikuwa mfalme wa Ashuru,  
wa mwisho kuponda mifupa yake  
alikuwa Nebukadneza mfalme wa Babeli.”   
 18 Kwa hiyo hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo:  
“Nitamwadhibu mfalme wa Babeli na nchi yake  
kama nilivyomwadhibu mfalme wa Ashuru.   
 19 Lakini nitamrudisha Israeli katika malisho yake mwenyewe  
naye atalisha huko Karmeli na Bashani;  
njaa yake itashibishwa  
juu ya vilima vya Efraimu na Gileadi.   
 20 Katika siku hizo, wakati huo,”  
asema Mwenyezi Mungu,  
“uchunguzi utafanyika kwa ajili ya kosa la Israeli,  
lakini halitaonekana,  
na kwa ajili ya dhambi za Yuda,  
lakini haitapatikana hata moja,  
kwa kuwa nitawasamehe  
mabaki nitakaowaacha.   
 21 “Shambulieni nchi ya Merathaimu  
na wale wanaoishi huko Pekodi.  
Wafuatieni, waueni  
na kuwaangamiza kabisa,”  
asema Mwenyezi Mungu.  
“Fanyeni kila kitu nilichowaamuru.   
 22 Kelele ya vita iko ndani ya nchi,  
kelele ya maangamizi makuu!   
 23 Tazama jinsi nyundo ya dunia yote  
ilivyovunjika na kuharibika!  
Tazama jinsi Babeli ilivyokuwa ukiwa  
miongoni mwa mataifa!   
 24 Nimetega mtego kwa ajili yako, ee Babeli,  
nawe ukakamatwa kabla hujafahamu;  
ulipatikana na ukakamatwa  
kwa sababu ulimpinga Mwenyezi Mungu.   
 25 Mwenyezi Mungu amefungua ghala lake la silaha  
na kuzitoa silaha za ghadhabu yake,  
kwa kuwa Bwana Mwenyezi Mungu,  
Mungu wa majeshi ya mbinguni,  
anayo kazi ya kufanya  
katika nchi ya Wakaldayo.   
 26 Njooni dhidi yake kutoka mbali.  
Zifungueni ghala zake za nafaka;  
mlundikeni kama lundo la nafaka.  
Mwangamizeni kabisa  
na msimwachie mabaki yoyote.   
 27 Waueni mafahali wake wachanga wote;  
waacheni washuke machinjoni!  
Ole wao! Kwa kuwa siku yao imewadia,  
wakati wao wa kuadhibiwa.   
 28 Wasikilizeni watoro na wakimbizi kutoka Babeli  
wakitangaza katika Sayuni  
jinsi Mwenyezi Mungu, Mungu wetu  
alivyolipiza kisasi,  
kisasi kwa ajili ya Hekalu lake.   
 29 “Waiteni wapiga mishale dhidi ya Babeli,  
wote wavutao upinde.  
Pigeni kambi kumzunguka kabisa,  
asitoroke mtu yeyote.  
Mlipizeni kwa matendo yake;  
mtendeeni kama alivyotenda.  
Kwa kuwa alimdharau Mwenyezi Mungu,  
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.   
 30 Kwa hiyo, vijana wake wanaume wataanguka barabarani;  
askari wake wote watanyamazishwa siku ile,”  
asema Mwenyezi Mungu.   
 31 “Tazama, niko kinyume nawe, ewe mwenye majivuno,”  
asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni,  
“kwa kuwa siku yako imewadia,  
yaani wakati wako wa kuadhibiwa.   
 32 Mwenye majivuno atajikwaa na kuanguka,  
wala hakuna yeyote atakayemuinua;  
nitawasha moto katika miji yake,  
utakaowateketeza wote wanaomzunguka.”   
 33 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni:  
“Watu wa Israeli wamedhulumiwa,  
hata watu wa Yuda pia.  
Wote waliowateka wamewashikilia sana,  
wanakataa kuwaachia waende.   
 34 Lakini Mkombozi wao ana nguvu;  
Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ndilo jina lake.  
Atatetea shauri lao kwa nguvu  
ili alete amani nchini mwao,  
lakini ataleta msukosuko  
kwa wale wanaoishi Babeli.   
 35 “Upanga dhidi ya Wakaldayo!”  
asema Mwenyezi Mungu,  
“dhidi ya wale wanaoishi Babeli,  
na dhidi ya maafisa wake na wenye busara!   
 36 Upanga dhidi ya manabii wake wa uongo!  
Watakuwa wapumbavu.  
Upanga dhidi ya mashujaa wake!  
Watajazwa na hofu kuu   
 37 Upanga dhidi ya farasi na magari yake ya vita  
pamoja na askari wake wote wa kigeni katika safu zake!  
Wao watakuwa kama wanawake.  
Upanga dhidi ya hazina zake!  
Hizo zitatekwa nyara.   
 38 Ukame juu ya maji yake!  
Nayo yatakauka.  
Kwa kuwa ni nchi ya sanamu,  
wao wanaenda wazimu kwa ajili ya sanamu.   
 39 “Kwa hiyo, viumbe vya jangwani na fisi wataishi humo,  
nao bundi watakaa humo.  
Kamwe haitakaliwa tena  
wala watu hawataishi humo kizazi hadi kizazi.   
 40 Kama Mungu alivyoangamiza Sodoma na Gomora  
pamoja na miji iliyokuwa jirani nayo,”  
asema Mwenyezi Mungu,  
“vivyo hivyo hakuna mtu atakayeishi humo.  
Naam, hakuna mtu atakayekaa humo.   
 41 “Tazama! Jeshi linakuja kutoka kaskazini;  
taifa kubwa na wafalme wengi  
wanaamshwa kutoka miisho ya dunia.   
 42 Wamejifunga pinde na mikuki;  
ni wakatili na hawana huruma.  
Wanatoa sauti kama bahari inayounguruma  
wanapoendesha farasi wao;  
wanakuja kama watu waliojipanga tayari kwa vita  
ili kukushambulia, ee Binti Babeli.   
 43 Mfalme wa Babeli amesikia habari kuwahusu,  
nayo mikono yake imelegea.  
Uchungu umemshika,  
maumivu kama ya mwanamke katika uchungu wa kuzaa.   
 44 Kama simba anayepanda kutoka vichaka vya Yordani  
kuja kwenye nchi ya malisho mengi,  
ndivyo nitakavyomfukuza Babeli kutoka nchi yake ghafula.  
Ni nani aliye mteule,  
nitakayemweka kwa ajili ya jambo hili?  
Ni nani aliye kama mimi,  
na ni nani awezaye kunipinga?  
Tena ni mchungaji yupi  
awezaye kusimama kinyume nami?”   
 45 Kwa hiyo, sikia ambacho Mwenyezi Mungu amepanga dhidi ya Babeli,  
kile alichokusudia dhidi ya nchi ya Wakaldayo:  
Aliye mchanga katika kundi ataburutwa mbali.  
Yeye ataharibu kabisa malisho yao kwa sababu yao.   
 46 Kwa sauti ya kutekwa kwa Babeli, dunia itatetemeka;  
kilio chake kitasikika pote miongoni mwa mataifa.