2
Arusi huko Kana
Siku ya tatu kulikuwa na arusi katika mji wa Kana ya Galilaya, naye mama yake Isa alikuwepo. Isa pamoja na wanafunzi wake walikuwa wamealikwa arusini pia. Divai ilipokwisha, mama yake Isa akamwambia, “Wameishiwa na divai.”
Isa akamwambia, “Mama, kwa nini unanihusisha? Saa yangu haijawadia.”
Mama yake akawaambia wale watumishi, “Fanyeni lolote atakalowaambia.”
Basi hapo palikuwa na mitungi sita iliyotengenezwa kwa mawe; iliwekwa hapo kwa ajili ya desturi ya Kiyahudi ya kujitakasa; kila mtungi ungeweza kuchukua vipipa viwili au vitatu*Kipipa kimoja chenye ujazo wa lita 40..
Isa akawaambia wale watumishi, “Ijazeni hiyo mitungi maji.” Nao wakaijaza ile mitungi hadi juu.
Kisha akawaambia, “Sasa choteni hayo maji kidogo; mpelekeeni mkuu wa sherehe.”
Hivyo wakachota, wakampelekea. Yule mkuu wa sherehe akayaonja yale maji ambayo yalikuwa yamebadilishwa kuwa divai. Hakujua divai hiyo ilikotoka ingawa wale watumishi waliochota yale maji walifahamu. Basi akamwita bwana arusi kando, 10 akamwambia, “Watu wote hutoa divai nzuri kwanza, kisha huleta ile divai hafifu wageni wakisha kunywa sana; lakini wewe umeiweka ile nzuri zaidi hadi sasa.”
11 Huu ndio muujiza wa kwanza wa Isa; aliufanya huko Kana ya Galilaya. Hivyo Isa alidhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.
12 Baada ya hayo, Isa pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, walishuka hadi Kapernaumu, wakakaa huko siku chache.
Isa atakasa Hekalu
(Mathayo 21:12-17; Marko 11:15-17; Luka 19:45-48)
13 Ilipokaribia wakati wa Pasaka ya WayahudiSherehe iliyowakumbusha Waisraeli jinsi Mwenyezi Mungu alivyowakomboa kutoka utumwani huko Misri., Isa alipanda kwenda Yerusalemu. 14 Huko uani la Hekalu aliwakuta watu wakiuza ng’ombe, kondoo na njiwa, nao wengine walikuwa wameketi mezani wakibadili fedha. 15 Akatengeneza mjeledi kutokana na kamba, akawafukuza wote kutoka ua la Hekalu, pamoja na kondoo na ng’ombe. Akazipindua meza za wale wabadili fedha na kuzimwaga fedha zao. 16 Akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, “Waondoeni hapa! Mnathubutuje kuifanya nyumba ya Baba yangu kuwa mahali pa biashara?”
17 Wanafunzi wake wakakumbuka kuwa imeandikwa: “Wivu wa nyumba yako utanila.”
18 Ndipo Wayahudi wakamuuliza, “Unaweza kutuonesha ishara gani ili kuthibitisha mamlaka uliyo nayo ya kufanya mambo haya yote?”
19 Isa akawajibu, “Libomoeni hili Hekalu, nami nitalijenga tena kwa siku tatu!”
20 Wale Wayahudi wakamjibu, “Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita, nawe wasema utalijenga kwa siku tatu?” 21 Lakini yeye Hekalu alilozungumzia ni mwili wake. 22 Baada ya kufufuliwa kutoka kwa wafu, wanafunzi wake wakakumbuka yale aliyokuwa amesema. Ndipo wakayaamini Maandiko na yale maneno Isa alikuwa ameyasema.
23 Ikawa Isa alipokuwa Yerusalemu kwenye Sikukuu ya Pasaka, watu wengi waliona ishara na miujiza aliyokuwa akifanya, nao wakaamini katika jina lake. 24 Lakini Isa hakujiaminisha kwao, kwa sababu aliwajua wanadamu wote. 25 Hakuhitaji ushuhuda wa mtu yeyote kuhusu mwanadamu, kwa kuwa alijua yote yaliyokuwa moyoni mwa kila mtu.

*2:6 Kipipa kimoja chenye ujazo wa lita 40.

2:13 Sherehe iliyowakumbusha Waisraeli jinsi Mwenyezi Mungu alivyowakomboa kutoka utumwani huko Misri.