4
Isa azungumza na mwanamke Msamaria
Isa alipata habari kuwa Mafarisayo*Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. walisikia kwamba yeye alikuwa akipata wanafunzi kuliko Yahya na kuwabatiza, ingawa kwa kweli si Isa mwenyewe aliyekuwa akibatiza, ila ni wanafunzi wake. Bwana Isa alipojua mambo haya, aliondoka Yudea akarudi tena Galilaya.
Wakati huo ilimlazimu apitie Samaria. Akafika kwenye mji mmoja wa Samaria uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa mwanawe Yusufu. Kisima cha Yakobo kilikuwa huko. Naye Isa alikuwa amechoka kwa kuwa alikuwa ametoka safarini. Akaketi karibu na hicho kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana.
Mwanamke mmoja Msamaria alipokuja kuteka maji, Isa akamwambia, “Naomba maji ninywe.” (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wameenda mjini kununua chakula.)
Yule mwanamke Msamaria akamjibu, “Wewe ni Myahudi na mimi ni Msamaria. Yawezekanaje uniombe maji ya kunywa?” (Wayahudi walikuwa hawashirikiani kabisa na Wasamaria.)
10 Isa akamjibu, “Kama ungeijua karama ya Mungu, na ni nani anakuomba maji ya kunywa, ungemwomba yeye, naye angekupa maji ya uzima.”
11 Yule mwanamke akamjibu, “BwanaWale ambao hawakumfahamu Isa kuwa Masihi walimwita “Bwana” kwa heshima ya kawaida., wewe huna chombo cha kutekea maji na kisima hiki ni kirefu. Hayo maji ya uzima utayapata wapi? 12 Kwani wewe ni mkuu kuliko baba yetu Yakobo ambaye alitupatia kisima hiki, ambacho yeye pamoja na watoto wake na mifugo yake walikitumia?”
13 Isa akamjibu, “Kila mtu anayekunywa maji ya kisima hiki ataona kiu tena. 14 Lakini yeyote anywaye maji nitakayompa hataona kiu kamwe. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujika uzima wa milele.”
15 Yule mwanamke akamwambia, “Bwana, tafadhali nipe maji hayo ili nisipate kiu tena, wala nisije tena hapa kuteka maji!”
16 Isa akamjibu, “Nenda ukamwite mumeo, uje naye hapa.”
17 Yule mwanamke akajibu, “Sina mume.”
Isa akamwambia, “Umesema kweli kuwa huna mume. 18 Kwa maana umeshakuwa na wanaume watano, na mwanaume unayeishi naye sasa si mume wako! Umesema ukweli.”
19 Yule mwanamke akasema, “Bwana, naona bila shaka wewe ni nabii. 20 Baba zetu waliabudu kwenye mlima huu, lakini ninyi Wayahudi mnasema ni lazima tukaabudu huko Yerusalemu.”
21 Isa akamjibu, “Mwanamke, niamini: wakati unakuja ambapo hamtamwabudu BabaJina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. katika mlima huu, wala huko Yerusalemu. 22 Ninyi Wasamaria mnaabudu msichokijua. Sisi Wayahudi tunamwabudu Mungu tunayemjua kwa sababu wokovu unatoka kwa Wayahudi. 23 Lakini saa yaja, tena ipo, ambapo wale waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba anawatafuta watu wanaomwabudu kwa namna hii. 24 Mungu ni Roho, na wote wanaomwabudu imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”
25 Yule mwanamke akamwambia, “Ninafahamu kwamba Al-Masihi” (yaani Aliyetiwa mafuta) “anakuja. Yeye akija, atatueleza mambo yote.”
26 Isa akamwambia, “Mimi ninayezungumza nawe, ndiye.”
27 Wakati huo wanafunzi wake wakarudi, wakashangaa sana kumwona akizungumza na mwanamke. Lakini hakuna aliyemuuliza, “Unataka nini kwake?” Au, “Kwa nini unazungumza naye?”
28 Yule mwanamke akaacha mtungi wake, akarudi mjini, akawaambia watu, 29 “Njooni mkamwone mtu aliyeniambia kila kitu nilichotenda! Je, yawezekana huyu ndiye Al-Masihi§Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta.?” 30 Basi wakamiminika watu kutoka mjini, wakamwendea Isa.
31 Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wakimsihi, “Mwalimu, kula.”
32 Lakini yeye akawajibu, “Mimi ninacho chakula ambacho ninyi hamkifahamu.”
33 Basi wanafunzi wakaanza kuulizana, “Kuna mtu ambaye amemletea chakula?”
34 Lakini Isa akawajibu, “Chakula changu ni kufanya mapenzi ya Mungu ambaye amenituma na kuikamilisha kazi yake. 35 Je, ninyi hamsemi, ‘Bado miezi minne tuvune’? Inueni macho yenu myaangalie mashamba jinsi mazao yalivyo tayari kuvunwa! 36 Mvunaji tayari anapokea mshahara wake, naye anakusanya mazao kwa ajili ya uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wafurahi pamoja. 37 Hivyo ule msemo, ‘Mmoja hupanda na mwingine huvuna,’ ni kweli kabisa. 38 Niliwatuma mkavune mazao ambayo hamkupanda. Wengine walifanya kazi ngumu, nanyi mmevuna faida ya taabu yao.”
Wasamaria wengi waamini
39 Wasamaria wengi katika mji ule wakamwamini Isa kwa sababu ya ushuhuda wa yule mwanamke alipowaambia kwamba, “Ameniambia kila kitu nilichotenda.” 40 Hivyo wale Wasamaria walipomjia, wakamsihi akae kwao. Naye akakaa huko siku mbili. 41 Kwa sababu ya neno lake, watu wengi wakaamini.
42 Wakamwambia yule mwanamke, “Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu, bali kwa kuwa tumemsikia sisi wenyewe. Tumejua hakika kwamba huyu ndiye Al-Masihi, Mwokozi wa ulimwengu.”
Isa amponya mwana wa afisa
43 Baada ya zile siku mbili, Isa aliondoka kwenda Galilaya. 44 (Basi Isa mwenyewe alikuwa amesema kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe.) 45 Alipofika Galilaya, Wagalilaya walimkaribisha, kwani walikuwa wameona yale aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa Sikukuu ya Pasaka. Kwa maana wao pia walikuwa wamehudhuria hiyo Sikukuu.
46 Hivyo Isa akafika tena Kana ya Galilaya, kule alikuwa amebadili maji kuwa divai. Kulikuwa na afisa mmoja wa mfalme, ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu. 47 Huyo mtu aliposikia kwamba Isa alikuwa amewasili Galilaya kutoka Yudea, alimwendea na kumsihi aende akamponye mwanawe, aliyekuwa mgonjwa karibu ya kufa.
48 Isa akamwambia, “Ninyi watu msipoona ishara na miujiza kamwe hamtaamini.”
49 Yule afisa wa mfalme akamwambia, “Bwana, tafadhali shuka kabla mwanangu hajafa.”
50 Isa akamjibu, “Nenda zako, mwanao yu hai.”
Yule afisa akaamini yale maneno Isa aliyomwambia, akaenda zake. 51 Alipokuwa bado yuko njiani, akakutana na watumishi wake, wakamwambia kwamba mwanawe yu mzima. 52 Akawauliza saa ambayo alianza kupata nafuu. Wakamwambia, “Jana saa saba, ndipo homa iliisha.”
53 Ndipo baba wa huyo mtoto akakumbuka kuwa huo ndio wakati Isa alikuwa amemwambia, “Mwanao yu hai.” Kwa hiyo yeye na wote wa nyumbani mwake wakamwamini Isa.
54 Hii ilikuwa ishara ya pili ambayo Isa alifanya aliporudi Galilaya kutoka Yudea.

*4:1 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli.

4:11 Wale ambao hawakumfahamu Isa kuwa Masihi walimwita “Bwana” kwa heshima ya kawaida.

4:21 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi.

§4:29 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta.