7
Kutokuamini kwa ndugu zake Isa
1 Baada ya mambo haya, Isa alienda sehemu mbalimbali za Galilaya. Hakutaka kwenda Yudea kwa sababu viongozi wa Wayahudi huko walitaka kumuua. 2 Sikukuu ya Vibanda ya Wayahudi ilikuwa imekaribia. 3 Hivyo ndugu zake Isa wakamwambia, “Ondoka hapa uende Yudea ili wanafunzi Wako wapate kuona miujiza unayofanya. 4 Mtu anayetaka kujulikana hafanyi mambo yake kwa siri. Kama unafanya mambo haya, jioneshe kwa ulimwengu.” 5 Hata ndugu zake mwenyewe hawakumwamini.
6 Isa akawaambia, “Wakati wangu bado haujawadia, lakini wakati wenu upo siku zote. 7 Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini unanichukia mimi kwa sababu ninawashuhudia kwamba matendo yao ni maovu. 8 Ninyi nendeni kwenye Sikukuu, lakini mimi sitahudhuria Sikukuu hii kwa sababu wakati wangu haujawadia.” 9 Baada ya kusema hayo, akabaki Galilaya.
Isa kwenye Sikukuu ya Vibanda
10 Lakini ndugu zake walipokwisha kuondoka kwenda kwenye Sikukuu, yeye pia alienda lakini kwa siri. 11 Viongozi wa Wayahudi walikuwa wakimtafuta huko kwenye Sikukuu na kuulizana, “Yuko wapi huyu mtu?”
12 Kulikuwa na minong’ono iliyoenea kumhusu Isa katika umati wa watu, wakati wengine wakisema, “Ni mtu mwema.”
Wengine walikuwa wakisema, “La, yeye anawadanganya watu.” 13 Lakini hakuna mtu yeyote aliyemsema waziwazi kwa sababu ya kuwaogopa viongozi wa Wayahudi.
Isa afundisha kwenye Sikukuu
14 Ilipokaribia katikati ya Sikukuu, Isa alipanda kwenda Hekaluni na kuanza kufundisha. 15 Wayahudi wakastaajabia mafundisho yake wakasema, “Mtu huyu amepataje kujua mambo haya bila kufundishwa?”
16 Ndipo Isa akawajibu, “Mafundisho yangu si yangu mwenyewe, bali yanatoka kwake yeye aliyenituma. 17 Mtu yeyote akipenda kufanya mapenzi ya Mungu, atajua kama mafundisho yangu yanatoka kwa Mungu au ninasema kwa ajili yangu mwenyewe. 18 Wale wanenao kwa ajili yao wenyewe hufanya hivyo kwa kutaka utukufu wao wenyewe. Lakini yeye atafutaye utukufu wa yule aliyemtuma ni wa kweli, wala hakuna uongo ndani yake. 19 Je, Musa hakuwapa ninyi sheria? Lakini hakuna hata mmoja wenu anayeishika hiyo sheria. Kwa nini mnataka kuniua?”
20 Ule umati wa watu wakamjibu, “Wewe una pepo mchafu! Ni nani anayetaka kukuua?”
21 Isa akawajibu, “Nimefanya muujiza mmoja na nyote mkastaajabu. 22 Lakini kwa kuwa Musa aliwaamuru tohara (ingawa kwa kweli haikutoka kwa Musa bali kwa baba zetu wa zamani), mnamtahiri mtoto hata siku ya Sabato. 23 Ikiwa mtoto aweza kutahiriwa siku ya Sabato kusudi Torati ya Musa isivunjwe, kwa nini mnanikasirikia kwa kumponya mtu mwili wake wote siku ya Sabato? 24 Acheni kuhukumu mambo kwa jinsi mnavyoona tu, bali hukumuni kwa haki.”
Je, Isa ndiye Al-Masihi?
25 Ndipo baadhi ya watu wa Yerusalemu wakawa wanasema, “Tazameni, huyu si yule mtu wanayetaka kumuua? 26 Mbona yuko hapa anazungumza hadharani, na wala hawamwambii neno lolote? Je, inawezekana viongozi wanafahamu kuwa huyu ndiye Al-Masihi*Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta.? 27 Tunafahamu huyu mtu anakotoka, lakini Al-Masihi atakapokuja, hakuna yeyote atakayejua atokako.”
28 Ndipo Isa, akaendelea kufundisha Hekaluni, akisema, “Ninyi mnanifahamu na kujua nitokako. Mimi sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, bali yeye aliyenituma ni wa kweli na ninyi hammjui. 29 Mimi namjua kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye alinituma.”
30 Ndipo wakatafuta kumkamata, lakini hakuna mtu yeyote aliyethubutu kumshika kwa sababu saa yake ilikuwa bado haijawadia. 31 Nao watu wengi wakamwamini, wakasema, “Je, Al-Masihi atakapokuja, atafanya miujiza mikuu kuliko aliyoifanya mtu huyu?”
Walinzi wanatumwa kumkamata Isa
32 Mafarisayo†Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. wakasikia watu wakinong’ona mambo kama hayo kuhusu Isa, ndipo wao pamoja na viongozi wa makuhani wakatuma walinzi wa Hekalu waende kumkamata.
33 Isa akasema, “Mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo, kisha nitarudi kwake yeye aliyenituma. 34 Mtanitafuta lakini hamtaniona, nami niliko ninyi hamwezi kuja.”
35 Wayahudi wakaulizana wao kwa wao, “Huyu mtu anataka kwenda wapi ambako hatuwezi kumfuata? Je, anataka kwenda kwa Wayunani ambako baadhi ya watu wetu wametawanyikia, akawafundishe Wayunani? 36 Yeye ana maana gani anaposema, ‘Mtanitafuta lakini hamtaniona,’ na, ‘nami niliko ninyi hamwezi kuja’?”
Mito ya maji ya uzima
37 Siku ile ya mwisho ya Sikukuu, siku ile kuu, wakati Isa akiwa amesimama huko, akapaza sauti yake akasema, “Kama mtu yeyote anaona kiu na aje kwangu anywe. 38 Yeyote aniaminiye mimi, kama Maandiko yanavyosema, vijito vya maji ya uzima vitatiririka kutoka ndani yake.” 39 Isa aliposema haya, alimaanisha Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye wote waliomwamini wangempokea. Kwa maana hadi wakati huo Roho wa Mungu alikuwa hajatolewa, kwa kuwa Isa alikuwa bado hajatukuzwa.
Mgawanyiko miongoni mwa watu
40 Waliposikia maneno hayo, baadhi ya watu miongoni mwa umati ule wakasema, “Hakika huyu ndiye yule Nabii.”
41 Wengine wakasema, “Huyu ndiye Al-Masihi!”
Lakini wengine wakauliza, “Je, Al-Masihi kwao ni Galilaya? 42 Je, Maandiko hayasemi kwamba Al-Masihi atakuja kutoka jamaa ya Daudi na kutoka Bethlehemu, mji alioishi Daudi?” 43 Kwa hiyo watu wakagawanyika kwa ajili ya Isa. 44 Baadhi yao walitaka kumkamata, lakini hakuna aliyethubutu kumgusa.
Kutokuamini kwa viongozi wa Wayahudi
45 Hatimaye wale walinzi wa Hekalu wakarudi kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliokuwa wamewatuma ili kumkamata Isa, wakaulizwa, “Mbona hamkumkamata?”
46 Wale walinzi wakajibu, “Kamwe hajanena mtu yeyote kama yeye anenavyo.”
47 Mafarisayo wakajibu, “Je, nanyi pia mmedanganyika? 48 Je, kuna kiongozi yeyote au mmoja wa Mafarisayo ambaye amemwamini? 49 Lakini umati huu wa watu wasiojua Torati ya Musa, wamelaaniwa.”
50 Ndipo Nikodemo, yule aliyekuwa amemwendea Isa siku moja usiku, na alikuwa mmoja wao, akauliza, 51 “Je, sheria zetu zinaturuhusu kumhukumu mtu kabla ya kumsikiliza na kufahamu alilotenda?”
52 Wakamjibu, “Je, wewe pia unatoka Galilaya? Chunguza nawe utaona kwamba hakuna nabii atokae Galilaya!”
[ 53 Kisha wakaondoka, kila mtu akarudi nyumbani mwake.