17
Isa ajiombea mwenyewe
Baada ya Isa kusema haya, alitazama kuelekea mbinguni akawaombea na kusema:
“Baba*Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu., saa imewadia. Mtukuze Mwanao, ili Mwanao apate kukutukuza wewe. Kwa kuwa umempa mamlaka juu ya wote wenye mwili ili awape uzima wa milele wale uliompa. Nao uzima wa milele ndio huu: wakujue wewe uliye Mungu wa pekee wa kweli, na Isa Al-Masihi uliyemtuma. Nimekutukuza wewe duniani kwa kuitimiza ile kazi uliyonipa niifanye. Hivyo sasa, Baba, unitukuze mbele zako kwa ule utukufu niliokuwa nao pamoja na wewe kabla ulimwengu haujaumbwa.
Isa awaombea wanafunzi wake
“Nimelidhihirisha jina lako kwa wale ulionipa kutoka ulimwengu. Walikuwa wako, nawe ukanipa mimi, nao wamelitii neno lako. Sasa wamejua ya kuwa vyote ulivyonipa vimetoka kwako, kwa kuwa maneno yale uliyonipa nimewapa wao, nao wameyapokea na kujua kwamba kweli nimetoka kwako, nao wameamini kuwa wewe ulinituma. Ninawaombea wao. Siuombei ulimwengu, bali nawaombea wale ulionipa kwa sababu wao ni wako. 10 Wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu, nami nimetukuzwa ndani yao. 11 Mimi sasa simo tena ulimwenguni, lakini wao bado wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba Mtakatifu, uwalinde kwa uweza wa jina lako ulilonipa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja. 12 Nilipokuwa pamoja nao, niliwalinda, wakawa salama kwa lile jina ulilonipa. Hakuna hata mmoja aliyepotea, isipokuwa yule aliyekusudiwa upotevu, ili Maandiko yapate kutimia.
13 “Lakini sasa naja kwako, nami ninasema mambo haya wakati bado nikiwa ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu kamili ndani yao. 14 Nimewapa neno lako, nao ulimwengu umewachukia, kwa kuwa wao si wa ulimwengu kama mimi nisivyo wa ulimwengu huu. 15 Siombi kwamba uwaondoe ulimwenguni, bali uwalinde dhidi ya yule mwovu. 16 Wao si wa ulimwengu huu, kama vile mimi nisivyo wa ulimwengu. 17 Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndilo kweli. 18 Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami nawatuma vivyo hivyo. 19 Kwa ajili yao najiweka wakfu ili wao nao wapate kutakaswa katika ile kweli.
Isa awaombea wote watakaomwamini
20 “Siwaombei hawa peke yao, bali nawaombea na wale wote watakaoniamini kupitia neno lao, 21 ili wawe na umoja kama vile wewe Baba ulivyo ndani yangu na mimi nilivyo ndani yako. Wao nao wawe ndani yetu, ili ulimwengu upate kuamini ya kuwa wewe ndiwe uliyenituma mimi. 22 Utukufu ule ulionipa nimewapa wao, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo wamoja. 23 Mimi ndani yao na wewe ndani yangu: ili wawe wamekamilika katika umoja, na ulimwengu upate kujua ya kuwa umenituma, nami nimewapenda wao kama unavyonipenda mimi.
24 “Baba, shauku yangu ni kwamba wale ulionipa wawe pamoja nami pale nilipo, ili waweze kuuona utukufu wangu, yaani utukufu ule ulionipa kwa kuwa ulinipenda hata kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu.
25 “Baba Mwenye Haki, ingawa ulimwengu haukujui, mimi ninakujua, nao wanajua ya kuwa umenituma. 26 Nimefanya jina lako lijulikane kwao, nami nitaendelea kufanya lijulikane, ili upendo ule unaonipenda mimi uwe ndani yao, na mimi mwenyewe nipate kuwa ndani yao.”

*17:1 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu.