21
Isa awatokea wanafunzi saba
1 Baada ya haya Isa akawatokea tena wanafunzi wake kando ya Bahari ya Tiberia*yaani Bahari ya Galilaya. Yeye alijionesha kwao hivi: 2 Simoni Petro, Tomaso (aitwaye Didimasi†yaani Pacha), Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, wana wa Zebedayo, na wanafunzi wengine wawili walikuwa pamoja. 3 Simoni Petro akawaambia wenzake, “Mimi naenda kuvua samaki.” Nao wakamwambia, “Tutaenda pamoja nawe.” Wakatoka, wakaingia ndani ya mashua, lakini usiku ule hawakupata chochote.
4 Mara baada ya kupambazuka, Isa akasimama ufuoni, lakini wanafunzi hawakumtambua kwamba alikuwa Isa.
5 Isa akawaambia, “Wanangu, je, mna samaki wowote?”
Wakamjibu, “La.”
6 Akawaambia, “Shusheni nyavu upande wa kuume wa mashua yenu nanyi mtapata samaki.” Wakashusha nyavu, na tazama, wakapata samaki wengi mno hata wakashindwa kuvutia zile nyavu zilizojaa samaki ndani ya mashua.
7 Basi yule mwanafunzi aliyependwa na Isa akamwambia Petro, “Huyu ni Bwana Isa!” Simoni Petro aliposikia kwamba ni Bwana Isa, akajifunga nguo yake (kwa kuwa alikuwa ameitoa), naye akajitosa baharini. 8 Wale wanafunzi wengine wakaja kwa ile mashua huku wakikokota ule wavu uliojaa samaki, maana hawakuwa mbali na nchi kavu, ilikuwa yapata dhiraa mia mbili‡Dhiraa 200 ni kama mita 90.. 9 Walipofika ufuoni, wakaona moto wa makaa na samaki wakiokwa juu yake, na mikate.
10 Isa akawaambia, “Leteni baadhi ya hao samaki mliovua sasa hivi.”
11 Simoni Petro akapanda kwenye mashua na kuukokota ule wavu ufuoni. Ulikuwa umejaa samaki wakubwa mia moja hamsini na watatu (153). Ingawa samaki walikuwa wengi kiasi hicho, ule wavu haukuchanika. 12 Isa akawaambia, “Njooni mpate kifungua kinywa.” Hakuna hata mmoja wa wanafunzi aliyethubutu kumuuliza, “Wewe ni nani?” Walijua kuwa ni Bwana Isa. 13 Isa akaja, akachukua ule mkate, akawapa, na vivyo hivyo akawagawia wale samaki. 14 Hii ilikuwa mara ya tatu Isa kuwatokea wanafunzi wake baada yake kufufuliwa kutoka kwa wafu.
Isa amrejesha Petro
15 Walipokwisha kula, Isa akamuuliza Simoni Petro, “Je, Simoni mwana wa Yohana, unanipenda kweli kuliko hawa?”
Yeye akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.”
Isa akamwambia, “Lisha wana-kondoo wangu.”
16 Isa akamuuliza tena, “Simoni, mwana wa Yohana, wanipenda?”
Petro akamjibu, “Ndiyo Bwana, wewe unajua ya kuwa ninakupenda.”
Isa akamwambia, “Chunga kondoo wangu.”
17 Kwa mara ya tatu Isa akamuuliza Petro, “Simoni mwana wa Yohana, unanipenda?”
Petro akahuzunika sana kwa kuwa Isa alimuuliza mara ya tatu, “Unanipenda?” Akamjibu, “Bwana, wewe unajua yote, unajua ya kuwa ninakupenda.”
Isa akamwambia, “Lisha kondoo wangu. 18 Amin, amin nakuambia, ulipokuwa kijana ulivaa na kwenda unakotaka. Lakini utakapokuwa mzee, utanyoosha mikono yako na mtu mwingine atakuvika na kukupeleka usipotaka kwenda.” 19 Isa alisema haya ili kuashiria aina ya kifo ambacho Petro angemtukuza nacho Mungu. Kisha Isa akamwambia Petro, “Nifuate!”
20 Petro akageuka, akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Isa akiwafuata. (Huyu ndiye yule mwanafunzi aliyeegama kifuani mwa Isa walipokula naye chakula cha mwisho na kuuliza, “Bwana, ni nani atakayekusaliti?”) 21 Petro alipomwona huyo mwanafunzi, akamuuliza Isa, “Bwana, na huyu je?”
22 Isa akamjibu, “Ikiwa nataka aishi hadi nitakaporudi, inakuhusu nini? Wewe inakupasa unifuate!” 23 Kwa sababu ya maneno haya ya Isa, uvumi ukaenea miongoni mwa ndugu kwamba huyu mwanafunzi hangekufa. Lakini Isa hakusema kuwa hangekufa. Yeye alisema tu kwamba, “Ikiwa nataka aishi hadi nitakaporudi, inakuhusu nini?”
24 Huyu ndiye yule mwanafunzi anayeshuhudia mambo haya, na ndiye ameandika habari hizi. Nasi tunajua ya kuwa ushuhuda wake ni kweli.
25 Lakini kuna mambo mengine mengi ambayo Isa alifanya. Kama yote yangeandikwa, nadhani hata ulimwengu wote haungekuwa na nafasi ya kutosha kuweka vitabu ambavyo vingeandikwa.