2
Jaribu la pili la Ayubu
Siku nyingine wana wa Mungu walienda kujionesha mbele za Mwenyezi Mungu. Shetani naye akaja pamoja nao kujionesha mbele zake. Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani, “Umetoka wapi?”
Shetani akamjibu Mwenyezi Mungu, “Natoka kuzunguka duniani, nikitembea huku na huko.”
Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Hakuna mtu mwingine duniani aliye kama yeye, mtu asiye na hatia, ni mnyofu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Naye bado anadumisha uadilifu wake, ingawa ulinichochea dhidi yake, ili nimwangamize pasipo sababu.”
Shetani akamjibu Mwenyezi Mungu, “Ngozi kwa ngozi! Mwanadamu atatoa vyote alivyo navyo kwa ajili ya uhai wake. Lakini nyoosha mkono wako na kuipiga nyama yake na mifupa yake, naye kwa hakika atakulaani mbele za uso wako.”
Mwenyezi Mungu akamwambia Shetani, “Vema sana; kwa hiyo, yeye yumo mikononi mwako, lakini lazima umwachie uhai wake.”
Basi Shetani akatoka mbele za Mwenyezi Mungu, naye akampiga Ayubu kwa majipu mabaya tangu nyayo za miguu yake hadi utosi wa kichwa. Ndipo Ayubu akachukua kigae na kujikuna nacho, huku akiketi kwenye majivu.
Mke wake akamwambia, “Je, bado unashikamana na uadilifu wako? Mlaani Mungu nawe ukafe!”
10 Akamjibu, “Unazungumza kama mwanamke mpumbavu*maana yake kupungukiwa maadili. Je, tupokee mema kutoka kwa Mungu, bali tusipokee mabaya?”
Katika mambo haya yote, Ayubu hakutenda dhambi katika kusema kwake.
 
Rafiki watatu wa Ayubu
11 Basi rafiki watatu wa Ayubu, ndio Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi na Sofari Mnaamathi, waliposikia kuhusu taabu yote iliyompata Ayubu, wakajipanga kutoka nyumbani mwao, wakakutana ili kwenda kumtuliza katika taabu hiyo na kumfariji. 12 Walipomwona kwa mbali, ilikuwa vigumu kumtambua. Wakaanza kulia kwa sauti kubwa, wakayararua majoho yao na kujirushia mavumbi juu ya vichwa vyao. 13 Kisha wakaketi chini kwenye udongo pamoja na Ayubu kwa siku saba usiku na mchana. Hakuna yeyote aliyesema naye neno, kwa sababu waliona jinsi mateso yake yalivyokuwa makubwa.

*2:10 maana yake kupungukiwa maadili