4
Elifazi anasema: Ayubu ametenda dhambi
Ndipo Elifazi Mtemani akajibu:
“Kama mtu akithubutu kuzungumza nawe,
kutakukasirisha?
Lakini ni nani awezaye
kujizuia asiseme?
Fikiri jinsi umewafundisha watu wengi,
jinsi umeitia nguvu
mikono iliyokuwa dhaifu.
Maneno yako yamewategemeza wale waliojikwaa;
umeyatia nguvu magoti yaliyokuwa dhaifu.
Lakini sasa hii taabu imekujia wewe,
nawe unashuka moyo;
imekupiga wewe,
nawe unafadhaika.
Je, kumcha Mungu kwako hakupaswi kuwa
ndiyo matumaini yako
na njia zako kutokuwa na lawama
ndilo taraja lako?
 
“Fikiri sasa: Ni mtu yupi asiye na hatia
ambaye aliwahi kuangamia?
Ni wapi wanyofu
waliwahi kuangamizwa?
Kwa jinsi mimi nimechunguza,
wale walimao ubaya
na wale hupanda uovu,
huvuna hayo hayo.
Kwa pumzi ya Mungu huangamizwa;
kwa mshindo wa hasira zake huangamia.
10 Simba anaweza kunguruma na kukoroma,
lakini bado meno ya simba mkubwa huvunjika.
11 Simba anaweza kuangamia kwa kukosa mawindo,
nao wana wa simba jike hutawanyika.
 
12 “Neno lililetwa kwangu kwa siri,
masikio yangu yakasikia mnong’ono wake.
13 Katikati ya ndoto za kutia wasiwasi wakati wa usiku,
hapo usingizi mzito uwapatapo wanadamu,
14 hofu na kutetemeka kulinishika
na kufanya mifupa yangu yote itetemeke.
15 Kuna roho aliyepita mbele ya uso wangu,
nazo nywele za mwili wangu zikasimama.
16 Yule roho akasimama,
lakini sikuweza kutambua kilikuwa kitu gani.
Umbo fulani lilisimama mbele ya macho yangu,
kukawa na ukimya kisha nikasikia sauti:
17 ‘Je, binadamu aweza kuwa mwadilifu kuliko Mungu?
Je, mtu aweza kuwa safi kuliko Muumba wake?
18 Ikiwa Mungu hawaamini watumishi wake,
ikiwa yeye huwalaumu malaika wake kwa kukosea,
19 ni mara ngapi zaidi wale wanaoishi katika nyumba
za udongo wa mfinyanzi,
ambazo misingi yake ipo mavumbini,
ambao wamepondwa kama nondo!
20 Kati ya mawio na machweo
huvunjwa vipande vipande;
bila yeyote kutambua,
huangamia milele.
21 Je, kamba za hema lao hazikung’olewa,
hivyo hufa bila hekima?’