31
Ayubu anakamilisha maneno yake
“Nimefanya agano na macho yangu
yasimtazame msichana kwa kumtamani.
Kwa kuwa fungu la mwanadamu ni lipi kutoka kwa Mungu juu,
urithi wake kutoka juu kwa Mwenyezi?
Je, si uharibifu kwa watu waovu,
maangamizi kwa wale watendao mabaya?
Je, yeye hazioni njia zangu
na kuihesabu kila hatua yangu?
 
“Kama nimeishi katika uongo
au mguu wangu umekimbilia udanganyifu,
Mungu na anipime katika mizani za uaminifu,
naye atajua kwamba sina hatia:
kama hatua zangu zimepotoka kutoka njia,
kama moyo wangu umeongozwa na macho yangu,
au kama mikono yangu imetiwa unajisi,
basi wengine na wale nilichokipanda,
nayo yale yote niliyootesha na yang’olewe.
 
“Kama moyo wangu umeshawishiwa na mwanamke,
au kama nimevizia mlangoni mwa jirani yangu,
10 basi mke wangu na asage nafaka ya mwanaume mwingine,
nao wanaume wengine walale naye.
11 Kwa kuwa hilo lingekuwa aibu,
naam, dhambi ya kuhukumiwa.
12 Ni moto uwakao kwa Uharibifu*Kwa Kiebrania ni Abadon (Ayubu 26:6; Mithali 15:11).;
ungekuwa umeng’oa mavuno yangu.
 
13 “Kama ningewanyima haki watumishi wangu wanaume au vijakazi wangu,
walipokuwa na manung’uniko dhidi yangu,
14 nitafanya nini Mungu atakaponikabili?
Nitamjibu nini nitakapoitwa kujitetea?
15 Je, yeye aliyeniumba tumboni mwa mama yangu,
siye aliyewaumba?
Je, si ni yeye huyo mmoja aliyetuumba sote
ndani ya mama zetu?
 
16 “Ikiwa nimewanyima maskini haja zao,
au kuyaacha macho ya wajane yadhoofike,
17 kama nimekula chakula changu mwenyewe,
bila kuwashirikisha yatima;
18 lakini tangu ujana wangu nimemlea yatima kama ambavyo baba angefanya,
nami tangu kuzaliwa kwangu nimewaongoza wajane:
19 kama nilimwona yeyote akiteseka kwa kukosa nguo,
au mtu mhitaji asiye na mavazi,
20 ambaye wala moyo wake haukunibariki
kwa kumpatia joto kwa mavazi ya manyoya ya kondoo wangu,
21 na kama nimeinua mkono wangu dhidi ya yatima,
nikijua kuwa nina ushawishi mahakamani,
22 basi mkono wangu na unyofoke toka begani mwangu,
nao na uvunjike kutoka kiungio chake.
23 Kwa kuwa niliogopa uharibifu kutoka kwa Mungu,
nami kwa kuuogopa utukufu wake sikuweza kufanya mambo kama hayo.
 
24 “Kama nimeweka tumaini langu kwenye dhahabu,
au kuiambia dhahabu safi, ‘Wewe ndiwe salama yangu,’
25 kama nimefurahia wingi wa utajiri wangu,
ustawi ambao mikono yangu ilikuwa imepata,
26 kama nimelitazama jua katika kung’aa kwake
au mwezi ukienda kwa fahari yake,
27 hivyo moyo wangu kushawishiwa kwa siri,
au kubusu mkono wangu kwa kuviheshimu,
28 basi hiyo pia ingekuwa dhambi ya kuhukumiwa,
kwa kuwa ningekuwa si mwaminifu kwa Mungu aishiye juu sana.
 
29 “Kama nimeshangilia msiba wa adui yangu,
au kutazama kwa furaha taabu iliyomjia,
30 lakini sikuruhusu kinywa changu kufanya dhambi
kwa kuomba laana dhidi ya maisha yake;
31 kama watu wa nyumbani mwangu kamwe hawakusema,
‘Ni nani ambaye hajashibishwa na nyama ya Ayubu?’
32 Lakini hakuna mgeni aliyelala njiani,
kwa maana mlango wangu ulikuwa wazi kwa msafiri;
33 kama nimeifunika dhambi yangu kama wanadamu wengine wafanyavyo,
kwa kuficha hatia yangu moyoni mwangu,
34 kwa sababu ya kuogopa umati wa watu,
na hivyo kuwa na hofu ya kudharauliwa na jamaa,
nikakaa kimya, nisitoke nje ya mlango.
 
35 (“Laiti angekuwepo mtu wa kunisikia!
Tazama sasa ninatia sahihi kwenye utetezi wangu:
Mwenyezi na anijibu;
mshtaki wangu na aweke mashtaka yake kwenye maandishi.
36 Hakika ningeyavaa begani mwangu,
ningeyavaa kama taji.
37 Ningempa hesabu ya kila hatua yangu,
ningemwendea kama mwana wa mfalme.)
 
38 “Kama nchi yangu inalia dhidi yangu,
na mifereji yake yote imelowana kwa machozi,
39 kama nimekula mazao yake bila malipo,
au kuvunja mioyo ya wapangaji wake,
40 basi miiba na iote badala ya ngano,
na magugu badala ya shayiri.”
Mwisho wa maneno ya Ayubu.

*31:12 Kwa Kiebrania ni Abadon (Ayubu 26:6; Mithali 15:11).