36
Elihu atukuza wema wa Mwenyezi Mungu
Elihu akaendelea kusema:
“Nivumilie kidogo zaidi nami nitakuonesha
kwamba yako mengi zaidi ya kusemwa kwa ajili ya Mungu.
Ninayapata maarifa yangu kutoka mbali,
nami nitamhesabia haki Muumba wangu.
Uwe na hakika kwamba maneno yangu si ya uongo;
mmoja aliye mkamilifu katika maarifa yuko pamoja na wewe.
 
“Mungu ni mwenye nguvu, lakini hamdharau mwanadamu;
ni mwenye nguvu, naye ni thabiti katika kusudi lake.
Hawaachi waovu waendelee kuishi,
bali huwapa walioteswa haki yao.
Yeye haondoi macho yake kwa wenye haki;
huwaketisha penye viti vya utawala pamoja na wafalme,
na kuwatukuza milele.
Lakini ikiwa watu wamefungwa kwenye minyororo,
wakiwa wameshikiliwa na kamba za mateso,
huwaonesha yale waliyoyatenda,
kwamba wametenda dhambi kwa majivuno.
10 Huwafanya wao kusikia maonyo,
na huwaagiza kutubu uovu wao.
11 Wakitii na kumtumikia,
wataishi siku zao zilizobaki katika mafanikio,
na miaka yao katika utoshelevu.
12 Lakini wasiposikiliza,
wataangamia kwa upanga,
nao watakufa pasipo maarifa.
 
13 “Wasiomcha Mungu moyoni mwao huficha chuki;
hata anapowafunga, hawamwombi msaada.
14 Wanakufa wangali vijana,
miongoni mwa mahanithi wa mahali pa ibada za sanamu.
15 Bali wao wanaoteseka huwaokoa katika mateso yao,
na kuzungumza nao katika dhiki zao.
 
16 “Yeye anakubembeleza utoke katika mataya ya dhiki,
ili kukuweka mahali palipo na nafasi mbali na kizuizi,
hadi kwenye meza yako ya faraja iliyojaa vyakula vizuri.
17 Lakini sasa umelemewa na hukumu kwa ajili ya uovu;
hukumu na haki vimekukamata.
18 Uwe mwangalifu ili yeyote asikushawishi kwa utajiri;
usipotoshwe kwa fungu kubwa la rushwa.
19 Je, utajiri wako hata nguvu zako nyingi
vinaweza kukusaidia usiingie kwenye dhiki?
20 Usiutamani usiku uje,
ili uwaburute watu mbali na nyumba zao.
21 Jihadhari usigeukie uovu,
ambao unaupenda zaidi ya mateso.
 
22 “Mungu ametukuzwa katika nguvu zake.
Ni nani aliye mwalimu kama yeye?
23 Ni nani aliyemwelekeza katika njia zake,
au kumwambia, ‘Wewe umetenda yasiyo sawa’?
24 Kumbuka kuzitukuza kazi zake,
ambazo watu wamezisifu katika wimbo.
25 Wanadamu wote wameiona;
watu wanaikazia macho kwa mbali.
26 Tazama jinsi Mungu alivyo mkuu,
kupita ufahamu wetu!
Hesabu ya miaka yake haitafutiki.
 
27 “Yeye huvuta juu matone ya maji,
ayachujayo kama mvua kutoka vijito;
28 mawingu huangusha chini maji yake,
nayo mvua nyingi huwanyeshea wanadamu.
29 Ni nani ajuaye jinsi ayatandazavyo mawingu,
jinsi angurumavyo kutoka kwenye hema lake.
30 Tazama anavyotandaza radi yake kumzunguka,
naye huvifunika vilindi vya bahari.
31 Hivi ndivyo atawalavyo mataifa,
na kuwapa chakula kwa wingi.
32 Huujaza mkono wake kwa radi,
na kuiagiza kulenga shabaha yake.
33 Ngurumo zake hutangaza dhoruba inayokuja;
hata mifugo hujulisha kukaribia kwake*au hutangaza kuja kwake.

*36:33 au hutangaza kuja kwake