4
Ukumbusho wa kuvuka Yordani
Taifa lote lilipokwisha kuvuka Mto Yordani, Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, “Chagua watu kumi na wawili miongoni mwa watu, kila kabila mtu mmoja, uwaambie wachukue mawe kumi na mbili katikati ya Mto Yordani, pale makuhani waliposimama, wayachukue na kuyaweka mahali mtakapokaa usiku huu.”
Basi Yoshua akawaita watu kumi na wawili ambao alikuwa amewachagua miongoni mwa Waisraeli, mtu mmoja kutoka kila kabila, naye akawaambia, “Mtangulie mbele ya Sanduku la Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, mwende katikati ya Mto Yordani. Kila mmoja wenu atainua jiwe begani mwake, kulingana na idadi ya makabila ya Israeli, kuwa ishara miongoni mwenu. Siku zijazo, watoto wenu watakapowauliza, ‘Ni nini maana ya mawe haya?’ waambieni kwamba maji ya Mto Yordani yaliyokuwa yakitiririka, yalitindika mbele ya Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu. Sanduku lilipovuka Yordani, maji ya Yordani yalitindika. Mawe haya yatakuwa kumbukumbu kwa watu wa Israeli milele.”
Hivyo Waisraeli wakafanya kama Yoshua alivyowaagiza. Wakachukua mawe kumi na mbili kutoka katikati ya Mto Yordani, kulingana na idadi ya makabila ya Israeli, kama Mwenyezi Mungu alivyomwambia Yoshua, nao wakayabeba hadi kambini mwao, mahali walipoyatua chini. Yoshua akayasimamisha yale mawe kumi na mbili yaliyokuwa katikati ya Mto Yordani, mahali miguu ya makuhani waliobeba Sanduku la Agano iliposimama. Nayo yako huko hadi leo.
10 Makuhani waliobeba lile Sanduku walibakia wakiwa wamesimama katikati ya Mto Yordani hadi kila kitu Mwenyezi Mungu alichomwamuru Yoshua kilipokuwa kimekamilishwa na watu, sawasawa na vile Musa alivyokuwa amemwamuru Yoshua. Watu wakafanya haraka kuvuka, 11 na mara tu watu wote walipokwisha kuvuka, Sanduku la Mwenyezi Mungu na makuhani wakavuka watu wakiwa wanatazama. 12 Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase wakavuka mbele ya Waisraeli, wakiwa wamejiandaa kwa vita, kama Musa alivyowaamuru. 13 Idadi ya wanaume elfu arobaini waliojiandaa kwa vita walivuka mbele za Mwenyezi Mungu hadi nchi tambarare za Yeriko kwa ajili ya vita.
14 Siku ile Mwenyezi Mungu akamtukuza Yoshua mbele ya Israeli yote, nao wakamheshimu siku zote za maisha yake, kama vile walivyomheshimu Musa.
15 Basi Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, 16 “Waamuru hao makuhani wanaolibeba Sanduku la Ushuhuda wapande kutoka ndani ya Mto Yordani.”
17 Kwa hiyo Yoshua akawaamuru hao makuhani akisema, “Pandeni kutoka ndani ya Mto Yordani.”
18 Nao makuhani wakapanda kutoka ndani ya Mto Yordani wakilibeba hilo Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu. Mara tu walipoiweka miguu yao ukingoni mwa mto, maji ya Yordani yakarudi kufurika kama ilivyokuwa kabla.
19 Siku ya kumi ya mwezi wa kwanza watu walipanda kutoka Yordani na kupiga kambi huko Gilgali, kwenye mpaka wa mashariki wa Yeriko. 20 Naye Yoshua akayasimamisha huko Gilgali yale mawe kumi na mbili waliyokuwa wameyachukua katikati ya Mto Yordani. 21 Akawaambia Waisraeli, “Wazao wenu watakapowauliza baba zao siku zijazo wakisema, ‘Mawe haya maana yake ni nini?’ 22 Basi waambieni, ‘Israeli ilivukia mahali pakavu katika Mto Yordani.’ 23 Kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alikausha maji ya Yordani mbele yenu, hadi mlipomaliza kuvuka. Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alifanya haya kwa Mto Yordani sawasawa na kile alichoifanyia Bahari ya Shamu alipoikausha mbele yetu hadi tulipomaliza kuvuka. 24 Alifanya hivi ili mataifa yote ya dunia yapate kujua kuwa mkono wa Mwenyezi Mungu ni wenye nguvu, na ili kila wakati mpate kumcha Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.”