6
Yeriko yaangamizwa
1 Basi malango ya Yeriko yalifungwa kwa uthabiti kwa sababu ya Waisraeli. Hakuna mtu yeyote aliyetoka au kuingia.
2 Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeitia Yeriko mikononi mwako, pamoja na mfalme wake na wapiganaji wake. 3 Zunguka mji mara moja pamoja na watu wote wenye silaha. Fanya hivi kwa siku sita. 4 Uwe na makuhani saba wakibeba mabaragumu ya pembe za kondoo dume mbele ya Sanduku. Siku ya saba, mzunguke mji mara saba, nao makuhani wakipiga baragumu hizo. 5 Utakapowasikia wamepaliza sauti kubwa ya baragumu, watu wote wapige kelele kwa sauti kuu, kisha ukuta wa mji utaanguka na wapiganaji watapanda, kila mtu akielekea mbele yake.”
6 Ndipo Yoshua mwana wa Nuni akaita makuhani na kuwaambia, “Chukueni Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu na makuhani saba wachukue baragumu za pembe za kondoo dume mbele yake.” 7 Naye akawaagiza watu, “Songeni mbele! Mkauzunguke mji, na walinzi wenye silaha watangulie mbele ya Sanduku la Mwenyezi Mungu.”
8 Baada ya Yoshua kuzungumza na watu, wale makuhani saba waliozibeba zile baragumu saba mbele za Mwenyezi Mungu, wakatangulia mbele, wakipiga baragumu zao na Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu likawafuata. 9 Walinzi waliokuwa na silaha wakaenda mbele ya hao makuhani waliopiga hizo baragumu na hao walinzi wa nyuma wakafuata Sanduku. Wakati wote huu baragumu zilikuwa zikipigwa. 10 Bali Yoshua alikuwa amewaagiza watu, “Msipige ukelele wa vita; msipaze sauti zenu, wala kusema neno lolote hadi siku ile nitakayowaambia mpige kelele. Ndipo mtapiga kelele!” 11 Basi akalipeleka Sanduku la Mwenyezi Mungu kuzungushwa huo mji, likizungushwa mara moja. Kisha watu wakarudi kambini kulala.
12 Yoshua akaamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, nao makuhani wakalichukua Sanduku la Mwenyezi Mungu. 13 Wale Makuhani saba waliobeba zile baragumu saba wakatangulia mbele ya Sanduku la Mwenyezi Mungu wakizipiga. Watu wenye silaha wakatangulia mbele yao na walinzi wa nyuma wakalifuata Sanduku la Mwenyezi Mungu, huku baragumu hizo zikiendelea kulia. 14 Siku ya pili wakauzunguka mji mara moja na kurudi kambini. Wakafanya hivi kwa siku sita.
15 Siku ya saba, wakaamka asubuhi na mapema wakauzunguka mji kama walivyokuwa wakifanya, isipokuwa siku ile waliuzunguka mji mara saba. 16 Walipouzunguka mara ya saba, makuhani walipiga baragumu kwa sauti kubwa, naye Yoshua akawaamuru watu akisema, “Pigeni kelele! Kwa maana Mwenyezi Mungu amewapa mji huu! 17 Mji huu pamoja na vyote vilivyomo utatengewa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuangamizwa. Rahabu yule kahaba atasalimishwa, pamoja na wote walio naye nyumbani mwake, kwa sababu aliwaficha wale wapelelezi tuliowatuma. 18 Lakini mjiepushe na vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa, msije mkajiletea maangamizi kwa kuchukua chochote katika hivyo; la sivyo, mtailetea kambi ya Israeli maangamizi na taabu. 19 Fedha yote na dhahabu, vyombo vya shaba na chuma ni vitakatifu kwa Mwenyezi Mungu, lazima viletwe katika hazina yake.”
20 Baragumu zilipopigwa, watu walipiga kelele; kwa ile sauti ya baragumu na watu kupaza sauti, ukuta ukaanguka; hivyo kila mtu akapanda akiendelea mbele na kuuteka mji. 21 Wakauweka mji wakfu kwa Mwenyezi Mungu, na kila chenye uhai ndani yake walikiangamiza kwa upanga: wanaume na wanawake, vijana kwa wazee, ng’ombe, kondoo na punda.
22 Yoshua akawaambia wale watu wawili waliokuwa wameipeleleza nchi, “Nendeni nyumbani mwa yule kahaba; mleteni pamoja na wote walio nyumbani mwake, kulingana na kiapo chenu kwake.” 23 Basi wale vijana waliofanya upelelezi wakaenda kumleta Rahabu, baba yake na mama yake, na ndugu zake na watu wote waliokuwa pamoja naye. Wakaleta jamaa yake yote na kuwaweka mahali nje ya kambi ya Israeli.
24 Kisha wakauchoma mji wote na kila kitu kilichokuwa ndani yake. Lakini fedha, dhahabu, na vyombo vya shaba na vya chuma wakaviweka katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi Mungu. 25 Lakini Yoshua akamhifadhi Rahabu yule kahaba, jamaa yake yote na vyote alivyokuwa navyo, kwa sababu aliwaficha watu waliotumwa na Yoshua kuipeleleza Yeriko, naye anaishi miongoni mwa Waisraeli hata leo.
26 Wakati ule Yoshua akatamka kiapo hiki akasema, “Na alaaniwe mbele za Mwenyezi Mungu mtu atakayeinuka kuujenga tena mji huu wa Yeriko:
“Kwa gharama ya mzaliwa wake wa kwanza wa kiume
ataiweka misingi yake;
kwa gharama ya mtoto wake wa mwisho
atayaweka malango yake.”
27 Hivyo Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja na Yoshua, na sifa zake zikaenea katika nchi yote.