21
Miji kwa Walawi
1 Basi viongozi wa jamaa ya Walawi, wakamwendea kuhani Eleazari, Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa jamaa nyingine za makabila ya Israeli 2 huko Shilo katika Kanaani na kuwaambia, “Mwenyezi Mungu aliamuru kupitia Musa kuwa mtupe miji ya kuishi yenye maeneo ya malisho kwa mifugo yetu.”
3 Hivyo kama vile Mwenyezi Mungu alivyoamuru, Waisraeli wakawapa Walawi miji ifuatayo, na maeneo ya malisho ya kila mji kutoka urithi wao wenyewe.
4 Kura ya kwanza ikaangukia Wakohathi, kufuatana na koo zao. Walawi waliokuwa wazao wa kuhani Haruni walipewa miji kumi na tatu kutoka makabila ya Yuda, Simeoni na Benyamini.
5 Wazao wengine waliobaki wa Wakohathi walipewa miji kumi kutoka koo za makabila ya Efraimu, Dani na nusu ya Manase.
6 Wazao wa Gershoni walipewa miji kumi na tatu kutoka koo za makabila ya Isakari, Asheri, Naftali na nusu ya Manase huko Bashani.
7 Wazao wa Merari, kufuatana na koo zao, walipewa miji kumi na mbili kutoka makabila ya Reubeni, Gadi na Zabuloni.
8 Kwa hiyo Waisraeli wakawapa Walawi miji hii na maeneo ya malisho ya kila mji, kama Mwenyezi Mungu alivyoamuru kupitia kwa Musa.
9 Kutoka makabila ya Yuda na Simeoni waligawa miji ifuatayo kwa majina 10 (miji hii walipewa wazao wa Haruni ambao walitokana na koo za Wakohathi wa Walawi, kwa sababu kura ya kwanza iliwaangukia):
11 Waliwapa Kiriath-Arba (yaani Hebroni), pamoja na eneo lake la malisho lililouzunguka, katika nchi ya vilima ya Yuda. (Arba alikuwa baba wa Anaki.) 12 Lakini mashamba na vijiji vilivyouzunguka mji walikuwa wamempa Kalebu mwana wa Yefune kuwa milki yake.
13 Kwa hiyo wazao wa kuhani Haruni wakapewa Hebroni (mji mkuu wa makimbilio kwa ajili ya yeyote aliyeshtakiwa kwa mauaji), Libna, 14 Yatiri, Eshtemoa, 15 Holoni, Debiri, 16 Aini, Yuta na Beth-Shemeshi, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji tisa kutoka kwa makabila haya mawili.
17 Kutoka kabila la Benyamini wakawapa
Gibeoni, Geba, 18 Anathothi na Almoni, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne.
19 Miji yote waliyopewa makuhani, wazao wa Haruni, ilikuwa kumi na tatu, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji.
20 Koo nyingine za Wakohathi, ambao pia ni Walawi, walipewa miji kutoka kabila la Efraimu:
21 Katika nchi ya vilima ya Efraimu, walipewa:
Shekemu (mji wa makimbilio kwa yeyote anayeshtakiwa kwa mauaji) na Gezeri, 22 Kibsaimu na Beth-Horoni, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne.
23 Pia kutoka kabila la Dani, wakapokea:
Elteke, Gibethoni, 24 Aiyaloni na Gath-Rimoni pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne.
25 Kutoka nusu ya kabila la Manase, wakapokea:
Taanaki na Gath-Rimoni pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji miwili.
26 Miji hii kumi, na maeneo ya malisho ya kila mji, ilipewa koo za Wakohathi zilizobaki.
27 Koo za Walawi za Wagershoni walipewa:
kutoka nusu ya kabila la Manase:
Golani katika Bashani (mji wa makimbilio kwa yeyote aliyeshtakiwa kwa mauaji) na Beeshtera, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji miwili;
28 kutoka kabila la Isakari, walipewa:
Kishioni, Daberathi, 29 Yarmuthi na En-Ganimu, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne;
30 kutoka kabila la Asheri, walipewa:
Mishali, Abdoni, 31 Helkathi na Rehobu, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne.
32 Kutoka kabila la Naftali, walipewa:
Kedeshi katika Galilaya (mji wa makimbilio kwa ajili ya yeyote anayeshtakiwa kwa mauaji), Hamoth-Dori na Kartani, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji mitano.
33 Miji yote ya koo za Wagershoni ilikuwa kumi na tatu, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji.
34 Koo za Wamerari (Walawi waliobaki) walipewa:
kutoka kabila la Zabuloni:
Yokneamu, Karta, 35 Dimna na Nahalali, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne;
36 kutoka kabila la Reubeni, walipewa:
Bezeri, Yahasa, 37 Kedemothi na Mefaathi, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne;
38 kutoka kabila la Gadi, walipewa:
Ramothi katika Gileadi (mji wa makimbilio kwa ajili ya yeyote anayeshtakiwa kwa ajili ya mauaji), Mahanaimu, 39 Heshboni na Yazeri, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji: miji minne.
40 Miji yote waliyopewa koo za Wamerari, waliokuwa mabaki ya Walawi, ilikuwa ni kumi na mbili.
41 Miji yote ya Walawi katika eneo lililomilikiwa na Waisraeli ilikuwa arobaini na nane, pamoja na maeneo ya malisho ya kila mji. 42 Kila mji kati ya miji hii ulikuwa na maeneo ya malisho kuuzunguka; ndivyo ilivyokuwa kwa miji hii yote.
43 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akawapa Israeli nchi yote aliyokuwa ameapa kuwapa baba zao, nao wakaimiliki na kukaa humo. 44 Mwenyezi Mungu akawapa pumziko kila upande, kama vile alivyokuwa amewaapia baba zao, hakuna hata mmoja wa adui zao aliyeweza kusimama mbele yao, Mwenyezi Mungu akawatia adui zao wote mikononi mwao. 45 Hakuna hata mojawapo ya ahadi nzuri ya Mwenyezi Mungu kwa nyumba ya Israeli ambayo haikutimia; kila moja ilitimia.