24
Agano lafanywa upya huko Shekemu
1 Ndipo Yoshua akaita pamoja makabila yote ya Israeli huko Shekemu. Akawaita wazee, viongozi, waamuzi na maafisa wa Israeli, nao wakaja mbele za Mungu.
2 Yoshua akawaambia watu wote, “Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Hapo zamani baba zenu, pamoja na Tera baba yake Ibrahimu na Nahori, waliishi ng’ambo ya Mto*yaani Mto Frati, nao waliiabudu miungu mingine. 3 Lakini nilimwondoa baba yenu Ibrahimu kutoka nchi hiyo ng’ambo ya Mto, nami nikamwongoza katika nchi yote ya Kanaani, nikampa wazao wengi. Nikampa Isaka, 4 naye Isaka nikampa Yakobo na Esau. Esau nikampa nchi ya vilima ya Seiri, lakini Yakobo pamoja na wanawe wakashuka Misri.
5 “ ‘Kisha nikawatuma Musa na Haruni, nami nikawapiga Wamisri kwa kile nilichokitenda huko, tena nikawatoa ninyi huko. 6 Nilipowatoa baba zenu Misri, mlifika kwenye bahari, nao Wamisri wakawafuatia baba zenu kwa magari ya vita na wapanda farasi hadi Bahari ya Shamu. 7 Lakini wakamlilia Mwenyezi Mungu wakitaka msaada, naye akaweka giza kati yenu na Wamisri, akaileta bahari juu yao ikawafunika. Ninyi mliona kwa macho yenu wenyewe kile nilichowatendea Wamisri. Kisha mliishi jangwani kwa muda mrefu.
8 “ ‘Nikawaleta katika nchi ya Waamori ambao waliishi mashariki mwa Yordani. Wakapigana nanyi, lakini nikawatia mikononi mwenu. Nikawaangamiza mbele yenu nanyi mkaimiliki nchi yao. 9 Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, alipojiandaa kupigana dhidi ya Israeli, alimwita Balaamu mwana wa Beori apate kuwalaani. 10 Lakini sikumkubali Balaamu, kwa hiyo aliwabariki tena na tena, nami niliwaokoa toka mkononi mwake.
11 “ ‘Ndipo mlipovuka Yordani mkafika Yeriko. Raia wa Yeriko wakapigana nanyi, kama walivyofanya Waamori, Waperizi, Wakanaani, Wahiti, Wagirgashi, Wahivi na Wayebusi, lakini niliwatia mikononi mwenu. 12 Nikatuma nyigu mbele yenu, ambao pia waliwafukuza mbele yenu, hao wafalme wawili wa Waamori. Siyo upanga au upinde wenu wenyewe vilivyowapatia ushindi. 13 Hivyo nikawapa ninyi nchi ambayo hamkuitaabikia, na miji ambayo hamkuijenga, na mnaishi ndani yake, na kula kutoka mashamba ya mizabibu na mizeituni msiyoipanda.’
14 “Sasa basi mcheni Mwenyezi Mungu na kumtumikia kwa uaminifu wote. Itupeni mbali miungu ambayo baba zenu waliiabudu huko ng’ambo ya Mto na huko Misri, nanyi mtumikieni Mwenyezi Mungu. 15 Lakini msipoona vyema kumtumikia Mwenyezi Mungu, chagueni hivi leo mtakayemtumikia, kama ni miungu ile baba zenu waliitumikia ng’ambo ya Frati, au miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia Mwenyezi Mungu.”
16 Ndipo hao watu wakajibu, “Hili jambo liwe mbali nasi la kumsahau Mwenyezi Mungu na kuitumikia miungu mingine! 17 Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, mwenyewe ndiye alitutoa sisi na baba zetu akatupandisha kutoka Misri, kutoka nchi ile ya utumwa, na kutenda zile ishara kubwa mbele ya macho yetu. Ndiye aliyetulinda katika safari yetu yote na kutokana na mataifa yote ambayo tulipita katikati yao. 18 Mwenyezi Mungu akayafukuza mbele yetu mataifa yote pamoja na Waamori, walioishi katika nchi hii. Hivyo sisi nasi tutamtumikia Mwenyezi Mungu kwa kuwa yeye ndiye Mungu wetu.”
19 Yoshua akawaambia watu, “Hamwezi kumtumikia Mwenyezi Mungu. Yeye ni Mungu Mtakatifu, ni Mungu mwenye wivu. Hatasamehe uasi wenu na dhambi zenu. 20 Ikiwa mkimwacha Mwenyezi Mungu na kuitumikia miungu migeni, atageuka na kuwaleteeni maafa na kuwaangamiza, baada ya kuwa mwema kwenu.”
21 Lakini watu wakamwambia Yoshua, “Sivyo! Sisi tutamtumikia Mwenyezi Mungu.”
22 Ndipo Yoshua akawaambia, “Ninyi mmekuwa mashahidi juu yenu wenyewe kuwa mmechagua kumtumikia Mwenyezi Mungu.”
Nao wakajibu, “Ndiyo, tu mashahidi.”
23 Yoshua akawaambia, “Sasa basi, itupeni mbali hiyo miungu migeni mliyo nayo, nanyi mtoleeni Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, mioyo yenu.”
24 Nao watu wakamwambia Yoshua, “Tutamtumikia Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, na kumtii yeye.”
25 Siku ile Yoshua akafanya agano kwa ajili ya watu na hapo Shekemu ndipo alipowaandikia amri na sheria. 26 Naye Yoshua akayaandika mambo haya katika Kitabu cha Torati ya Mungu. Ndipo akalitwaa jiwe kubwa, akalisimamisha huko chini ya mwaloni, karibu na mahali patakatifu pa Mwenyezi Mungu.
27 Yoshua akawaambia watu wote, “Tazameni! Jiwe hili litakuwa shahidi juu yetu. Limesikia maneno yote Mwenyezi Mungu aliyotuambia. Litakuwa shahidi juu yenu kama mtakuwa waongo kwa Mungu wenu.”
28 Basi Yoshua akawatuma watu kila mmoja aende katika urithi wake mwenyewe.
Kuzikwa katika nchi ya ahadi
29 Baada ya mambo haya, Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Mwenyezi Mungu akafa akiwa na umri wa miaka mia moja na kumi. 30 Nao wakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-Sera†Unajulikana pia kama Timnath-Heresi(taz. Yoshua 19:50; Waamuzi 2:9). katika nchi ya vilima ya Efraimu, kaskazini mwa Mlima Gaashi.
31 Israeli wakamtumikia Mwenyezi Mungu siku zote za maisha ya Yoshua, na za hao wazee walioishi baada ya Yoshua kufa, ambao waliona kila kitu Mwenyezi Mungu alichowatendea Israeli.
32 Nayo ile mifupa ya Yusufu, ambayo Waisraeli waliipandisha kutoka huko Misri, wakaizika huko Shekemu kwenye eneo ambalo Yakobo alilinunua kwa wana wa Hamori baba yake Shekemu, kwa vipande mia vya fedha. Eneo hili likawa ni urithi wa uzao wa Yusufu.
33 Naye Eleazari mwana wa Haruni akafariki, akazikwa huko Gibea, mlima aliokuwa amepewa mtoto wake Finehasi, kwenye nchi ya vilima ya Efraimu.