14
Kutakasa kutoka maambukizo ya magonjwa ya ngozi
Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Haya ndio masharti yanayomhusu mtu mgonjwa wakati wa ibada yake ya utakaso, anapoletwa kwa kuhani: Kuhani ataenda kumchunguza nje ya kambi. Kama mtu huyo atakuwa amepona ugonjwa wake wa ngozi wa kuambukiza, kuhani ataagiza vitu vifuatavyo viletwe kwa ajili ya mtu atakayetakaswa: ndege wawili safi walio hai, mti wa mwerezi, kitani nyekundu, na hisopo. Kisha kuhani ataagiza kwamba mmoja wa ndege wale achinjwe kwenye chungu chenye maji safi. Kisha kuhani atamchukua ndege aliye hai na kumtumbukiza pamoja na mti wa mwerezi, kitani nyekundu na hisopo ndani ya damu ya yule ndege aliyechinjiwa kwenye maji safi. Atamnyunyizia yule mwenye ugonjwa wa kuambukiza maji hayo mara saba, na kumtangaza kuwa safi. Kisha atamwachia yule ndege aliye hai aende zake kwenye mashamba.
“Huyo mtu atakayetakaswa ni lazima afue nguo zake, anyoe nywele zake zote, na aoge kwa maji; ndipo atakapotakasika. Baada ya hili anaweza kuingia kambini, lakini ni lazima akae nje ya hema lake kwa siku saba. Siku ya saba ni lazima anyoe nywele zake zote; yaani anyoe nywele za kichwa, ndevu zake, kope zake na nywele nyingine zote. Ni lazima afue nguo zake, na aoge kwa maji, naye atakuwa safi.
10 “Siku ya nane, ni lazima alete kondoo dume wawili na kondoo jike mmoja, wote wa mwaka mmoja na wasio na dosari, pamoja na sehemu tatu za kumi ya efa*Sehemu tatu za kumi ya efa ni sawa na kilo 3. ya unga laini uliochanganywa na mafuta, kwa ajili ya sadaka ya nafaka, na logi mojaKipimo cha ujazo, sawa na lita 0.3. ya mafuta. 11 Kuhani anayemtangaza kuwa safi atamkabidhi mtu huyo atakayetakaswa pamoja na sadaka zake zote mbele za Mwenyezi Mungu katika ingilio la Hema la Kukutania.
12 “Kisha kuhani atamchukua mmoja wa wale kondoo dume na kumtoa kuwa sadaka ya hatia, pamoja na ile logi moja ya mafuta; ataviinua mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa. 13 Atamchinja huyo kondoo katika mahali patakatifu ambapo sadaka ya dhambi na ile ya kuteketezwa huchinjiwa. Kama ilivyo sadaka ya dhambi, sadaka ya hatia ni ya kuhani; ni takatifu sana. 14 Kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya hatia na kuitia kwenye ncha ya sikio la kuume la yule atakayetakaswa, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume. 15 Kisha kuhani atachukua sehemu ya ile logi ya mafuta, ayamimine kwenye kiganja cha mkono wake mwenyewe wa kushoto, 16 na achovye kidole chake cha shahada cha mkono wake wa kuume kwenye mafuta yaliyo kwenye kiganja chake, na kwa kidole hicho anyunyize mafuta hayo mara saba mbele za Mwenyezi Mungu. 17 Kuhani atampaka yule anayetakaswa sehemu ya mafuta yaliyobaki kiganjani kwenye ncha ya sikio lake la kuume, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume, mahali palepale alipompaka damu ya sadaka ya kuondoa hatia. 18 Kuhani atayapaka mafuta yaliyobaki kwenye kiganja chake juu ya kichwa cha yule anayetakaswa, na kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Mwenyezi Mungu.
19 “Kisha kuhani atatoa dhabihu ya sadaka ya dhambi na kufanya upatanisho kwa ajili ya yule atakayetakaswa kutoka unajisi wake. Baada ya hayo, kuhani atachinja sadaka ya kuteketezwa 20 na kuitoa juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya nafaka ili kumfanyia upatanisho, naye atakuwa safi.
21 “Hata hivyo, kama ni maskini na hawezi kupata vitu hivi, lazima achukue mwana-kondoo wa kiume mmoja kuwa sadaka ya hatia ipate kuinuliwa ili kumfanyia upatanisho, pamoja na sehemu ya kumi ya efaSehemu ya kumi ya efa ni sawa na lita 2. ya unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka, logi moja ya mafuta, 22 na hua wawili au makinda wawili wa njiwa, kile atakachoweza kupata, mmoja kwa sadaka ya dhambi, na mwingine kwa sadaka ya kuteketezwa.
23 “Katika siku ya nane, lazima avilete vitu hivyo kwa kuhani, kwa ajili ya kutakaswa kwake kwenye ingilio la Hema la Kukutania mbele za Mwenyezi Mungu. 24 Kuhani atamchukua mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya hatia, pamoja na ile logi ya mafuta ya kuinuliwa mbele za Mwenyezi Mungu kuwa sadaka ya kuinuliwa. 25 Atamchinja huyo mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya hatia. Kisha ataichukua sehemu ya damu yake na kuipaka kwenye ncha ya sikio la kuume la yule anayetakaswa, na aipake pia kwenye kidole gumba cha mkono wa kuume wa huyo mtu, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume. 26 Kuhani atamiminia sehemu ya mafuta kwenye kiganja chake cha mkono wa kushoto, 27 na kwa kidole chake cha shahada cha mkono wa kuume, atamnyunyizia yule anayetakaswa yale mafuta yaliyo kwenye kiganja chake mara saba mbele za Mwenyezi Mungu. 28 Atampaka mafuta yaliyobaki kwenye kiganja chake katika sehemu zote, kama alivyompaka damu ya sadaka ya hatia: yaani kwenye ncha ya sikio la kuume la yule anayetakaswa, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume. 29 Kuhani atayapaka mafuta yaliyobaki katika kiganja chake kwenye kichwa cha yule anayetakaswa, na kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Mwenyezi Mungu. 30 Kisha atatoa dhabihu wale hua ama makinda wa njiwa ambao yule mtu ataweza kuwapata, 31 mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa, pamoja na sadaka ya nafaka. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho mbele za Mwenyezi Mungu kwa ajili ya yule anayetakaswa.”
32 Haya ndio masharti kwa mtu yeyote mwenye ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, na ambaye hana uwezo wa kutoa sadaka za kawaida kwa ajili ya kutakaswa kwake.
Kutakaswa upele
33 Mwenyezi Mungu akawaambia Musa na Haruni, 34 “Mtakapoingia katika nchi ya Kanaani ninayowapa kuwa milki yenu, nami nikaweka ukoma§ugonjwa wowote wa ngozi wa kuambukiza; pia hutumiwa kwa maambukizi kwenye mawe au matofali ya nyumba unaoenea kwenye nyumba katika nchi ile, 35 ni lazima mwenye nyumba hiyo akamwambie kuhani, ‘Nimeona kitu fulani kinachofanana na ukoma kwenye nyumba yangu.’ 36 Kuhani ataagiza vitu vyote vitolewe ndani ya nyumba, kabla hajaenda kuchunguza kama ina ukoma huo, ili kitu chochote ndani ya nyumba kisitangazwe kuwa najisi. Baada ya hili, kuhani ataingia ndani na kuikagua hiyo nyumba. 37 Atachunguza ukoma huo katika kuta za nyumba hiyo, nazo kama zina rangi ya kijani kibichi au wekundu, na kuna mibonyeo ndani ya ukuta, 38 kuhani atatoka na kufunga mlango wa nyumba hiyo kwa siku saba. 39 Siku ya saba, kuhani atarudi kuikagua nyumba. Kama ukoma umeenea juu ya kuta, 40 ataagiza kwamba mawe yote yaliyoambukizwa yaondolewe na kutupwa katika eneo lililo najisi nje ya mji. 41 Kuta zote za ndani ya nyumba hiyo ni lazima zikwanguliwe, na kifusi chake kitupwe mahali najisi nje ya mji. 42 Kisha watachukua mawe mengine na kujenga palipobomolewa kwa udongo mpya wa mfinyanzi, na wapake nyumba hiyo chokaa.
43 “Ikiwa ukoma huo utatokea tena ndani ya ile nyumba baada ya mawe kuondolewa, na nyumba kukwanguliwa na kupakwa chokaa, 44 kuhani ataenda kuikagua, na kama ukoma umeenea ndani ya nyumba, basi ni ukoma unaoharibu; nyumba hiyo ni najisi. 45 Ni lazima ibomolewe: mawe yake, mbao na chokaa yote; vyote vikatupwe nje ya mji mahali palipo najisi.
46 “Yeyote atakayeingia katika nyumba hiyo ikiwa imefungwa, atakuwa najisi hadi jioni. 47 Yeyote atakayelala au kula ndani ya nyumba hiyo ni lazima afue nguo zake.
48 “Lakini ikiwa kuhani atakuja kuikagua na kukuta kuwa ukoma haujaenea tena baada ya nyumba kupakwa chokaa, ataitangaza nyumba ile kuwa safi, kwa sababu ukoma umekwisha. 49 Ili kuitakasa nyumba hiyo, mwenye nyumba ataleta ndege wawili, mti wa mwerezi, kitani nyekundu na hisopo. 50 Atamchinja mmoja wa wale ndege kwenye chungu chenye maji safi. 51 Kisha atachukua mti wa mwerezi, hisopo, kitani nyekundu na ndege aliye hai, na kuvitumbukiza ndani ya damu ya ndege aliyechinjwa pamoja na maji safi, na kuinyunyizia nyumba ile mara saba. 52 Ataitakasa nyumba kwa damu ya yule ndege, maji safi, ndege aliye hai, mti wa mwerezi, hisopo na uzi mwekundu. 53 Kisha atamwachia yule ndege aliye hai huru mashambani nje ya mji. Kwa njia hii atafanya upatanisho kwa ajili ya nyumba ile, nayo itakuwa safi.”
54 Haya ndio masharti kuhusu aina yoyote ya ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza*yaani ukoma; ni neno lililotumika kueleza magonjwa mbalimbali ya ngozi, ambayo si lazima yawe ni ukoma halisi, kidonda chochote, 55 ukoma katika vazi au ndani ya nyumba, 56 kwa uvimbe, upele, au alama nyeupe katika ngozi, 57 kupambanua wakati kitu fulani ni safi au najisi.
Haya ndio masharti kuhusu magonjwa ya ngozi ya kuambukiza na ukoma.

*14:10 Sehemu tatu za kumi ya efa ni sawa na kilo 3.

14:10 Kipimo cha ujazo, sawa na lita 0.3.

14:21 Sehemu ya kumi ya efa ni sawa na lita 2.

§14:34 ugonjwa wowote wa ngozi wa kuambukiza; pia hutumiwa kwa maambukizi kwenye mawe au matofali ya nyumba

*14:54 yaani ukoma; ni neno lililotumika kueleza magonjwa mbalimbali ya ngozi, ambayo si lazima yawe ni ukoma halisi