2
Kuzaliwa kwa Isa
(Mathayo 1:18-25)
Siku zile Kaisari Augusto alitoa amri kwamba watu wote waandikishwe katika ulimwengu wa Rumi. (Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyofanyika wakati Krenio alikuwa mtawala wa Siria.) Kila mtu alienda kuandikishwa katika mji wake alikozaliwa.
Hivyo Yusufu akapanda kutoka mji wa Nasiri ulioko Galilaya kwenda Yudea, hadi Bethlehemu, mji wa Daudi, kwa sababu yeye alikuwa wa ukoo na wa nyumba ya Daudi. Alienda huko kujiandikisha pamoja na Mariamu, aliyekuwa amemposa, na alikuwa mjamzito. Wakiwa Bethlehemu, wakati wa Mariamu wa kujifungua ukawa umetimia, naye akamzaa mwanawe, kifungua mimba. Akamfunika nguo za kitoto na kumlaza katika hori la kulia ng’ombe, kwa sababu hapakuwa na nafasi katika nyumba ya wageni.
Wachungaji na malaika
Katika eneo lile walikuwako wachungaji waliokuwa wakikaa mashambani, wakilinda makundi yao ya kondoo usiku. Ghafula tazama, malaika wa Mwenyezi Mungu akawatokea, nao utukufu wa Mwenyezi Mungu ukawang’aria kotekote, wakaingiwa na hofu. 10 Lakini malaika akawaambia: “Msiogope. Kwa maana tazama, nawaletea habari njema ya furaha itakayokuwa kwa watu wote. 11 Leo katika mji wa Daudi kwa ajili yenu amezaliwa Mwokozi, ndiye Al-Masihi*Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta., Bwana. 12 Hii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amefunikwa nguo za kitoto na kulazwa katika hori la kulia ng’ombe.”
13 Ghafula pakawa na jeshi kubwa la mbinguni pamoja na huyo malaika wakimsifu Mungu wakisema,
14 “Utukufu kwa Mungu juu mbinguni,
na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”
15 Hao malaika walipokwisha kuondoka na kwenda zao mbinguni, wale wachungaji wakasemezana wao kwa wao, “Twendeni Bethlehemu tukaone mambo haya yaliyotukia, ambayo Mwenyezi Mungu ametuambia habari zake.”
16 Hivyo wakaenda haraka Bethlehemu, wakawakuta Mariamu na Yusufu na yule mtoto mchanga akiwa amelala katika hori la kulia ng’ombe. 17 Walipomwona yule mtoto, wakawaeleza yale waliyokuwa wameambiwa kuhusu huyo mtoto. 18 Nao wote waliosikia habari hizi wakastaajabia yale waliyoambiwa na wale wachungaji wa kondoo. 19 Lakini Mariamu akayaweka mambo haya yote moyoni mwake na kuyatafakari. 20 Wale wachungaji wakarudi, huku wakimtukuza Mungu na kumsifu kwa ajili ya mambo yote waliyokuwa wameambiwa na kuyaona.
21 Hata zilipotimia siku nane, uliokuwa wakati wa kumtahiri mtoto, akaitwa Isa, jina alilopewa na malaika kabla hajatungwa mimba.
Isa apelekwa Hekaluni
22 Ulipotimia wakati wa utakaso wake Mariamu kwa mujibu wa Torati ya Musa, basi Yusufu na Mariamu walimpeleka mtoto Yerusalemu, ili kumweka wakfu kwa Mwenyezi Mungu 23 (kama ilivyoandikwa katika Torati ya Mwenyezi Mungu, kwamba, “Kila mtoto wa kiume kifungua mimba atawekwa wakfu kwa Mwenyezi Mungu”), 24 na pia kutoa dhabihu kulingana na yale yaliyonenwa katika Torati ya Mwenyezi Mungu: “Hua wawili au makinda wawili wa njiwa”.
25 Basi huko Yerusalemu kulikuwa mtu mmoja aliyeitwa Simeoni, aliyekuwa mwenye haki na mcha Mungu. Alikuwa akitazamia faraja ya Israeli, na Roho Mtakatifu wa Mungu alikuwa juu yake. 26 Roho wa Mungu alikuwa amemfunulia kuwa hatakufa kabla hajamwona Al-Masihi wa Bwana. 27 Simeoni, akiwa ameongozwa na Roho wa Mungu, alienda Hekaluni. Wazazi walipomleta mtoto Isa ili kumfanyia kama ilivyokuwa desturi ya Torati, 28 ndipo Simeoni akampokea mtoto mikononi mwake na kumsifu Mungu, akisema:
29 “Bwana Mungu Mwenyezi, kama ulivyoahidi,
sasa mruhusu mtumishi wako
aende kwa amani.
30 Kwa maana macho yangu yameuona wokovu wako,
31 ulioweka tayari machoni pa watu wote,
32 nuru kwa ajili ya ufunuo kwa watu wa Mataifa
na kwa ajili ya utukufu kwa watu wako Israeli.”
33 Naye Yusufu na mama yake mtoto wakastaajabu kwa yale yaliyokuwa yamesemwa kumhusu huyo mtoto. 34 Kisha Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, “Mtoto huyu amewekwa kwa makusudi ya kuanguka na kuinuka kwa wengi katika Israeli. Atakuwa ishara ambayo watu watanena dhidi yake, 35 ili mawazo ya mioyo mingi yadhihirike. Nao upanga utauchoma moyo wako.”
36 Tena alikuwako Hekaluni nabii mmoja mwanamke, jina lake Ana binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa mzee sana; naye alikuwa ameolewa na kuishi na mume kwa miaka saba tu, kisha mumewe akafa. 37 Hivyo alikuwa mjane na umri wake ulikuwa miaka themanini na nne. Yeye hakuondoka humo Hekaluni usiku wala mchana, bali alikuwa akimwabudu Mungu, akifunga na kuomba. 38 Wakati huo huo, Ana alikuja akaanza kusifu, akimshukuru Mungu na kusema habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wakitarajia ukombozi wa Yerusalemu.
39 Yusufu na Mariamu walipokuwa wamekamilisha mambo yote yaliyotakiwa na Torati ya Mwenyezi Mungu, walirudi mjini kwao Nasiri huko Galilaya. 40 Naye yule mtoto akakua na kuongezeka nguvu, akijawa na hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.
Kijana Isa Hekaluni
41 Kila mwaka Yusufu na Mariamu mama yake Isa walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kwa ajili ya Sikukuu ya PasakaSherehe iliyowakumbusha Waisraeli jinsi Mwenyezi Mungu alivyowakomboa kutoka utumwani huko Misri.. 42 Isa alipokuwa na umri wa miaka kumi na mbili, walipanda kwenda kwenye Sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi. 43 Baada ya Sikukuu kumalizika, wakati Yusufu na Mariamu mama yake walipokuwa wakirudi nyumbani, Isa alibaki Yerusalemu lakini hawakutambua. 44 Wao wakidhani kuwa yuko miongoni mwa wasafiri, walienda mwendo wa kutwa nzima. Ndipo wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na rafiki zao. 45 Walipomkosa walirudi Yerusalemu ili kumtafuta. 46 Baada ya siku tatu wakamkuta ndani ya Hekalu, akiwa ameketi katikati ya walimu wa Torati, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47 Wote waliomsikia walistaajabishwa na uwezo wake mkubwa wa kuelewa, na majibu aliyoyatoa. 48 Yusufu na Mariamu mama yake walipomwona walishangaa. Mama yake akamuuliza, “Mwanangu, mbona umetufanyia hivi? Tazama, mimi na baba yako tumekuwa tukikutafuta kwa wasiwasi mkubwa kila mahali.”
49 Isa akawaambia, “Kwa nini kunitafuta? Hamkujua kwamba imenipasa kuwa katika nyumba ya BabaJina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. yangu?”
50 Lakini wao hawakuelewa maana ya lile alilowaambia.
51 Ndipo akashuka pamoja nao hadi Nasiri, naye alikuwa mtiifu kwao. Lakini mama yake akayaweka moyoni mwake mambo haya yote. 52 Naye Isa akakua katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.

*2:11 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta.

2:41 Sherehe iliyowakumbusha Waisraeli jinsi Mwenyezi Mungu alivyowakomboa kutoka utumwani huko Misri.

2:49 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu.