10
Isa awatuma sabini na wawili
1 Baada ya hayo, Bwana Isa akawachagua wengine sabini na wawili, akawatuma wawili wawili katika kila mji na kila sehemu aliyokusudia kwenda baadaye. 2 Akawaambia, “Mavuno ni mengi, lakini watendakazi ni wachache. Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili apeleke watendakazi katika shamba lake la mavuno. 3 Nendeni! Tazama ninawatuma kama wana-kondoo katikati ya mbwa-mwitu. 4 Msichukue mkoba, wala mfuko, wala viatu, na msimsalimu mtu yeyote njiani.
5 “Mkiingia katika nyumba yoyote, kwanza semeni, ‘Amani iwe kwenu.’ 6 Kama kuna mtu wa amani humo, basi amani yenu itakuwa juu yake. La sivyo, itawarudia. 7 Kaeni katika nyumba hiyo, mkila na kunywa kile watakachowapa, kwa sababu kila mtendakazi anastahili malipo yake. Msihamehame kutoka nyumba hadi nyumba.
8 “Mkienda katika mji na watu wake wakawakaribisha, kuleni chochote kiwekwacho mbele yenu, 9 waponyeni wagonjwa waliomo na waambieni: ‘Ufalme wa Mungu umewakaribia.’ 10 Lakini mkiingia katika mji, nao hawakuwakaribisha, tokeni mwende katika barabara zake mkaseme: 11 ‘Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu, tunayakung’uta dhidi yenu. Lakini mjue kwamba ufalme wa Mungu umekaribia.’ 12 Ninawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa Sodoma kustahimili katika siku ile kuliko mji ule.
Onyo kwa miji isiyotubu
(Mathayo 11:20-24)
13 “Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani, kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu. 14 Lakini itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi. 15 Nawe Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha! Utashushwa hadi Kuzimu*Kuzimu kwa Kiyunani ni Hades, yaani mahali pa wafu..
16 “Yeye awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi; naye awakataaye ninyi amenikataa mimi. Lakini yeye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.”
17 Wale sabini na wawili wakarudi kwa furaha, na kusema, “Bwana Isa, hata pepo wachafu wanatutii kwa jina lako.”
18 Isa akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kutoka mbinguni kama radi. 19 Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na juu ya nguvu zote za adui; wala hakuna kitu chochote kitakachowadhuru. 20 Basi, msifurahi kwa kuwa pepo wachafu wanawatii, bali furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni.”
Hakuna amjuaye Baba ila Mwana
(Mathayo 11:25-27; 13:16-17)
21 Wakati huo Isa akashangilia katika Roho wa Mungu, akasema, “Nakuhimidi Baba†Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu., Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.
22 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu. Hakuna mtu amjuaye Mwana ni nani ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ni nani ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.”
23 Basi Isa akawageukia wanafunzi wake akanena nao faraghani, akawaambia, “Heri macho yanayoona yale mambo mnayoyaona. 24 Kwa maana nawaambia, manabii wengi na wafalme walitamani kuona yale mnayoyaona lakini hawakuyaona, na walitamani kusikia yale mnayoyasikia lakini hawakuyasikia.”
Mfano wa Msamaria mwema
25 Wakati huo mtaalamu mmoja wa Torati alisimama ili kumjaribu Isa, akamuuliza, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”
26 Isa akamjibu, “Imeandikwaje katika Torati? Kwani unasoma nini humo?”
27 Akajibu, “ ‘Mpende Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote’; tena, ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.’ ”
28 Isa akamwambia, “Umejibu vyema. Fanya hivyo nawe utaishi.”
29 Lakini yule mtaalamu wa Torati, akitaka kujionesha kuwa mwenye haki, akamuuliza Isa, “Jirani yangu ni nani?”
30 Isa akamjibu akasema, “Mtu mmoja alikuwa akiteremka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko, naye akaangukia mikononi mwa wanyang’anyi. Wakampiga, wakaondoka, wakamwacha akiwa karibu kufa. 31 Kuhani mmoja alikuwa akipitia njia ile, alipomwona huyo mtu, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani. 32 Vivyo hivyo, Mlawi mmoja naye alipofika mahali pale, alimwona, akapita upande mwingine, akamwacha hapo barabarani. 33 Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa akisafiri alipomwona, alimhurumia. 34 Akaenda alipokuwa na akasafisha majeraha yake kwa divai na mafuta, kisha akayafunga. Ndipo akampandisha kwenye punda wake, akampeleka hadi kwenye nyumba ya wageni na kumtunza. 35 Kesho yake, yule Msamaria akachukua dinari mbili‡Dinari mbili ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku mbili. akampa yule mwenye nyumba ya wageni na kusema, ‘Mtunze, nami nirudipo nitakulipa gharama yoyote ya ziada uliyotumia kwa ajili yake.’
36 “Ni yupi basi miongoni mwa hawa watatu wewe unadhani ni jirani yake yule mtu aliyeangukia mikononi mwa wanyang’anyi?”
37 Yule mtaalamu wa Torati akajibu, “Ni yule aliyemhurumia.”
Ndipo Isa akamwambia, “Nenda, ukafanye vivyo hivyo.”
Isa awatembelea Martha na Mariamu
38 Ikawa Isa na wanafunzi wake walipokuwa wakienda Yerusalemu, akaingia kwenye kijiji kimoja ambapo mwanamke mmoja aliyeitwa Martha alimkaribisha nyumbani mwake. 39 Martha alikuwa na dada yake aliyeitwa Mariamu, ambaye aliketi chini miguuni mwa Bwana Isa akisikiliza yale alikuwa akisema. 40 Lakini Martha alikuwa akihangaika na maandalizi yote yaliyokuwa yafanyike. Martha akaja kwa Isa na kumuuliza, “Bwana, hujali kwamba dada yangu ameniachia kazi zote mwenyewe? Basi mwambie anisaidie.”
41 Lakini Bwana Isa akamjibu, “Martha, Martha, mbona unasumbuka na kuhangaika na mengi? 42 Lakini kunahitajika kitu kimoja tu. Mariamu amechagua kile kilicho bora, wala hakuna mtu atakayemwondolea.”