19
Zakayo mtoza ushuru
1 Isa akaingia Yeriko, naye alikuwa anapita katikati ya huo mji. 2 Tazama, palikuwa na mtu mmoja mkuu wa watoza ushuru naye alikuwa tajiri, jina lake Zakayo. 3 Yeye alikuwa akijitahidi kumwona Isa ni mtu wa namna gani. Lakini kutokana na umati mkubwa wa watu hakuweza, kwa sababu alikuwa mfupi wa kimo. 4 Kwa hiyo akatangulia mbio mbele ya umati wa watu akapanda juu ya mkuyu ili amwone Isa, kwa sababu angeipitia njia ile.
5 Isa alipofika pale chini ya huo mkuyu, akatazama juu, akamwambia, “Zakayo, shuka upesi, kwa maana leo nitakuwa mgeni nyumbani mwako!” 6 Hivyo Zakayo akashuka upesi, akamkaribisha Isa nyumbani mwake kwa furaha kubwa.
7 Watu wote walipoona hivyo, wakaanza kunung’unika wakisema, “Ameenda kuwa mgeni wa mtu mwenye dhambi.”
8 Lakini Zakayo akasimama na kumwambia Bwana Isa, “Tazama, Bwana! Sasa hivi nusu ya mali yangu ninawapa maskini, nami kama nimemdhulumu mtu yeyote kitu chochote, nitamrudishia mara nne ya hicho kiwango.”
9 Ndipo Isa akamwambia, “Leo, wokovu umeingia nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. 10 Kwa maana Mwana wa Adamu amekuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.”
Mfano wa fedha
(Mathayo 25:14-30)
11 Walipokuwa wanasikiliza haya, Isa akaendelea kuwaambia mfano, kwa sababu alikuwa anakaribia Yerusalemu na watu walikuwa wakidhani ya kuwa ufalme wa Mungu ulikuwa unakuja saa hiyo. 12 Hivyo akawaambia: “Mtu mmoja mwenye cheo kikubwa alisafiri kwenda nchi ya mbali ili akapokee madaraka ya kuwa mfalme, kisha arudi. 13 Hivyo akawaita kumi miongoni mwa watumishi wake, na akawapa kila mmoja fungu la fedha. Akawaambia, ‘Fanyeni biashara na fedha hizi hadi nitakaporudi.’
14 “Lakini raia wa nchi yake walimchukia wakapeleka ujumbe na kusema, ‘Hatutaki huyu mtu awe mfalme wetu.’
15 “Hata hivyo alirudi akiwa amekwisha kupokea mamlaka ya ufalme, akawaita wale watumishi wake aliokuwa amewaachia fedha, ili afahamu ni faida kiasi gani kila mmoja wao aliyopata kwa kufanya biashara.
16 “Wa kwanza akaja na kusema, ‘Bwana, kutokana na fedha uliyoniachia, nimepata faida mara kumi zaidi.’
17 “Yule bwana akamjibu, ‘Umefanya vizuri mtumishi mwema! Kwa sababu umekuwa mwaminifu katika wajibu mdogo sana, nakupa mamlaka juu ya miji kumi.’
18 “Wa pili naye akaja. Akasema, ‘Bwana, fedha yako imeleta faida mara tano zaidi.’
19 “Bwana wake akajibu, ‘Nakupa mamlaka juu ya miji mitano.’
20 “Kisha akaja yule mtumishi mwingine, akasema, ‘Bwana, hii hapa fedha yako. Niliitunza vizuri kwenye kitambaa. 21 Nilikuogopa, kwa sababu wewe ni mtu mgumu. Unachukua ambapo hukuweka, na kuvuna ambapo hukupanda.’
22 “Bwana wake akamjibu, ‘Nitakuhukumu kwa maneno yako mwenyewe, wewe mtumishi mwovu! Kama ulifahamu kwamba mimi ni mtu mgumu, ninayechukua nisichoweka, na kuvuna nisichopanda, 23 kwa nini basi hukuweka fedha zangu kwa watoa riba, ili nitakaporudi nichukue iliyo yangu na riba yake?’
24 “Ndipo akawaambia wale waliokuwa wamesimama karibu, ‘Mnyang’anyeni fungu lake la fedha, mkampe yule mwenye kumi.’
25 “Wakamwambia, ‘Bwana, mbona; tayari anayo mafungu kumi!’
26 “Akawajibu, ‘Nawaambia kwamba kila aliye na kitu, ataongezewa. Lakini yule asiye na kitu, hata alicho nacho atanyang’anywa. 27 Lakini wale adui zangu ambao hawakutaka mimi niwe mfalme juu yao. Waleteni hapa mkawaue mbele yangu.’ ”
Isa aingia Yerusalemu kwa shangwe
(Mathayo 21:1-11; Marko 11:1-11; Yohana 12:12-19)
28 Baada ya Isa kusema haya, alitangulia kupanda kwenda Yerusalemu. 29 Naye alipokaribia Bethfage na Bethania kwenye mlima ulioitwa Mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia, 30 “Nendeni katika kijiji kilichoko mbele yenu. Na mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtampata mwana-punda amefungwa hapo, ambaye hajapandwa na mtu bado. Mfungueni, mkamlete hapa. 31 Kama mtu akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji.’ ”
32 Wale waliotumwa wakaenda, wakapata kila kitu kama Isa alivyowaambia. 33 Walipokuwa wanamfungua yule mwana-punda, wenyewe wakawauliza, “Mbona mnamfungua huyo mwana-punda?”
34 Wale wanafunzi wakajibu, “Bwana anamhitaji.”
35 Wakamleta kwa Isa, nao baada ya kutandika mavazi yao juu ya huyo mwana-punda, wakampandisha Isa juu yake. 36 Alipokuwa akienda, watu wakatandaza mavazi yao barabarani.
37 Alipokaribia mahali yanapoanzia miteremko ya Mlima wa Mizeituni, umati wote wa wafuasi wake wakaanza kumsifu Mungu kwa furaha kwa sauti kuu kwa ajili ya matendo yote ya miujiza waliyoyaona. Wakasema:
38 “Amebarikiwa mfalme ajaye kwa Jina la Mwenyezi Mungu!”
“Amani mbinguni na utukufu huko juu sana.”
39 Baadhi ya Mafarisayo*Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. waliokuwamo miongoni mwa umati ule wa watu wakamwambia, “Mwalimu, waamuru wanafunzi wako wanyamaze.”
40 Isa akawajibu, “Nawaambia ninyi, kama hawa watanyamaza, mawe yatapaza sauti.”
Isa aulilia mji wa Yerusalemu
41 Alipokaribia Yerusalemu na kuuona mji, aliulilia, 42 akisema, “Laiti ungejua, hata wewe leo, yale yangeleta amani, lakini sasa yamefichika machoni pako. 43 Hakika siku zinakujia, ambazo adui zako watakuzingira, nao watakuzunguka pande zote na kukuzuilia ndani. 44 Watakuponda chini, wewe na watoto walio ndani ya kuta zako. Nao hawataacha hata jiwe moja juu ya jingine, kwa sababu hukutambua wakati wa kujiliwa kwako.”
Huduma ya Isa huko Yerusalemu
(Luka 19:45–20:47)
Isa atakasa Hekalu
(Mathayo 21:12-17; Marko 11:15-19; Yohana 2:13-22)
45 Ndipo akaingia eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza vitu humo. 46 Naye akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyang’anyi.’ ”
47 Kila siku alikuwa akifundisha Hekaluni. Lakini viongozi wa makuhani, walimu wa Torati na viongozi wa watu walikuwa wakitafuta njia ili kumuua. 48 Lakini hawakupata nafasi kwa sababu watu wote walimfuata wakiyasikiliza maneno yake kwa usikivu mwingi.
*19:39 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli.