9
Isa amponya mtu aliyepooza
(Marko 2:1-12; Luka 5:17-26)
1 Isa akaingia kwenye chombo, akavuka na kufika katika mji wa kwao. 2 Wakati huo huo wakamletea mtu aliyepooza, akiwa amelazwa kwenye mkeka. Isa alipoiona imani yao, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Mwanangu, jipe moyo mkuu. Dhambi zako zimesamehewa.”
3 Kwa ajili ya jambo hili, baadhi ya walimu wa Torati wakasema mioyoni mwao, “Huyu mtu anakufuru!”
4 Lakini Isa akiyafahamu mawazo yao, akawaambia, “Kwa nini mnawaza maovu mioyoni mwenu? 5 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi: kusema, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Inuka, uende’? 6 Lakini nataka mpate kujua kwamba Mwana wa Adamu ana mamlaka duniani kusamehe dhambi.” Ndipo akamwambia yule aliyepooza, “Inuka, chukua mkeka wako, uende nyumbani mwako.” 7 Yule mtu akasimama, akaenda nyumbani mwake. 8 Umati wa watu walipoyaona haya, wakajawa na hofu ya Mungu, wakamtukuza Mungu aliyekuwa amewakabidhi wanadamu mamlaka kama haya.
Isa amwita Mathayo
(Marko 2:13-17; Luka 5:27-32)
9 Isa alipokuwa akienda kutoka huko, alimwona mtu mmoja jina lake Mathayo akiwa ameketi forodhani mahali pa kutoza ushuru. Isa akamwambia, “Nifuate.” Mathayo akasimama, akamfuata.
10 Isa alipokuwa ameketi akila chakula ndani ya nyumba ya Mathayo, watoza ushuru wengi na wenye dhambi wakaja, wakaketi kula pamoja naye na wanafunzi wake. 11 Mafarisayo*Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. walipoona mambo haya, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini Mwalimu wenu anakula na watoza ushuru na wenye dhambi?”
12 Lakini Isa aliposikia hayo, akawaambia, “Watu wenye afya hawahitaji tabibu, lakini wale walio wagonjwa ndio wanaohitaji tabibu. 13 Nendeni mkajifunze maana ya maneno haya: ‘Nataka rehema, wala si dhabihu.’ Kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.”
Isa aulizwa kuhusu kufunga
(Marko 2:18-22; Luka 5:33-39)
14 Wanafunzi wa Yahya wakaja na kumuuliza Isa, “Imekuwaje kwamba sisi na Mafarisayo tunafunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?”
15 Isa akawajibu, “Wageni wa bwana arusi wanawezaje kuomboleza wakati angali pamoja nao? Wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao. Hapo ndipo watakapofunga.
16 “Hakuna mtu anayeshonea kiraka kipya kwenye nguo iliyochakaa, kwa maana kile kiraka kitachanika kutoka kwenye hiyo nguo, nayo hiyo nguo itachanika zaidi. 17 Wala watu hawaweki divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Wakifanya hivyo, viriba vitapasuka nayo divai itamwagika, navyo viriba vitaharibika. Lakini divai mpya huwekwa kwenye viriba vipya, na hivyo divai na viriba huwa salama.”
Isa amponya mwanamke na kumfufua msichana
(Marko 5:21-43; Luka 8:40-56)
18 Isa alipokuwa akiwaambia mambo haya, kiongozi wa sinagogi†Nyumba ya ibada na mafunzo. akaingia, akapiga magoti mbele yake, akamwambia, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini njoo uweke mkono wako juu yake, naye ataishi.” 19 Isa akaondoka akafuatana naye, nao wanafunzi wake pia wakaandamana naye.
20 Wakati huo huo, mwanamke mmoja, aliyekuwa na ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na mbili, akaja nyuma ya Isa, akagusa upindo wa vazi lake, 21 kwa maana alisema moyoni mwake, “Nikigusa tu vazi lake, nitaponywa.”
22 Isa akageuka, naye alipomwona akamwambia, “Binti, jipe moyo, imani yako imekuponya.” Naye yule mwanamke akapona kuanzia saa hiyo.
23 Isa alipofika nyumbani mwa yule kiongozi wa sinagogi na kuwaona waombolezaji wakipiga filimbi za maombolezo na watu wengi wakipiga kelele, 24 akawaambia, “Ondokeni! Kwa maana binti huyu hakufa, bali amelala.” Wakamcheka kwa dhihaka. 25 Lakini watu walipokwisha kutolewa nje, akaingia mle ndani na kumshika yule binti mkono, naye akaamka. 26 Habari hizi zikaenea katika maeneo yale yote.
Isa awaponya Vipofu
27 Isa alipokuwa akiondoka mahali pale, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti na kusema, “Mwana wa Daudi‡Ina maana kwamba Isa ni mrithi wa kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu (Zaburi 89:3-4)., tuhurumie!”
28 Alipoingia mle nyumbani wale vipofu wakamjia. Naye Isa akawauliza, “Mnaamini kwamba ninaweza kufanya jambo hili?”
Wakamjibu, “Ndiyo, Bwana.”
29 Ndipo Isa akagusa macho yao na kusema, “Iwe kwenu sawasawa na imani yenu.” 30 Macho yao yakafunguka. Isa akawaonya vikali, akisema, “Chungeni mtu yeyote asijue kuhusu jambo hili.” 31 Lakini wao wakaenda na kueneza habari zake katika eneo lile lote.
Isa amponya bubu
32 Walipokuwa wanatoka, mtu mmoja aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu na ambaye hakuweza kuongea aliletwa kwa Isa. 33 Yule pepo mchafu alipotolewa, yule mtu aliyekuwa bubu akaongea, na umati wa watu wakastaajabu na kusema, “Jambo kama hili kamwe halijapata kuonekana katika Israeli.”
34 Lakini Mafarisayo wakasema, “Huyo anatoa pepo wachafu kwa uwezo wa mkuu wa pepo wachafu.”
Watendakazi ni wachache
35 Isa akazunguka katika miji yote na vijiji vyote, akifundisha katika masinagogi§Nyumba za ibada na mafunzo. yao, akihubiri Habari Njema za ufalme, na akiponya kila ugonjwa na kila aina ya maradhi. 36 Alipoona umati wa watu, aliwahurumia kwa sababu walikuwa wanasumbuka bila msaada, kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. 37 Ndipo akawaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache. 38 Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili atume watendakazi katika shamba lake la mavuno.”
*9:11 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli.
†9:18 Nyumba ya ibada na mafunzo.
‡9:27 Ina maana kwamba Isa ni mrithi wa kiti cha enzi cha Mwenyezi Mungu (Zaburi 89:3-4).
§9:35 Nyumba za ibada na mafunzo.