11
Isa na Yahya
(Luka 7:18-35)
Baada ya Isa kumaliza kutoa maagizo kwa wanafunzi wake kumi na wawili, aliondoka hapo akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji ya Galilaya.
Yahya aliposikia akiwa gerezani mambo ambayo Al-Masihi*Al-Masihi maana yake Masihi, yaani Aliyetiwa mafuta. alikuwa akiyafanya, aliwatuma wanafunzi wake ili wakamuulize, “Wewe ndiwe yule aliyekuwa aje, au tumngojee mwingine?”
Isa akajibu, “Rudini mkamwambie Yahya yale mnayosikia na kuyaona: Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa Habari Njema. Amebarikiwa mtu yule asiyechukizwa na mimi.”
Wale wanafunzi wa Yahya walipokuwa wanaondoka, Isa akaanza kusema na umati wa watu kuhusu Yahya. Akawauliza, “Mlipoenda kule nyikani, mlienda kuona nini? Je, ni unyasi ukipeperushwa na upepo? Kama sivyo, mlienda kuona nini basi? Mtu aliyevaa mavazi ya kifahari? La hasha! Watu wanaovaa mavazi ya kifahari wako katika majumba ya wafalme. Basi mlienda kuona nini? Mlienda kumwona nabii? Naam, nawaambia, yeye ni zaidi ya nabii. 10 Huyu ndiye ambaye habari zake zimeandikwa:
“ ‘Tazama nitamtuma mjumbe wangu mbele yako,
atakayetengeneza njia mbele yako.’
11 Amin, nawaambia, miongoni mwa wale waliozaliwa na wanawake, hajatokea mtu aliye mkuu kuliko Yahya. Lakini aliye mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko Yahya. 12 Tangu siku za Yahya hadi sasa, ufalme wa mbinguni hunyakuliwa kwa nguvu, nao wenye nguvu wanauteka. 13 Kwa maana manabii wote na Torati walitabiri hadi wakati wa Yahya. 14 Ikiwa mko tayari kukubali hilo, yeye ndiye yule Ilya ambaye manabii walikuwa wamesema angekuja. 15 Yeye aliye na masikio, na asikie.
16 “Lakini kizazi hiki nikifananishe na nini? Kinafanana na watoto waliokaa sokoni wakiwaita wenzao na kuwaambia,
17 “ ‘Tuliwapigia filimbi,
lakini hamkucheza;
tuliwaimbia nyimbo za maombolezo,
lakini hamkuomboleza.’
18 Kwa maana Yahya alikuja, alikuwa hali wala hanywi, nao wanasema, ‘Yeye ana pepo mchafu.’ 19 Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nao wanasema, ‘Tazameni huyu mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’ Lakini hekima huthibitishwa kuwa kweli kwa matendo yake.”
Onyo kwa miji isiyotubu
(Luka 10:13-15)
20 Ndipo Isa akaanza kuishutumu miji ambayo alifanya miujiza yake mingi, kwa maana watu wake hawakutubu. 21 “Ole wako, Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa maana kama miujiza iliyofanyika kwenu, ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu. 22 Lakini nawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi. 23 Nawe Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha! Utashushwa hadi KuzimuKuzimu kwa Kiyunani ni Hades, yaani mahali pa wafu.. Miujiza iliyofanyika kwako ingefanyika huko Sodoma, mji huo ungekuwepo hadi leo. 24 Lakini nakuambia kwamba, itakuwa rahisi zaidi kwa Sodoma kustahimili katika siku ya hukumu kuliko wewe.”
Hakuna amjuaye Baba ila Mwana
(Luka 10:21-22)
25 Wakati huo Isa alisema, “Nakuhimidi BabaJina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu., Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. 26 Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.
27 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu: Hakuna mtu amjuaye Mwana ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.
Isa awaita waliolemewa na mizigo
28 “Njooni kwangu, ninyi nyote mnaotaabika na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jifungeni nira yangu, mjifunze kutoka kwangu, kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtapata raha katika nafsi zenu. 30 Kwa maana nira yangu ni laini na mzigo wangu ni mwepesi.”

*11:2 Al-Masihi maana yake Masihi, yaani Aliyetiwa mafuta.

11:23 Kuzimu kwa Kiyunani ni Hades, yaani mahali pa wafu.

11:25 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu.