17
Isa abadilika sura
(Marko 9:2-13; Luka 9:28-36)
1 Siku sita baada ya jambo hili, Isa akawachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, akawapeleka juu ya mlima mrefu peke yao. 2 Wakiwa huko, Isa alibadilika sura mbele yao. Uso wake ukang’aa kama jua na nguo zake zikawa nyeupe kama nuru. 3 Ghafula wakawatokea mbele yao Musa na Ilya, wakizungumza na Isa.
4 Ndipo Petro akamwambia Isa, “Bwana, ni vyema sisi tukae hapa. Ukitaka, nitafanya vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Musa na kingine cha Ilya.”
5 Petro alipokuwa angali ananena, ghafula wingu lililong’aa likawafunika, na sauti ikatoka kwenye hilo wingu ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa naye sana. Msikieni yeye.”
6 Wanafunzi waliposikia haya, wakaanguka kifudifudi, wakajawa na hofu. 7 Lakini Isa akaja na kuwagusa, akawaambia, “Inukeni na wala msiogope.” 8 Walipoinua macho yao, hawakumwona mtu mwingine yeyote isipokuwa Isa.
9 Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Isa akawaagiza, “Msimwambie mtu yeyote mambo mliyoyaona hapa, hadi Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka kwa wafu.”
10 Wale wanafunzi wakamuuliza, “Kwa nini basi walimu wa Torati husema kwamba ni lazima Ilya aje kwanza?”
11 Isa akawajibu, “Ni kweli, Ilya lazima aje kwanza, naye atatengeneza mambo yote. 12 Lakini nawaambia, Ilya amekwisha kuja, nao hawakumtambua, bali walimtendea kila kitu walichotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu pia atateswa mikononi mwao.” 13 Ndipo wale wanafunzi wakaelewa kuwa alikuwa anazungumza nao habari za Yahya.
Isa amponya kijana mwenye pepo mchafu
(Marko 9:14-29; Luka 9:37-45)
14 Walipofika penye umati wa watu, mtu mmoja akamjia Isa na kupiga magoti mbele yake, akasema, 15 “Bwana*Wale ambao hawakumfahamu Isa kuwa Masihi walimwita “Bwana” kwa heshima ya kawaida., mhurumie mwanangu. Yeye ana kifafa na anateseka sana. Mara kwa mara huanguka kwenye moto au kwenye maji. 16 Nilimleta kwa wanafunzi wako, lakini hawakuweza kumponya.”
17 Isa akajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka! Nitakaa nanyi hadi lini? Nitawavumilia hadi lini? Mleteni mvulana hapa kwangu.” 18 Isa akamkemea yule pepo mchafu, akamtoka yule kijana, naye akapona tangu saa hiyo.
19 Kisha wanafunzi wakamwendea Isa wakiwa peke yao, wakamuuliza, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?”
20 Akawajibu, “Kwa sababu ya imani yenu ndogo. Ninawaambia kweli, mkiwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mtauambia mlima huu, ‘Ondoka hapa uende pale,’ nao utaondoka. Wala hakutakuwa na jambo lisilowezekana kwenu. [ 21 Lakini hali kama hii haitoki ila kwa kuomba na kufunga.]†Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.”
Isa atabiri kifo chake mara ya pili
22 Siku moja walipokuwa pamoja huko Galilaya, Isa akawaambia, “Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutiwa mikononi mwa watu. 23 Nao watamuua, lakini siku ya tatu atafufuliwa.” Wanafunzi wakahuzunika sana.
Isa na Petro watoa kodi ya Hekalu
24 Baada ya Isa na wanafunzi wake kufika Kapernaumu, wakusanya kodi ya Hekalu‡Kodi hii ilikuwa drakma mbili kwa kila mwanaume; drakma moja ilikuwa na thamani sawa na mshahara wa kibarua wa siku moja. wakamjia Petro na kumuuliza, “Je, Mwalimu wenu halipi kodi ya Hekalu?”
25 Petro akajibu, “Ndiyo, yeye hulipa.” Petro aliporudi nyumbani, Isa akawa wa kwanza kulizungumzia, akamuuliza, “Unaonaje Simoni? Wafalme wa dunia hupokea ushuru na kodi kutoka kwa nani? Je, ni kutoka kwa watoto wao au kutoka kwa watu wengine?”
26 Petro akamjibu, “Kutoka kwa watu wengine.”
Isa akamwambia, “Kwa hiyo watoto wao wamesamehewa. 27 Lakini ili tusije tukawaudhi, nenda baharini ukatupe ndoana. Mchukue samaki wa kwanza utakayemvua. Fungua kinywa chake nawe utakuta humo fedha, ichukue ukalipe kodi yako na yangu.”