21
Isa aingia Yerusalemu kwa shangwe
(Marko 11:1-11; Luka 19:28-40; Yohana 12:12-19)
Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage katika Mlima wa Mizeituni. Ndipo Isa akawatuma wanafunzi wake wawili, akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu, nanyi mtampata punda amefungwa hapo, na mwana-punda pamoja naye. Wafungueni na mniletee. Mtu yeyote akiwasemesha lolote, mwambieni kwamba Bwana ana haja nao, naye atawaruhusu mwalete mara moja.”
Haya yalitukia ili litimie neno lililonenwa na nabii, aliposema:
“Mwambieni Binti Sayuni,
‘Tazama, mfalme wako anakuja kwako,
ni mpole, naye amepanda punda,
juu ya mwana-punda, mtoto wa punda.’ ”
Wale wanafunzi wakaenda, wakafanya kama Isa alivyokuwa amewaagiza. Wakamleta yule punda na mwana-punda, nao wakatandika mavazi yao juu ya hao punda, naye Isa akaketi juu yake. Umati mkubwa wa watu wakatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakakata matawi kwenye miti, wakayatandaza barabarani. Wale umati wa watu waliomtangulia na wale waliomfuata wakapaza sauti na kusema,
“Hosana*Kiebrania kusema Okoa; basi likawa neno la shangwe., Mwana wa Daudi!”
 
“Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Mwenyezi Mungu!”
 
“Hosana juu mbinguni!”
10 Isa alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakauliza, “Huyu ni nani?”
11 Wale umati wa watu wakajibu, “Huyu ni Isa, yule nabii kutoka Nasiri ya Galilaya.”
Isa atakasa Hekalu
(Marko 11:15-19; Luka 19:45-48; Yohana 2:13-22)
12 Isa akaingia katika eneo la Hekalu na kuwafukuza wote waliokuwa wakinunua na kuuza vitu Hekaluni. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa. 13 Akawaambia, “Imeandikwa, ‘Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala,’ lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.”
14 Vipofu na vilema wakamwendea kule Hekaluni, naye akawaponya. 15 Lakini viongozi wa makuhani na walimu wa Torati walipoona mambo ya ajabu aliyofanya, na kuwasikia watoto wakishangilia katika eneo la Hekalu, wakisema, “Hosana Mwana wa Daudi,” walikasirika.
16 Wakamuuliza Isa, “Je, unasikia hayo hawa wanayosema?”
Akawajibu, “Naam; kwani hamkusoma,
“ ‘Midomoni mwa watoto wachanga na wanaonyonya
umeamuru sifa’?”
17 Akawaacha, akatoka nje ya mji, akaenda hadi Bethania, akalala huko.
Mtini ulionyauka
(Marko 11:12-14, 20-24)
18 Asubuhi na mapema, Isa alipokuwa akirudi mjini, alikuwa na njaa. 19 Akauona mtini kando ya barabara, naye akaukaribia, lakini hakupata tunda lolote ila majani. Ndipo akauambia, “Wewe usizae matunda tena kamwe!” Papo hapo ule mtini ukanyauka.
20 Wanafunzi wake walipoona jambo hili, wakashangaa, wakamuuliza, “Imekuwaje mtini huu kunyauka ghafula?”
21 Isa akawajibu, “Amin, nawaambia, mkiwa na imani wala msiwe na shaka, si kwamba mtaweza kufanya tu yale yaliyofanyika kwa huu mtini, bali hata mkiuambia huu mlima, ‘Ng’oka, ukatupwe baharini,’ litafanyika. 22 Yoyote mtakayoyaomba mkisali na mkiamini, mtayapokea.”
Swali kuhusu mamlaka ya Isa
(Marko 11:27-33; Luka 20:1-8)
23 Isa alipoingia Hekaluni, viongozi wa makuhani na wazee wa watu wakamjia alipokuwa anafundisha, wakamuuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Na ni nani aliyekupa mamlaka haya?”
24 Isa akawajibu, “Nami nitawauliza swali moja. Mkinijibu, nitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya. 25 Je, ubatizo wa Yahya ulitoka wapi? Ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?”
Wakahojiana wao kwa wao na kusema, “Tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona basi hamkumwamini?’ 26 Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu,’ tunawaogopa hawa watu, maana wote wanamtambua Yahya kuwa ni nabii.”
27 Hivyo basi wakamjibu Isa, “Sisi hatujui.”
Naye akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.
Mfano wa wana wawili
28 “Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili. Akamwendea yule wa kwanza akamwambia, ‘Mwanangu, nenda ukafanye kazi kwenye shamba la mizabibu leo.’
29 “Yule mwanawe akamjibu ‘Mimi sitaenda.’ Baadaye akabadili mawazo yake akaenda.
30 “Kisha yule baba akamwendea yule mwanawe mwingine, akamwambia vilevile. Yeye akajibu, ‘Nitaenda, bwana,’ lakini hakuenda.
31 “Ni yupi kati yao hao wawili aliyetimiza kile alichotaka baba yake?”
Wakamjibu, “Ni yule wa kwanza.”
Isa akawaambia, “Amin, amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanawatangulia kuingia katika ufalme wa Mungu. 32 Kwa maana Yahya alikuja kwenu kuwaonesha njia ya haki, lakini hamkumsadiki, lakini watoza ushuru na makahaba wakamsadiki. Nanyi hata mlipoona hayo, baadaye hamkutubu na kumsadiki.
Mfano wa wapangaji waovu
(Marko 12:1-12; Luka 20:9-19)
33 “Sikilizeni mfano mwingine: Kulikuwa na mtu mmoja mwenye shamba ambaye alipanda shamba la mizabibu. Akajenga ukuta kulizunguka, akatengeneza shinikizo la kukamulia zabibu ndani yake, na akajenga mnara wa ulinzi. Kisha akalikodisha hilo shamba la mizabibu kwa wakulima fulani, naye akaondoka, akasafiri hadi nchi nyingine. 34 Wakati wa mavuno ulipokaribia, akawatuma watumishi wake kwa hao wapangaji ili kukusanya matunda yake.
35 “Wale wapangaji wakawakamata wale watumishi, wakampiga mmoja, wakamuua mwingine, na yule wa tatu wakampiga mawe. 36 Kisha akawatuma watumishi wengine kwao, wengi kuliko wale wa kwanza, nao wale wapangaji wakawatendea vilevile. 37 Mwisho wa yote, akamtuma mwanawe kwao, akisema, ‘Watamheshimu mwanangu.’
38 “Lakini wale wapangaji walipomwona mwanawe, wakasemezana wao kwa wao, ‘Huyu ndiye mrithi. Njooni tumuue, ili tuchukue urithi wake.’ 39 Hivyo wakamchukua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamuua.
40 “Basi huyo mwenye shamba la mizabibu atakapokuja, atawafanyia nini hao wakulima?”
41 Wakamjibu, “Kwa hasira kuu, atawaangamiza kabisa hao wadhalimu na kulipangisha shamba lake la mizabibu kwa wakulima wengine ambao watampatia fungu lake la matunda wakati wa mavuno.”
42 Isa akawaambia, “Je, hamjasoma katika Maandiko kwamba:
“ ‘Jiwe walilolikataa waashi
limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Mwenyezi Mungu ndiye alitenda jambo hili,
nalo ni la kushangaza machoni petu’?
43 “Kwa hiyo ninawaambia, ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu na kupewa watu wengine wawezao kuzaa matunda yake. 44 Yeye aangukaye juu ya jiwe hili atavunjika vipande vipande, lakini yule litakayemwangukia atasagwa kabisa.”
45 Viongozi wa makuhani na MafarisayoKundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. waliposikia mifano ya Isa, walitambua kuwa alikuwa akiwasema wao. 46 Wakatafuta njia ya kumkamata, lakini wakaogopa umati wa watu, kwa kuwa watu walimwona Isa kuwa ni nabii.

*21:9 Kiebrania kusema Okoa; basi likawa neno la shangwe.

21:45 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli.