11
Isa aingia Yerusalemu kwa shangwe
(Mathayo 21:1-11; Luka 19:28-40; Yohana 12:12-19)
1 Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage na Bethania katika Mlima wa Mizeituni. Isa akawatuma wawili wa wanafunzi wake, 2 akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Na hapo mtakapoingia kijijini, mtampata mwana-punda amefungwa hapo, ambaye hajapandwa na mtu bado. Mfungueni, mkamlete hapa. 3 Mtu yeyote akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ mwambieni, ‘Bwana anamhitaji, na atamrudisha hapa baada ya muda mfupi.’ ”
4 Wakaenda, wakampata mwana-punda amefungwa kando ya barabara, karibu na mlango wa nyumba. 5 Walipokuwa wanamfungua, watu waliokuwa wamesimama karibu wakawauliza, “Kwa nini mnamfungua huyo mwana-punda?” 6 Wakawajibu kama vile Isa alivyokuwa amewaagiza, nao wale watu wakawaruhusu. 7 Kisha wakamleta huyo mwana-punda kwa Isa na kutandika mavazi yao juu yake, naye akampanda. 8 Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakatandaza matawi waliyokuwa wamekata mashambani. 9 Kisha wale waliokuwa wametangulia mbele na wale waliokuwa wakifuata nyuma wakapaza sauti, wakisema,
“Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Mwenyezi Mungu!”
10 “Umebarikiwa ufalme unaokuja wa baba yetu Daudi!”
“Hosana kwake yeye aliye juu!”
11 Isa akaingia Yerusalemu na kwenda Hekaluni†Nyumba kuu ya ibada kwa Waisraeli iliyokuwa Yerusalemu.. Akaangalia kila kitu kilichokuwamo, lakini kwa kuwa ilishakuwa jioni, akaenda zake Bethania pamoja na wale kumi na wawili.
Isa aulaani mtini usiozaa
(Mathayo 21:18-19)
12 Kesho yake walipokuwa wakitoka Bethania, Isa alikuwa na njaa. 13 Akauona mtini kwa mbali, naye akaenda ili aone kama ulikuwa na matunda. Alipoufikia, akakuta una majani tu, kwa kuwa hayakuwa majira ya tini. 14 Akauambia ule mti, “Tangu leo mtu yeyote asile kamwe matunda kutoka kwako.” Wanafunzi wake walimsikia akisema hayo.
Isa atakasa Hekalu
(Mathayo 21:12-17; Luka 19:45-48; Yohana 2:13-22)
15 Walipofika Yerusalemu, Isa akaingia katika eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakinunua na kuuza humo. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa, 16 wala hakumruhusu mtu yeyote kuchukua bidhaa kupitia ukumbi wa Hekalu. 17 Naye alipokuwa akiwafundisha, akasema, “Je, haikuandikwa kuwa:
“ ‘Nyumba yangu itaitwa
nyumba ya sala kwa mataifa yote’?
Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyang’anyi.’ ”
18 Viongozi wa makuhani na walimu wa Torati wakapata habari hizi, nao wakaanza kutafuta njia ya kumuua, kwa kuwa walikuwa wakimwogopa, kwa sababu umati wote walishangazwa na mafundisho yake.
19 Ilipofika jioni, Isa na wanafunzi wake wakatoka nje ya mji.
Mtini ulionyauka
(Mathayo 21:20-22)
20 Kesho yake asubuhi walipokuwa wakipita, wakauona ule mtini umenyauka kutoka juu hadi kwenye mizizi yake. 21 Petro akakumbuka na kumwambia Isa, “Mwalimu, tazama! Ule mtini ulioulaani umenyauka!”
22 Isa akawajibu, “Mwaminini Mungu. 23 Amin, nawaambia, mtu yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ng’oka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, atatimiziwa. 24 Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote mtakayoyaomba mkisali, aminini kwamba mmeyapokea, nayo yatakuwa yenu. 25 Nanyi kila msimamapo kusali, sameheni mkiwa na neno na mtu, ili naye Baba‡Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu. [ 26 Lakini kama ninyi msiposamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]§Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.”
Swali kuhusu mamlaka ya Isa
(Mathayo 21:23-27; Luka 20:1-8)
27 Wakafika tena Yerusalemu, na Isa alipokuwa akitembea Hekaluni, viongozi wa makuhani, walimu wa Torati pamoja na wazee wa watu wakamjia. 28 Wakamuuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Na ni nani aliyekupa mamlaka ya kufanya hayo?”
29 Isa akawajibu, “Nitawauliza swali moja. Nijibuni, nami nitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya. 30 Je, ubatizo wa Yahya ulitoka mbinguni au kwa wanadamu? Niambieni!”
31 Wakahojiana wao kwa wao na kusema, “Tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona hamkumwamini?’ 32 Lakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu’ ” (waliwaogopa watu, kwa sababu kila mtu aliamini kwamba Yahya alikuwa nabii wa kweli); 33 kwa hiyo wakamjibu Isa, “Hatujui.”
Naye Isa akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.”
*11:9 Kiebrania kusema Okoa; basi likawa neno la shangwe.
†11:11 Nyumba kuu ya ibada kwa Waisraeli iliyokuwa Yerusalemu.
‡11:25 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi.
§11:26 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.