15
Pilato amhoji Isa
(Mathayo 27:1-2, 11-14; Luka 23:3-25; Yohana 18:33–19:16)
Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani, pamoja na wazee, walimu wa Torati na Baraza la Wayahudi*Baraza la Wayahudi ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi; liliundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu. lote, wakafikia uamuzi. Wakamfunga Isa, wakamchukua na kumkabidhi kwa Pilato.
Pilato akamuuliza, “Je, wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi?”
Isa akajibu, “Wewe umesema.”
Viongozi wa makuhani wakamshtaki kwa mambo mengi. Pilato akamuuliza tena, “Je, huna la kujibu? Tazama ni mashtaka mangapi wanayaleta juu yako.”
Lakini Isa hakujibu lolote, hivyo Pilato akashangaa.
Pilato amtoa Isa asulubiwe
(Mathayo 27:15-26; Luka 23:13-25; Yohana 18:39–19:16)
Ilikuwa desturi wakati wa Sikukuu ya Pasaka kumfungulia mfungwa yeyote ambaye watu wangemtaka. Wakati huo, mtu aliyeitwa Baraba alikuwa amefungwa gerezani pamoja na waasi wengine waliokuwa wametekeleza uuaji wakati wa maasi. Umati ule wa watu wakamjia Pilato na kumwomba awafanyie kama ilivyokuwa desturi yake.
Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie huyu mfalme wa Wayahudi?” 10 Kwa maana yeye alitambua kuwa viongozi wa makuhani walikuwa wamemtia Isa mkononi mwake kwa ajili ya wivu. 11 Lakini viongozi wa makuhani wakachochea umati ule wa watu wamwombe awafungulie Baraba badala yake.
12 Pilato akawauliza tena, “Basi mnataka nifanye nini na huyu mtu mnayemwita mfalme wa Wayahudi?”
13 Wakapiga kelele, wakisema, “Msulubishe!”
14 Pilato akawauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?”
Lakini wao wakapiga kelele zaidi, wakisema, “Msulubishe!”
15 Pilato, akitaka kuridhisha umati ule wa watu, akawafungulia Baraba. Naye baada ya kuamuru Isa apigwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe.
Askari wamdhihaki Isa
(Mathayo 27:27-31; Yohana 19:2-3)
16 Askari wakampeleka Isa hadi kwenye ukumbi wa ndani wa jumba la kifalme, ndio PraitorioPraitorio ilikuwa makao makuu ya mtawala wa jimbo. Hapa ni jumba la kifalme ambapo Pontio Pilato aliishi huko Yerusalemu, palipokuwa na kiti cha hukumu., wakakusanya kikosi kizima cha askari. 17 Wakamvalisha Isa joho la zambarau, wakasokota taji la miiba, wakamvika kichwani. 18 Wakaanza kumsalimu kwa dhihaka, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” 19 Wakampiga kwa fimbo ya mwanzi tena na tena kichwani na kumtemea mate. Wakapiga magoti mbele yake, wakamsujudia kwa kumdhihaki. 20 Walipokwisha kumdhihaki, wakamvua lile joho la zambarau, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakamtoa nje ili wakamsulubishe.
Isa asulubishwa
(Mathayo 27:32-44; Luka 23:26-43; Yohana 19:17-27)
21 Mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, baba yao Iskanda na Rufo, alikuwa anaingia mjini kutoka mashambani, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba. 22 Kisha wakampeleka Isa hadi mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa). 23 Nao wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini hakuinywa. 24 Basi wakamsulubisha, nazo nguo zake wakagawana miongoni mwao kwa kuzipigia kura ili kuamua ni gani kila mtu ataichukua.
25 Ilikuwa saa tatu asubuhi walipomsulubisha. 26 Tangazo likaandikwa la mashtaka dhidi yake lenye maneno haya:
Mfalme wa Wayahudi.
27 Pamoja naye walisulubiwa wanyang’anyi wawili, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto. [ 28 Nalo andiko likatimizwa, lisemalo, “Alihesabiwa pamoja na watenda dhambi.”]Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya. 29 Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Aha! Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu, 30 basi shuka kutoka msalabani na ujiokoe mwenyewe!”
31 Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani pamoja na walimu wa Torati wakamdhihaki miongoni mwao wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe! 32 Basi huyu Al-Masihi§Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta., huyu mfalme wa Israeli, ashuke sasa msalabani, ili tupate kuona na kuamini.” Wale waliosulubiwa pamoja naye pia wakamtukana.
Kifo cha Isa
(Mathayo 27:45-56; Luka 23:44-49; Yohana 19:28-30)
33 Ilipofika saa sita, giza liliifunika nchi yote hadi saa tisa. 34 Hapo saa tisa, Isa akapaza sauti, akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”)
35 Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama karibu waliposikia hayo, wakasema, “Msikieni, anamwita Ilya.”
36 Mtu mmoja akaenda mbio, akachovya sifongo kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Isa ili anywe, akisema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Ilya atakuja kumshusha kutoka hapo msalabani.”
37 Kisha Isa akatoa sauti kuu, akakata roho.
38 Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili kuanzia juu hadi chini. 39 Basi yule jemadari aliyekuwa amesimama hapo mbele ya msalaba wa Isa aliposikia ile sauti yake na kuona jinsi alivyokata roho, akasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu*Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili.!”
40 Palikuwa na wanawake waliokuwa wakiangalia kwa mbali. Miongoni mwao walikuwa Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo mdogo na Yose, pia na Salome. 41 Hawa walifuatana na Isa na kushughulikia mahitaji yake alipokuwa Galilaya. Pia walikuwako wanawake wengine wengi waliokuwa wamekuja pamoja naye hadi Yerusalemu.
Maziko ya Isa
(Mathayo 27:57-61; Luka 23:50-56; Yohana 19:38-42)
42 Ilipofika jioni, kwa kuwa ilikuwa Siku ya Maandalizi (yaani siku moja kabla ya Sabato), 43 Yusufu wa Arimathaya, mtu aliyeheshimiwa katika Baraza, na alikuwa anautarajia ufalme wa Mungu, akamwendea Pilato kwa ujasiri na kumwomba mwili wa Isa. 44 Pilato alikuwa akijiuliza kama Isa alikuwa amekwisha kufa. Hivyo akamwita yule jemadari, akamuuliza iwapo Isa alikuwa amekwisha kufa. 45 Baada ya kupata habari kutoka kwa yule jemadari kwamba kweli amekwisha kufa, Pilato akampa Yusufu ruhusa ya kuuchukua huo mwili. 46 Hivyo Yusufu akanunua kitambaa cha kitani safi, akaushusha mwili kutoka msalabani, akaufunga katika kile kitambaa cha kitani, na kuuweka ndani ya kaburi lililochongwa kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kwenye ingilio la kaburi. 47 Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yose walipaona mahali pale alipolazwa.

*15:1 Baraza la Wayahudi ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi; liliundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu.

15:16 Praitorio ilikuwa makao makuu ya mtawala wa jimbo. Hapa ni jumba la kifalme ambapo Pontio Pilato aliishi huko Yerusalemu, palipokuwa na kiti cha hukumu.

15:28 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.

§15:32 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta.

*15:39 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili.