Nahumu
1
1 Neno la unabii kuhusu Ninawi. Kitabu cha maono cha Nahumu Mwelkoshi.
Hasira ya Mwenyezi Mungu dhidi ya Ninawi
2 Mwenyezi Mungu ni mwenye wivu na Mungu mlipiza kisasi;
Mwenyezi Mungu hulipiza kisasi na amejaa ghadhabu.
Mwenyezi Mungu hulipiza kisasi juu ya watesi wake,
naye anadumisha ghadhabu yake dhidi ya adui zake.
3 Mwenyezi Mungu si mwepesi wa hasira naye ni mwenye nguvu,
Mwenyezi Mungu hataacha kuadhibu wenye hatia.
Njia yake ipo katika kisulisuli na tufani,
na mawingu ni vumbi la miguu yake.
4 Anakemea bahari na kuikausha,
anafanya mito yote kukauka.
Bashani na Karmeli zinanyauka
na maua ya Lebanoni hukauka.
5 Milima hutikisika mbele yake
na vilima huyeyuka.
Nchi hutetemeka mbele yake,
dunia na wote wanaoishi ndani yake.
6 Ni nani awezaye kuzuia hasira yake yenye uchungu?
Nani awezaye kuvumilia hasira yake kali?
Ghadhabu yake imemiminwa kama moto,
na miamba inapasuka mbele zake.
7 Mwenyezi Mungu ni Mwema,
kimbilio wakati wa taabu.
Huwatunza wale wanaomtegemea,
8 lakini kwa mafuriko makubwa,
ataangamiza Ninawi;
atafuatilia adui zake hadi gizani.
9 Kila njama wanayopanga dhidi ya Mwenyezi Mungu
yeye atalikomesha;
taabu haitatokea mara ya pili.
10 Watasongwa katikati ya miiba
na kulewa kwa mvinyo wao.
Watateketezwa kama mabua makavu.
11 Ee Ninawi, kutoka kwako amejitokeza mmoja,
ambaye anapanga njama
dhidi ya Mwenyezi Mungu
na kushauri uovu.
12 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Ingawa wana muungano nao ni wengi sana,
watakatiliwa mbali na kuangamia.
Ingawa nimekutesa wewe, ee Yuda,
sitakutesa tena.
13 Sasa nitavunja nira zao kutoka shingo yako,
nami nitazivunjilia mbali pingu zako.”
14 Hii ndiyo amri Mwenyezi Mungu aliyoitoa kukuhusu wewe, Ninawi:
“Hutakuwa na wazao
watakaoendeleza jina lako.
Nitaharibu sanamu za kuchonga na sanamu za kusubu
zilizopo katika hekalu la miungu yenu.
Nitaandaa kaburi lako,
kwa maana wewe ni mwovu kabisa.”
15 Tazama, huko juu milimani,
miguu ya huyo mmoja aletaye habari njema,
ambaye anatangaza amani!
Ee Yuda, sherehekea sikukuu zako,
nawe utimize nadhiri zako.
Waovu hawatakuvamia tena;
wataangamizwa kabisa.