10
Tarumbeta za fedha
1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa: 2 “Tengeneza tarumbeta mbili za fedha ya kufua, uzitumie kwa kuita jumuiya pamoja na wakati wa kuvunja makambi ili kuondoka. 3 Tarumbeta zote mbili zikipigwa, jumuiya yote itakusanyika mbele yako katika ingilio la Hema la Kukutania. 4 Kama tarumbeta moja tu ikipigwa, viongozi, yaani wakuu wa koo za Israeli, ndio watakaokusanyika mbele yako. 5 Mlio wa kujulisha hatari ukipigwa, makabila yaliyo na makambi upande wa mashariki yataondoka. 6 Mlio wa pili ukipigwa, walio kwenye makambi ya kusini wataondoka. Mlio huo wa kujulisha hatari utakuwa ishara ya kuondoka. 7 Ili kuwakusanya watu, piga tarumbeta zote, lakini siyo kwa mlio wa kujulisha hatari.
8 “Wana wa Haruni, makuhani, ndio watakaopiga hizo tarumbeta. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa ajili yenu na kwa vizazi vijavyo. 9 Mtakapopigana vita katika nchi yenu wenyewe dhidi ya adui anayewaonea, piga tarumbeta kwa mlio wa kujulisha hatari. Ndipo utakumbukwa na Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kuokolewa kutoka kwa adui zenu. 10 Pia nyakati za furaha yenu, yaani sikukuu zenu zilizoamriwa na sikukuu za Mwezi Mwandamo, mtapiga tarumbeta juu ya sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za amani, nazo zitakuwa ukumbusho kwa ajili yenu mbele za Mungu wenu. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.”
Waisraeli waondoka Sinai
11 Katika siku ya ishirini ya mwezi wa pili wa mwaka wa pili, wingu liliinuka kutoka juu ya Maskani ya Ushuhuda. 12 Ndipo Waisraeli wakaondoka kutoka Jangwa la Sinai wakasafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine hadi wingu lilipotua katika Jangwa la Parani. 13 Waliondoka kwa mara ya kwanza kwa agizo la Mwenyezi Mungu kupitia kwa Musa.
14 Vikosi vya kambi ya Yuda vilitangulia kwanza chini ya beramu yao. Nashoni mwana wa Aminadabu alikuwa kiongozi wao. 15 Nethaneli mwana wa Suari alikuwa kiongozi wa kabila la Isakari, 16 naye Eliabu mwana wa Heloni alikuwa kiongozi wa kabila la Zabuloni. 17 Ndipo Maskani iliposhushwa, nao wana wa Gershoni na wana wa Merari ambao waliibeba wakaondoka.
18 Vikosi vya kambi ya Reubeni vilifuata, chini ya beramu yao. Elisuri mwana wa Shedeuri alikuwa kiongozi wao. 19 Shelumieli mwana wa Surishadai aliongoza kikosi cha kabila la Simeoni, 20 naye Eliasafu mwana wa Deueli aliongoza kikosi cha kabila la Gadi. 21 Kisha Wakohathi wakaondoka, wakichukua vitu vitakatifu. Maskani ilipaswa kusimamishwa kabla wao hawajafika.
22 Vikosi vya kambi ya Efraimu vilifuata, chini ya beramu yao. Elishama mwana wa Amihudi alikuwa kiongozi wao. 23 Gamalieli mwana wa Pedasuri aliongoza kikosi cha kabila la Manase, 24 naye Abidani mwana wa Gideoni alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Benyamini.
25 Mwishowe, kama kikosi cha nyuma cha ulinzi wa vikosi vyote, vikosi vya kambi ya Dani viliondoka chini ya beramu yao. Ahiezeri mwana wa Amishadai alikuwa kiongozi wao. 26 Pagieli mwana wa Okrani aliongoza kikosi cha kabila la Asheri, 27 naye Ahira mwana wa Enani aliongoza kikosi cha kabila la Naftali. 28 Huu ndio ulikuwa utaratibu wa kuondoka wa vikosi vya Waisraeli walipokuwa wanaondoka.
29 Basi Musa akamwambia Hobabu mwana wa Reueli, Mmidiani, mkwewe Musa, “Tunaondoka kwenda mahali ambapo Mwenyezi Mungu amesema ‘Nitawapa ninyi mahali hapo.’ Twende pamoja, nasi tutakutendea mema, kwa maana Mwenyezi Mungu ameahidi mambo mema kwa Israeli.”
30 Akajibu, “Hapana, sitaenda; nitarudi kwenye nchi yangu mwenyewe na watu wangu mwenyewe.”
31 Lakini Musa akasema, “Tafadhali usituache. Wewe unajua mahali yatupasa kupiga kambi jangwani, nawe unaweza kuwa macho yetu. 32 Ikiwa utafuatana nasi, tutashirikiana nawe mema yoyote tutakayopewa na Mwenyezi Mungu.”
33 Hivyo waliondoka kutoka mlima wa Mwenyezi Mungu, nao wakasafiri kwa siku tatu. Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu liliwatangulia kwa zile siku tatu ili kuwatafutia mahali pa kupumzika. 34 Wingu la Mwenyezi Mungu lilikuwa juu yao wakati wa mchana walipoondoka kambini.
35 Wakati wowote Sanduku lilipoondoka, Musa alisema,
“Ee Mwenyezi Mungu, inuka!
Watesi wako na watawanyike;
adui zako na wakimbie mbele zako.”
36 Wakati wowote Sanduku liliposimama, alisema,
“Ee Mwenyezi Mungu, rudi,
kwa maelfu ya Waisraeli wasiohesabika.”