12
Miriamu na Haruni wampinga Musa
Miriamu na Haruni walianza kuzungumza dhidi ya Musa kwa sababu ya mke wake Mkushi, kwa kuwa alikuwa ameoa Mkushi. Waliuliza, “Je, Mwenyezi Mungu amesema kupitia Musa peke yake? Je, hajasema kutupitia sisi pia?” Naye Mwenyezi Mungu akasikia hili.
(Basi Musa alikuwa mtu mnyenyekevu sana, mnyenyekevu kuliko mtu mwingine yeyote katika uso wa dunia.)
Ghafula Mwenyezi Mungu akawaambia Musa, Haruni na Miriamu, “Njooni katika Hema la Kukutania, ninyi nyote watatu.” Kwa hiyo wote watatu wakaenda. Kisha Mwenyezi Mungu akashuka katika nguzo ya wingu, akasimama kwenye ingilio la Hema, akawaita Haruni na Miriamu. Waliposogea mbele, Mwenyezi Mungu akawaambia, “Sikilizeni maneno yangu:
“Akiwepo nabii wa Mwenyezi Mungu miongoni mwenu,
nitajifunua kwake kwa maono,
nitanena naye katika ndoto.
Lakini sivyo kwa mtumishi wangu Musa;
yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote.
Kwake nitanena naye uso kwa uso,
waziwazi wala si kwa mafumbo;
yeye ataona umbo la Mwenyezi Mungu.
Kwa nini basi ninyi hamkuogopa
kuzungumza kinyume cha mtumishi wangu Musa?”
Hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi yao, akawaacha.
10 Hilo wingu lilipoinuka kutoka juu ya Hema, Miriamu akawa tayari ana ukoma, mweupe kama theluji. Haruni akamgeukia, akaona ana ukoma. 11 Kisha Haruni akamwambia Musa, “Tafadhali, bwana wangu, usituhesabie dhambi hii ambayo tumeifanya kwa upumbavu. 12 Usimwache awe kama mtoto mchanga aliyezaliwa akiwa mfu, ambaye nusu ya mwili wake imeharibika hapo atokapo katika tumbo la mama yake.”
13 Hivyo Musa akamlilia Mwenyezi Mungu akisema, “Ee Mungu, nakuomba umponye!”
14 Mwenyezi Mungu akamjibu Musa, “Je, kama baba yake angemtemea usoni, asingeona aibu kwa siku saba? Mfungie nje ya kambi kwa siku saba; baada ya hapo anaweza kurudishwa kambini.” 15 Kwa hiyo Miriamu akafungiwa nje ya kambi kwa siku saba, nao watu hawakuendelea na safari hadi aliporudishwa kambini.
16 Baada ya hayo, watu waliondoka Haserothi, wakapiga kambi katika Jangwa la Parani.