17
Kuchipuka kwa fimbo ya Haruni
1 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 2 “Sema na Waisraeli, na ujipatie fimbo kumi na mbili kutoka kwao, moja kutoka kwa kila mmoja wa viongozi wa makabila ya baba zao. Andika jina la kila mtu kwenye fimbo yake. 3 Kwenye fimbo ya Lawi andika jina la Haruni, kwa maana ni lazima iwepo fimbo moja kwa kila kiongozi kwa ajili ya kila kabila la baba zao. 4 Ziweke hizo fimbo ndani ya Hema la Kukutania mbele ya Sanduku la Ushuhuda, mahali nikutanapo nawe. 5 Fimbo ya mtu nitakayemchagua itachipuka, nami mwenyewe nitayakomesha haya manung’uniko ya mara kwa mara ya Waisraeli dhidi yako.”
6 Hivyo Musa akasema na Waisraeli, nao viongozi wao wakampa fimbo kumi na mbili, fimbo moja kwa ajili ya kila kabila la baba zao, nayo fimbo ya Haruni ikiwa miongoni mwa hizo. 7 Musa akaziweka hizo fimbo mbele za Mwenyezi Mungu ndani ya Hema la Ushuhuda.
8 Siku iliyofuata Musa aliingia kwenye Hema la Ushuhuda akaona ile fimbo ya Haruni ambayo iliwakilisha jamaa ya Lawi haikuwa tu imechipuka, bali pia ilikuwa imetoa machipukizi, kuchanua maua na kuzaa malozi. 9 Ndipo Musa akaleta zile fimbo zote kwa Waisraeli wote kutoka mbele za Mwenyezi Mungu. Wakaziangalia, na kila mtu akaichukua fimbo yake mwenyewe.
10 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Rudisha fimbo ya Haruni mbele ya Sanduku la Ushuhuda, ili ihifadhiwe kama alama kwa waasi. Hili litakomesha manung’uniko yao dhidi yangu, ili wasife.” 11 Musa akafanya kama Mwenyezi Mungu alivyomwamuru.
12 Waisraeli wakamwambia Musa, “Tutakufa! Tumepotea, sote tumepotea! 13 Yeyote akaribiaye Maskani ya Mwenyezi Mungu atakufa. Je, sisi sote tutakufa?”