23
Ujumbe wa kwanza wa Balaamu
1 Balaamu akasema, “Nijengee hapa madhabahu saba, mnitayarishie mafahali saba na kondoo dume saba.” 2 Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema; hao wawili kila mmoja wao akatoa fahali mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.
3 Kisha Balaamu akamwambia Balaki, “Kaa hapa kando ya sadaka yako wakati mimi ninaenda kando. Huenda Mwenyezi Mungu atakuja kukutana nami. Lolote atakalonifunulia, nitakuambia.” Basi akaenda hata mahali peupe palipoinuka.
4 Mungu akakutana naye, kisha Balaamu akasema, “Nimekwisha kutengeneza madhabahu saba, na juu ya kila madhabahu nimetoa sadaka ya fahali mmoja na kondoo dume mmoja.”
5 Mwenyezi Mungu akaweka ujumbe katika kinywa cha Balaamu na kusema, “Rudi kwa Balaki umpe ujumbe huu.”
6 Basi Balaamu akarudi kwa Balaki, akamkuta amesimama kando ya sadaka yake akiwa na wakuu wote wa Moabu. 7 Ndipo Balaamu akasema ujumbe wake:
“Balaki amenileta kutoka Aramu,
mfalme wa Moabu kutoka milima ya mashariki.
Akasema, ‘Njoo, unilaanie Yakobo;
njoo unishutumie Israeli.’
8 Nitawezaje kuwalaani,
hao ambao Mungu hajawalaani?
Nitawezaje kuwashutumu
hao ambao Mwenyezi Mungu hakuwashutumu?
9 Kutoka vilele vya miamba ninawaona,
kutoka mahali palipoinuka ninawatazama.
Ninaliona taifa ambalo wanaishi peke yao,
nao hawahesabiwi kama mojawapo ya mataifa.
10 Ni nani awezaye kuhesabu mavumbi ya Yakobo,
au kuhesabu robo ya Israeli?
Mimi na nife kifo cha mtu mwenye haki,
na mwisho wangu na uwe kama wao!”
11 Balaki akamwambia Balaamu, “Ni nini ulichonitendea? Nimekuleta ulaani adui zangu, lakini wewe badala yake umewabariki!”
12 Balaamu akajibu, “Je, hainipasi kusema kile Mwenyezi Mungu anachoweka katika kinywa changu?”
Ujumbe wa pili wa Balaamu
13 Ndipo Balaki akamwambia, “Twende pamoja mahali pengine ambapo unaweza kuwaona; utawaona baadhi tu wala si wote. Nawe kutoka huko, unilaanie hao.” 14 Basi akampeleka kwenye shamba la Sofimu, juu ya kilele cha Mlima Pisga. Pale akajenga madhabahu saba na kutoa sadaka ya fahali na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.
15 Balaamu akamwambia Balaki, “Kaa hapa kando ya sadaka yako wakati ninapoenda kuonana na Mungu kule.”
16 Mwenyezi Mungu akakutana na Balaamu, akaweka ujumbe katika kinywa chake akasema, “Rudi kwa Balaki umpe ujumbe huu.”
17 Basi Balaamu akarudi kwa Balaki, akamkuta amesimama kando ya sadaka yake, akiwa na wakuu wa Moabu. Balaki akamuuliza, “Je, Mwenyezi Mungu amesema nini?”
18 Ndipo Balaamu akasema ujumbe wake:
“Balaki, inuka na usikilize,
nisikie mimi, wewe mwana wa Sipori.
19 Mungu si mtu, hata aseme uongo,
wala yeye si mwanadamu, hata ajute.
Je, anasema, kisha asitende?
Je, anaahidi, asitimize?
20 Nimepokea agizo kubariki;
amebariki, nami siwezi kubadilisha.
21 “Haijaonekana bahati mbaya katika Yakobo,
wala taabu katika Israeli.
Mwenyezi Mungu, Mungu wao, yu pamoja nao,
nayo sauti kuu ya Mfalme imo kati yao.
22 Mungu aliwatoa kutoka Misri;
wao wana nguvu kama za nyati.
23 Hakuna uchawi dhidi ya Yakobo,
wala hakuna uaguzi dhidi ya Israeli.
Sasa itasemwa kuhusu Yakobo
na Israeli, ‘Tazama yale Mungu aliyotenda!’
24 Taifa lainuka kama simba jike;
linajiinua kama simba
ambaye hatulii hadi amalize kurarua mawindo yake
na kunywa damu ya mawindo yake.”
25 Kisha Balaki akamwambia Balaamu, “Usiwalaani kabisa, wala usiwabariki kabisa!”
26 Balaamu akajibu, “Je, sikukuambia ni lazima nifanye lolote analosema Mwenyezi Mungu?”
Ujumbe wa tatu wa Balaamu
27 Basi Balaki akamwambia Balaamu, “Njoo, nikupeleke mahali pengine. Huenda itampendeza Mungu kukuruhusu unilaanie hao watu kutoka mahali hapo.” 28 Balaki akamchukua Balaamu juu ya Mlima Peori, unaotazamana na nyika.
29 Balaamu akasema, “Nijengee hapa madhabahu saba, uandae mafahali saba na kondoo dume saba kwa ajili yangu.” 30 Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema, kisha akatoa sadaka ya fahali mmoja na kondoo dume mmoja juu ya kila madhabahu.