25
Moabu yashawishi Israeli
Israeli alipokuwa akikaa Shitimu, wanaume wa Israeli walianza kuzini na wanawake wa Moabu, ambao waliwaalika kushiriki katika sadaka kwa miungu yao. Watu wakala na kusujudu mbele ya miungu hiyo. Kwa hiyo Israeli akaungana katika kumwabudu Baali wa Peori. Hasira ya Mwenyezi Mungu ikawaka dhidi yao.
Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Uwachukue viongozi wote wa watu hawa, uwaue hadharani mbele za Mwenyezi Mungu, ili hasira kali ya Mwenyezi Mungu iweze kuondoka kwa Israeli.”
Kwa hiyo Musa akawaambia waamuzi wa Israeli, “Kila mmoja wenu lazima awaue wale wanaume wenu, walioshiriki katika kumwabudu Baali wa Peori.”
Ndipo mwanaume Mwisraeli akamleta mwanamke Mmidiani katika jamaa yake palepale mbele ya Musa na mkutano wote wa Israeli walipokuwa wakilia kwenye lango la Hema la Kukutania. Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa kuhani Haruni, alipoona jambo hili, akaondoka kwenye kusanyiko, akachukua mkuki mkononi mwake, akamfuata yule Mwisraeli ndani ya hema. Akawachoma mkuki wote wawili kwa pamoja, ukapenya kwenye mwili wa yule Mwisraeli na mwili wa yule mwanamke. Ndipo tauni dhidi ya Waisraeli ikakoma. Lakini wale waliokufa kwa hiyo tauni walikuwa watu elfu ishirini na nne.
10 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 11 “Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa kuhani Haruni, amegeuza hasira yangu mbali na Waisraeli, kwa sababu alikuwa na wivu kama nilio nao kwa heshima yangu miongoni mwao, hata kwamba kwa wivu wangu sikuwaangamiza. 12 Kwa hiyo mwambie Finehasi ninafanya agano langu la amani naye. 13 Yeye pamoja na wazao wake watakuwa na agano la ukuhani milele, kwa sababu alikuwa na wivu kwa ajili ya heshima ya Mungu wake, na akafanya upatanisho kwa Waisraeli.”
14 Jina la Mwisraeli ambaye aliuawa pamoja na mwanamke Mmidiani ni Zimri mwana wa Salu, kiongozi wa jamaa ya Simeoni. 15 Jina la mwanamke Mmidiani aliyeuawa ni Kozbi binti Suri, aliyekuwa mkuu wa kabila la jamaa ya Wamidiani.
16 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, 17 “Watendeeni Wamidiani kama adui na mwaue, 18 kwa sababu wao waliwatendea kama adui wakati waliwadanganya katika tukio la Peori na dada yao Kozbi, binti ya kiongozi Mmidiani, mwanamke ambaye aliuawa wakati tauni ilikuja kama matokeo ya tukio la Peori.”