35
Miji kwa ajili ya Walawi
Mwenyezi Mungu akamwambia Musa katika nchi tambarare ya Moabu, kando ya Mto Yordani kuvukia Yeriko, “Waagize Waisraeli kuwapa Walawi miji ya kuishi kutoka urithi ambao Waisraeli wataumiliki. Wape maeneo ya malisho kuzunguka hiyo miji. Kisha watakuwa na miji ya kuishi na maeneo ya malisho kwa ajili ya ng’ombe wao, mbuzi na kondoo wao, na mifugo yao mingine yote.
“Maeneo ya malisho kuzunguka miji hiyo ambayo mtawapa Walawi yataenea dhiraa elfu moja*Dhiraa 1,000 ni kama mita 450. kutoka ukuta wa miji. Nje ya mji, pima dhiraa elfu mbiliDhiraa 2,000 ni kama mita 900. upande wa mashariki, upande wa kusini dhiraa elfu mbili, upande wa magharibi dhiraa elfu mbili, na upande wa kaskazini dhiraa elfu mbili, na mji utakuwa katikati. Eneo hili litakuwa lao la malisho.
Miji ya makimbilio
(Kumbukumbu 19:1-13; Yoshua 20:1-9)
“Miji sita mtakayowapa Walawi itakuwa ya makimbilio, ambayo mtu anayemuua mwenzake aweza kukimbilia humo. Zaidi ya hiyo, wapeni miji mingine arobaini na mbili. Kwa jumla inawapasa kuwapa Walawi miji arobaini na nane, pamoja na maeneo ya malisho yao. Miji ambayo mtawapa Walawi kutoka nchi ambayo Waisraeli wanamiliki itatolewa kwa uwiano wa urithi wa kila kabila. Chukua miji mingi kutoka lile kabila lenye miji mingi, lakini uchukue miji michache kutoka kwa kabila lile lenye miji michache.”
Kisha Mwenyezi Mungu akamwambia Musa: 10 “Sema na Waisraeli, uwaambie: ‘Mtakapovuka Yordani kuingia Kanaani, 11 chagueni baadhi ya miji iwe miji yenu ya makimbilio, ambayo mtu ambaye ameua mwenzake bila kukusudia aweza kukimbilia humo. 12 Itakuwa mahali pa kukimbilia kutoka mlipiza kisasi, ili mtu aliyeshtakiwa kwa mauaji asife kabla ya kujitetea mbele ya mkutano. 13 Miji hii sita mtakayoitoa itakuwa miji yenu ya makimbilio. 14 Mtatoa miji mitatu ng’ambo hii ya Yordani na miji mingine mitatu upande wa Kanaani kama miji ya makimbilio. 15 Miji hii sita itakuwa mahali pa makimbilio kwa ajili ya Waisraeli, wageni na watu wengine wanaoishi kati yenu, ili mtu ambaye ameua mtu mwingine pasipo kukusudia aweze kukimbilia humo.
16 “ ‘Kama mtu akimpiga mwenzake kwa chuma naye mtu huyo akafa, mtu huyo ni muuaji; muuaji sharti atauawa. 17 Au kama mtu analo jiwe mkononi mwake, naye akampiga mwenzake nalo akafa, yeye ni muuaji; muuaji huyo sharti atauawa. 18 Au kama mtu ana chombo cha mti mkononi mwake ambacho chaweza kuua, naye akampiga mwenzake akafa, yeye ni muuaji; muuaji huyo sharti atauawa. 19 Mlipiza kisasi cha damu atamuua muuaji; wakati akikutana naye, atamuua. 20 Ikiwa mtu ana chuki ya siku nyingi na mwenzake akamsukuma au akamtupia kitu kwa kukusudia naye akafa, 21 au ikiwa katika uadui akampiga ngumi naye akafa, mtu yule sharti atauawa; yeye ni muuaji. Mlipiza kisasi cha damu atamuua muuaji atakapokutana naye.
22 “ ‘Lakini kama mtu akimsukuma mwenziwe ghafula pasipo chuki, au kumtupia kitu pasipo kukusudia, 23 au, pasipo kumwona, akimwangushia jiwe ambalo laweza kumuua naye akafa, basi kwa kuwa hakuwa adui yake naye hakukusudia kumuumiza, 24 kusanyiko lazima waamue kati yake na mlipiza kisasi wa damu kufuatana na sheria hizi. 25 Kusanyiko lazima wamlinde yule anayeshtakiwa kuua kutoka kwa mlipiza kisasi wa damu, na kumrudisha katika mji wa makimbilio alikokuwa amekimbilia. Lazima akae humo hadi atakapokufa kuhani mkuu aliyekuwa amepakwa mafuta matakatifu.
26 “ ‘Lakini kama mshtakiwa atatoka nje ya mipaka ya mji wa makimbilio ambao amekimbilia, 27 na mlipiza kisasi wa damu akamkuta nje ya mji, mlipiza kisasi wa damu anaweza kumuua mshtakiwa huyo bila kuwa na hatia ya kuua. 28 Mshtakiwa lazima akae katika mji wake wa makimbilio hadi atakapokufa kuhani mkuu; atarudi tu kwenye mali yake baada ya kifo cha kuhani mkuu.
29 “ ‘Hizi ndizo kanuni za sheria zitakazohitajiwa kwenu na katika vizazi vyenu vijavyo, popote mtakapoishi.
30 “ ‘Yeyote anayeua mtu atauawa kama muuaji ikiwa tu kuna ushuhuda wa mashahidi. Lakini hakuna mtu atakayeuawa kwa ushuhuda wa shahidi mmoja tu.
31 “ ‘Usikubali fidia yoyote ya kuokoa uhai wa muuaji ambaye anastahili kufa. Mtu huyo hakika lazima auawe.
32 “ ‘Usikubali fidia ya mtu ambaye amekimbilia katika mji wa makimbilio, na hivyo kumruhusu kurudi kuishi katika nchi yake kabla ya kifo cha kuhani mkuu.
33 “ ‘Msiinajisi nchi mnayoishi. Umwagaji damu hunajisi nchi, na upatanisho hauwezekani kufanyika katika nchi ambayo damu imemwagwa, isipokuwa tu kwa damu ya yule aliyeimwaga damu. 34 Msiinajisi nchi mnayoishi, ambayo nami ninakaa, kwa kuwa Mimi, Mwenyezi Mungu, ninakaa katikati ya Waisraeli.’ ”

*35:4 Dhiraa 1,000 ni kama mita 450.

35:5 Dhiraa 2,000 ni kama mita 900.