9
Makaribisho ya hekima na ya upumbavu 
  1 Hekima amejenga nyumba yake;  
amechonga nguzo zake saba.   
 2 Ameandaa nyama na kuchanganya divai yake;  
pia ameandaa meza yake.   
 3 Amewatuma wajakazi wake, naye huita  
kutoka mahali pa juu sana pa mji.   
 4 Anawaambia wale wasio na akili,  
“Wote ambao ni wajinga na waje hapa!   
 5 Njooni, mle chakula changu  
na mnywe divai niliyoichanganya.   
 6 Acheni njia zenu za ujinga nanyi mtaishi;  
tembeeni katika njia ya ufahamu.   
 7 “Yeyote anayemkosoa mwenye dhihaka  
hukaribisha matusi;  
yeyote anayekemea mtu mwovu  
hupatwa na matusi.   
 8 Usimkemee mwenye dhihaka, la sivyo atakuchukia;  
mkemee mwenye hekima naye atakupenda.   
 9 Mfundishe mtu mwenye hekima  
naye atakuwa na hekima zaidi;  
mfundishe mtu mwadilifu  
naye atazidi kufundishika.   
 10 “Kumcha Mwenyezi Mungu ndicho chanzo cha hekima,  
na kumjua Aliye Mtakatifu ni ufahamu.   
 11 Kwa maana kwa msaada wangu  
siku zako zitakuwa nyingi,  
na miaka itaongezwa katika maisha yako.   
 12 Kama wewe una hekima, hekima yako itakupa tuzo;  
kama wewe ni mtu wa mzaha,  
wewe mwenyewe ndiwe utateseka.”   
 13 Mwanamke aitwaye Mpumbavu ana kelele;  
hana adabu na hana maarifa.   
 14 Huketi kwenye mlango wa nyumba yake,  
kwenye kiti katika mahali pa juu sana pa mji,   
 15 akiita wale wanaopita karibu,  
wanaoenda moja kwa moja kwenye njia yao.   
 16 Anawaambia wale wasio na akili,  
“Wote ambao ni wajinga na waje hapa ndani!   
 17 Maji yaliyoibiwa ni matamu;  
chakula kinacholiwa sirini ni kitamu!”   
 18 Lakini hawajui hata kidogo kuwa wafu wako humo,  
kwamba wageni wake huyo mwanamke  
wako katika vilindi vya Kuzimu*Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol, yaani Shimo lisilo na mwisho..