16
Mipango ya moyoni ni ya mwanadamu,
bali jibu la ulimi hutoka kwa Mwenyezi Mungu.
 
Njia zote za mtu huonekana safi machoni pake mwenyewe,
bali makusudi hupimwa na Mwenyezi Mungu.
 
Mkabidhi Mwenyezi Mungu lolote ufanyalo,
nayo mipango yako itafanikiwa.
 
Mwenyezi Mungu hufanya kila kitu kwa kusudi lake mwenyewe;
hata waovu kwa siku ya maangamizi.
 
Mwenyezi Mungu huwachukia sana wote wenye kiburi cha moyo.
Uwe na hakika kwa hili: Hawataepuka kuadhibiwa.
 
Kwa upendo na uaminifu uovu huondolewa;
kwa kumcha Mwenyezi Mungu mtu hujiepusha na ubaya.
 
Njia za mtu zinapompendeza Mwenyezi Mungu,
huwafanya hata adui zake waishi naye kwa amani.
 
Afadhali kitu kidogo pamoja na haki
kuliko mapato mengi pamoja na udhalimu.
 
Moyo wa mtu huifikiri njia yake,
bali Mwenyezi Mungu huelekeza hatua zake.
 
10 Midomo ya mfalme huzungumza kwa hekima ya kiungu,
wala kinywa chake hakipotoshi haki.
 
11 Vipimo na mizani za halali hutoka kwa Mwenyezi Mungu;
mawe yote ya kupimia yaliyo katika mfuko ameyafanya yeye.
 
12 Wafalme huchukia sana kutenda maovu,
kwa maana kiti cha ufalme hufanywa imara kupitia haki.
 
13 Wafalme hufurahia midomo ya uaminifu;
humthamini mtu asemaye kweli.
 
14 Ghadhabu ya mfalme ni mjumbe wa mauti,
bali mtu mwenye hekima ataituliza.
 
15 Uso wa mfalme ung’aapo, inamaanisha uhai;
upendeleo wake ni kama wingu la mvua wakati wa vuli.
 
16 Ni bora kiasi gani kupata hekima kuliko dhahabu,
kuchagua ufahamu kuliko fedha!
 
17 Njia kuu ya wanyofu huepuka ubaya;
yeye aichungaye njia yake, huchunga maisha yake.
 
18 Kiburi hutangulia maangamizi,
roho ya majivuno hutangulia maanguko.
 
19 Ni afadhali kuwa na roho ya unyenyekevu
miongoni mwa walioteswa
kuliko kugawana nyara na wenye kiburi.
 
20 Yeyote anayekubali mafundisho hustawi,
tena amebarikiwa yeye anayemtumaini Mwenyezi Mungu.
 
21 Wenye hekima moyoni huitwa wenye ufahamu,
na maneno ya kupendeza huchochea mafundisho.
 
22 Ufahamu ni chemchemi ya uzima kwa wale walio nao,
bali upumbavu huleta adhabu kwa wapumbavu.
 
23 Moyo wa mtu mwenye hekima huongoza kinywa chake,
na midomo yake huchochea mafundisho.
 
24 Maneno ya kupendeza ni kama sega la asali,
ni matamu kwa nafsi na uponyaji kwenye mifupa.
 
25 Iko njia ionekanayo kuwa sawa kwa mtu,
bali mwisho wake huelekeza mautini.
 
26 Shauku ya mfanyakazi humhimiza kufanya kazi;
njaa yake humsukuma aendelee.
 
27 Mtu mbaya kabisa hupanga mabaya,
maneno yake ni kama moto uunguzao.
 
28 Mtu mpotovu huchochea ugomvi,
nayo maongezi ya upuzi huwatenganisha rafiki wa karibu.
 
29 Mtu mkali humvuta jirani yake
na kumwongoza katika mapito yale mabaya.
 
30 Yeye akonyezaye kwa jicho lake anapanga upotovu;
naye akazaye midomo yake amenuia mabaya.
 
31 Mvi ni taji la utukufu;
hupatikana kwa maisha ya uadilifu.
 
32 Ni afadhali mtu mstahimilivu kuliko shujaa,
mtu anayeitawala hasira yake kuliko yule autekaye mji.
 
33 Kura hupigwa kwa siri,
lakini kila uamuzi wake hutoka kwa Mwenyezi Mungu.