Zaburi
Kitabu cha Kwanza
1
(Zaburi 1–41)
Furaha ya kweli
Heri mtu yule ambaye haendi
katika shauri la watu waovu,
wala hasimami katika njia ya wenye dhambi,
au kuketi katika baraza la wenye mizaha.
Bali huifurahia Torati ya Mwenyezi Mungu,
naye huitafakari hiyo Torati usiku na mchana.
Mtu huyo ni kama mti uliopandwa
kando ya vijito vya maji,
ambao huzaa matunda kwa majira yake
na majani yake hayanyauki.
Lolote afanyalo hufanikiwa.
Huzuni ya waovu
Sivyo walivyo waovu!
Wao ni kama makapi
yanayopeperushwa na upepo.
Kwa hiyo waovu hawatastahimili hukumu,
wala wenye dhambi katika kusanyiko la wenye haki.
 
Kwa maana Mwenyezi Mungu huziangalia njia za mwenye haki,
bali njia za waovu zitaangamia.